Tafuta

Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha "Sacro Cuore, Jimbo Kuu la Milano kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake: Vipaumbele: Moto, Matumaini na Huduma. Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha "Sacro Cuore, Jimbo Kuu la Milano kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake: Vipaumbele: Moto, Matumaini na Huduma. 

Jubilei ya Miaka 100 ya Chuo Kikuu Cha Kikatoliki: Vipaumbele: Moto, Matumaini na Huduma

Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 19 Desemba 2021, kama sehemu ya uzinduzi wa Mwaka wa Masomo 2021-2022, sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 ya Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” Jimbo kuu la Milano amewatumia ujumbe huku akikazia mambo makuu matatu: Moto, Matumaini na Huduma. Miaka 100 ya Ushuhuda wa Imani tendaji kwa vijana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kunako mwaka 1919, watu watano mashuhuri akina Padre Agostino Gemelli, Ludovico Necchi, Francesco Olgiati, Armida Barelli pamoja na Ernesto Lombardo walianzisha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” “L'Università Cattolica del Sacro Cuore (UCSC) Jimbo kuu la Milano. Kilianza kufanya kazi rasmi tarehe 7 Desemba 1921 ili kujibu hitaji la mahali pa malezi na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya nchini Italia, changamoto iliyovaliwa njuga na matokeo yake Chuo hiki kimeendelea kukua na kupanuka na hatimaye, kuwa ni jukwaa la malezi na majiundo ya kielimu kitaifa na kimataifa! Ni kati ya vyuo vikuu vya kikatoliki maarufu sana Barani Ulaya. Kuna wanafunzi zaidi ya 43, 302 wanaopata elimu bora na makini inayokidhi viwango vya soko la ajira Barani Ulaya. Ni Chuo kikuu ambacho kimewekeza sana katika tafiti makini, ili kuendelea kusoma alama za nyakati na hivyo kujibu kilio cha watu wa Mungu. Haya ni matokeo ya sadaka kubwa ya akili na ukarimu inayotekelezwa na wadau wa Jumuiya ya Chuo kikuu, bila kusahau kwamba, wanafunzi wana imani na wanathamini sana mchango huu mkubwa unaotolewa na Mama Kanisa.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 19 Desemba 2021, kama sehemu ya uzinduzi wa Mwaka wa Masomo 2021-2022, sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 ya Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore”, amewatumia ujumbe kwa njia ya video akikazia mambo makuu matatu: Moto, Matumaini na Huduma. Maadhimisho haya yamehudhuriwa pia na Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen “European Commission” baada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuu Mario Delpini wa Jimbo kuu la Milano, Kaskazini mwa Italia. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake amekazia kuhusu “dhana ya moto” wa elimu ambao umewasha, kurithishwa na kushuhudiwa na wadau mbalimbali. Elimu ni njia makini ya kujenga utu wa binadamu. Huu ni urithi mkubwa wa kitamaduni na maisha ya kiroho unaotoa utambulisho wa Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore.” Kuelimisha maana yake ni kuwasha moto wa elimu unaoweza kushuhudiwa na mtu binafsi na jumuiya katika ujumla wake. Hii ni historia ya miaka 100 inayong’arishwa na imani, elimu, ujuzi na maarifa, tayari kujielekeza kwa siku za usoni! Baba Mtakatifu aendelea kufafanua kuhusu matumaini, ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, huo ni utamaduni wa kutupa.

Chuo kikuu ni mahali pa kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini sanjari na mchakato wa malezi mtambuka unaotekelezwa na wadau mbalimbali ndani ya jamii. Hii ni dhamana ya majaalimu wa Chuo kikuu, wanaopaswa kuhakikisha kwamba, moto huu unaendelea kuwaka hadi kieleweke. Elimu isaidie kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii, ili kujibu maswali msingi yanayotolewa na jamii, bila woga wala makunyanzi. Ukweli, uwazi na ukarimu ni amali za kijamii zinazopaswa kurithishwa kwa vijana wa kizazi kipya. Upyaisho wa mfumo wa elimu katika ulimwengu mamboleo utawasaidia watu wa Mungu kupambana na changamoto zinazojitokeza kwa wakati huu, ili kujenga leo na kesho yenye matumaini. Elimu ni upendo unaowajibisha na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, ili kuondokana na ubinafsi unaopelekea watu kutokuthaminiana. Kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano unaosimikwa katika kipaji cha kusikiliza, kujadiliana na maelewano. Mabadiliko ya mfumo wa elimu duniani yanapaswa kuwahusisha wadau mbalimbali katika sekta ya elimu, ili kuondokana na ukosefu wa haki jamii; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili hatimaye, kuweza kupambana na umaskini pamoja na tabia ya watu kutowajali wengine.

Baba Mtakatifu anasema, huu ni mchakato fungamanishi unaopania kujenga madaraja yanayowakutanisha watu, ili kuondokana na: ubinafsi na upweke hasi, kwa kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu anawataka wanafunzi hasa katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kutokubali kupokwa matumaini na wajanja wachache ndani ya jamii wala kumezwa na tabia ya uchoyo na ubinafsi. Chuo Kikuu kiwe ni mahali pa kugundua umoja na tofauti msingi; mahali pa kumwilisha karama kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Jubilei ya Miaka 100 ya Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” iwe ni fursa ya kukua, kukomaa na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Chuo kikuu ni mahali pa kuwafunda vijana wa kizazi kipya kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma. Huu ni ushuhuda unatolewa na wadau mbalimbali chuoni hapo katika tafiti makini, dhamana na wajibu kitaifa na kimataifa bila kuwasahu wafanyakazi wote wanaojisadaka ili kuhakikisha kwamba, maisha na shughuli mbalimbali chuoni hapo zinasonga mbele, sawa na vyombo vya muziki vinavyounganishwa na kutoa muziki unaopendeza.

Baba Mtakatifu mwishoni mwa ujumbe wake, anawataka pia wawe waaminifu kwa tunu msingi za Kiinjili, daima wakijitahidi kumfuasa Kristo aliyejisadaka Msalabani, kielelezo cha Hekima ya Mungu iliyotundikwa Msalabani. Kuhudumia maana yake ni kutawala. Kumbe, wale wote wanaopata elimu na ujuzi chuoni hapo wanapaswa kushiriki kikamilifu katika utume wa kuelimisha kwa ujasiri, uvumilivu sanjari na kukabiliana na changamoto mbalimbali kwa amani na utulivu wa ndani. Uvumilivu uwe ni kwa ajili ya huduma kwa jamii na Kanisa katika ujumla wake. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 28 Novemba 2019 alizindua Mwaka wa Masomo wa Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” sanjari na uzinduzi wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 kwa mwaka 2020-2021 na kukazia umuhimu wa Chuo kikuu cha Kikatoliki kujikita katika diplomasia kwa ajili ya ujenzi wa amani duniani.

Mama Kanisa anapenda kujielekeza zaidi katika sekta ya elimu ili kuwasaidia wanafunzi kupata elimu bora, ujuzi na maarifa pamoja na kuhakikisha kwamba, Chuo Kikuu cha Kikatoliki, mara kwa mara kinapima mafanikio, matatizo na changamoto zinazojitokeza. Lengo ni kukiwezesha kuchangia katika mchakato wa maendeleo fungamani, ukuaji wa uchumi, majiundo makini pamoja na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni katika muktadha huu, Chuo Kikuu cha Kikatoliki kinapaswa kujielekeza zaidi katika kutoa nadharia ambayo inamwilishwa katika vitendo. Kwa kutambua changamoto zilizoko mbele yao na hivyo kutafuta nyenzo zitakazosaidia kupambana na matatizo pamoja na changamoto hizi ili hatimaye, suluhu ya kudumu iweze kupatikana kwa njia ya masomo yanayowapatia ujuzi, weledi na maarifa yanayotokana na tafiti makini za kisayansi.

Chuo Kikuu cha Kikatoliki
21 December 2021, 14:39