Historia ya Kuzaliwa Kwa Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu ni nuru halisi ya ulimwengu inayowatia watu nuru; inang'aa gizani wala giza halikuiweza. Wachungaji wanawawakilisha maskini wa Israeli, watu wenye unyenyekevu wa ndani, wanaotambua na kuhisi udhaifu pamoja na unyonge wao katika maisha, kiasi cha kujiaminisha kwa wengine. Fadhila ya unyenyekevu ni muhimu katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Historia ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu ni muhimu sana katika kipindi hiki cha Maadhimisho ya Sherehe za Noeli. “Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng’ombe.” Lk 2:10-12. Wahusika wakuu hapa ni Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu mtu wa haki, waliokuwa wanatekeleza amri iliyotoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wote ulimwenguni. Maria na Yosefu toka mjini Nazareti wakapanda kwenda mjini Bethlehemu. Mara walipowasili wakatafuta mahali pa kujisetiri, kwa sababu Bikira Maria aliyekuwa amaposwa na Yosefu alikuwa na mimba. Lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kupata nafasi katika nyumba ya wageni, akalazimika kumzaa, Mwanawe, kifungua mimba, akamvisha nguo za kitoto. Akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe. Rej. Lk 2-1-7.

Hii ndiyo historia ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, ambaye hakupata hata mahali pa kuzaliwa. Mwinjili Yohane anasikitika kusema kwamba, alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Yn 1:11. Kristo Yesu kama sehemu ya masharti ya kumfuasa ni pamoja na kuacha yote kwa sababu hata Yeye hakuwa na mahali pa kujilaza kichwa chake. Rej. Lk 9:58. Malaika wa Bwana ndiye aliyetangaza habari njema ya furaha kuu kwa wachungaji waliokuwa kondeni wakilinda mifugo yao. Mamajusi kutoka Mashariki waliongozwa na nyota hadi wakafikia mahali alipozaliwa Mtoto Yesu. Kristo Yesu ni nuru halisi ya ulimwengu inayowatia watu nuru. Kristo Yesu ni nuru inayong’aa gizani wala giza halikuiweza. Wachungaji wanawawakilisha maskini wa Israeli, watu wenye unyenyekevu wa ndani, wanaotambua na kuhisi udhaifu pamoja na unyonge wao katika maisha, kiasi cha kujiaminisha kwa wengine. Wachungaji kondeni ndio watu wa kwanza kushuhudia kuzaliwa kwa Mtoto Yesu, tukio ambalo liliwaletea mabadiliko makubwa katika maisha yao, kiasi cha kurudi majumbani mwao, huku wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuona kama walivyoambiwa. Rej. Lk 2: 20.

Hii ni sehemu ya Katekesi ya Kipindi cha Noeli iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, Jumatano tarehe 22 Desemba 2021. Anaendelea kudadavua kwa kusema, Mtoto Yesu alikuwa amezungukwa na Mamajusi Rej. Mt 2:1-12. Lakini Wainjili hawataji majina yao wala vyeo vyao, bali hawa ni Mamajusi waliotoka Mashariki ya Mbali, mahali panapoweza kudhaniwa kuwa ni Mji wa Uajemi, Iran, Babel au Falme za Kiarabu. Mamajusi walifunga safari kwenda kumtafuta Mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa mjini Bethlehemu na walitaka kumwabudu. Kutoka katika undani wa nyoyo zao walimwona Mtoto Yesu kuwa ni Mungu, ndiyo maana walitaka kumwabudu. Mamajusi wanawawakilisha watu wale wasiomfahamu Mungu, “wapagani”, yaani ni wale watu ambao kwa karne nyingi wamefunga safari kumtafuta Mwenyezi Mungu katika maisha. Wanawawakilisha pia matajiri na wakuu wa dunia; watu wenye unyenyekevu wa moyo na wala si watumwa wa mali na utajiri wanao umiliki au kudhani kwamba, wana umiliki.

Ujumbe wa Injili ni wazi kwamba tukio la kuzaliwa kwa Kristo Yesu linawahusu watu wote. Lakini, ikumbukwe kwamba, unyenyekevu ni fadhila inayowaongoza waamini kumtambua Mwenyezi Mungu, kujitambua wao wenyewe na hivyo kuwakirimia mambo msingi katika maisha. Fadhila ya unyenyekevu ni msingi wa furaha ya kweli na ukweli wenyewe; ufahamu kuhusu Mungu na binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wake. Mamajusi walijinyenyekesha na hivyo kukirimiwa neema ya kuweza kumwona na kumtambua Kristo Yesu hata katika uchanga wake. Ni fadhila ya unyenyekevu iliyo wawezesha Mamajusi kufunga safari, kumtafuta, kuulizia habari zake, kiasi hata cha kutaka kupotea. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila mwamini kutoka katika sakafu ya moyo wake, anapewa mwaliko wa kumtafuta Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mwenyezi Mungu neema na baraka za kumtafuta, ili hatimaye, kumpenda daima, kama anavyofundisha Mtakatifu Anselmi. Pango la Noeli, liwasaidie kuona uwapo wa Mungu katika hali ya unyenyekevu.

Mtakatifu Paulo VI anasema, maskini wanapaswa kupendwa kwa sababu wao ni Sakramenti ya Kristo Yesu, anayewakilishwa na watu wenye njaa, wenye kiu, wageni na wakimbizi; waliouchi, wagonjwa na wafungwa. Mama Kanisa anawaalika waoto wake, kuwasaidia wote hawa kwa hali na mali; kuteseka pamoja nao sanjari na kufuata mfano wao bora, ili kuweza kuurithi Ufalme wa Mungu. Kiburi na majivuno, vitawafanya waamini kushindwa kumwona na kumsujudia Kristo Yesu na matokeo yake ni kuanza kujitafuta wenyewe. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa linaamini kwamba, kumkiri Mungu hakupingi hata kidogo hadhi ya binadamu, kwa vile hadhi hiyo husimikwa na kutimilizika katika Mwenyezi Mungu; maana binadamu hupokea kutoka kwa Mungu Muumba vipawa vya akili na uhuru; tena huwekwa kuwa huru katika jamii; lakini hasa huitwa kuungana na Mungu mwenyewe kama wana wake na kushiriki heri yake Yeye. Rej. Gaudium e spes, 21.

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha Katekesi yake kuhusu Tukio la Kuzaliwa kwa Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu, kwa kuwataka waamini kuhifadhi katika undani wa nyoyo ule wimbo wa sifa wakisema, “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu anawaowaridhia. Waamini watambue kwamba, Mwenyezi Mungu amekuwa wa kwanza kuwapenda, na hii ndiyo sababu ya furaha yao. Kwa watu wote, Baba Mtakatifu amewatakia Sherehe Njema za Noeli kwa Mwaka 2021. Kila mtu atambue na kuonja uwepo wa Mungu kati yao kwa njia ya unyenyekevu, ile kiu ya kumtafuta Mungu iwakirimie matumaini na upeo mpana wa mawazo.

Papa Historia ya Noeli
22 December 2021, 15:42

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >