Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani 1 Desemba 2021: Mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani 1 Desemba 2021: Mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. 

Siku ya Ukimwi Duniani 2021: Mshikamano wa Udugu wa Kibinadamu

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kujikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata tiba muafaka katika hali ya usawa na ubora dhidi ya Ugonjwa wa UKIMWI. Vijana wanapaswa kuwa makini zaidi kwani ni waathirika wakuu zaidi! UKIMWI!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, tarehe 1 Desemba 2021, ametoa wito kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwakumbuka, kuwaombea na kuwasaidia watu ambao wameathirika kutokana na Ugonjwa wa UKIMWI sehemu mbalimbali za dunia. Kuna baadhi ya maeneo ya dunia, wagonjwa wengi hawawezi kupata dawa za kurefusha maisha au hata kupata tiba muafaka kwa magonjwa nyemelezi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya ya Kimataifa, kwa mara nyingine tena, itaweza kujikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata tiba muafaka katika hali ya usawa na ubora dhidi ya Ugonjwa wa UKIMWI.

Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kwa Mwaka 2021 yamemogeshwa na kauli mbiu “Zingatia Usawa. Tokomeza UKIMWI, Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko.” Huu ni mwaliko kwa watu kujitokeza kupima kwa hiyari na kwa wale walioathirika kuanza mara moja kutumia dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi. Vijana wanapaswa kuwa makini zaidi kwa sababu wao ni tegemeo kubwa la nguvu kazi ya Kanisa na Mataifa yao katika ujumla wake. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko aliwapongeza watawa na waamini walei ambao wamesadaka maisha na taaluma zao kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa Ugonjwa wa UKIMWI tangu ulipoanza kujitokeza kati ya Miaka 1980 na Miaka 1990, wakati ambapo kiwango cha vifo vya wagonjwa wa UKIMWI kilikuwa ni sawa na asilimia 100%.

Baba Mtakatifu anasema, kuna Mapadre, Watawa na Waamini walei walioamua kusadaka maisha yao kwa ajili ya kuwasindikiza na kuwasaidia waathirika wa Ugonjwa wa UKIMWI, kama kielelezo cha ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu badala ya kuwageuzia kisogo. Huduma kwa wagonjwa na waathirika wa UKIMWI ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa kwa waathirika na wagonjwa wa UKIMWI. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa. Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umesema jamii ikiwa ni pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali, asasi za kiraia na wanaharakati wanao mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa UKIMWI.

Ukimwi Duniani

 

01 December 2021, 14:37