Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Makardinali katika salam na matashi mema ya Noeli kwa Papa Francisko amegusia mambo muhimu yaliyojitokeza katika utume wa Papa Francisko kwa Mwaka 2021 Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Makardinali katika salam na matashi mema ya Noeli kwa Papa Francisko amegusia mambo muhimu yaliyojitokeza katika utume wa Papa Francisko kwa Mwaka 2021 

Muhtasari wa Matukio Makuu ya Utume wa Papa Francisko 2021

Kardinali Giovanni Battista Re katika hotuba yake amegusia matukio makuu yaliyojiri katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwaka 2021 sanjari na kumtakia heri na baraka kwa Sherehe za Noeli na Mwaka Mpya 2022. Hija za Kichungaji: Iraq, Hungaria, Slovakia, Cyprus na Ugiriki zilipania kudumisha: Majadiliano ya Kidini, Kiekumene, Utu na Heshima ya Binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali kwa niaba ya Makardinali, Maaskofu na Jumuiya ya wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican, “Curia Roma” Jumanne, tarehe 23 Desemba 2021, kama sehemu ya salam na matashi mema katika Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2021 amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kujilia Kanisa kumpata Baba Mtakatifu Francisko kama zawadi kwa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Hata katika kipindi hiki, watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia, wanaendelea kuteseka kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake, ameendelea kuwa ni rejea inayotoa mwanga angavu, msaada na faraja kwa watu wanaoteseka kiroho na kimwili. Kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021, Baba Mtakatifu Francisko alifanya hija ya kitume nchini Iraq, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Hija za kitume ni muhimu sana katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni nyenzo ya majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi na Serikali mbalimbali duniani.

Ni fursa ya kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene, kitamaduni na kisiasa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vatican inapenda kuheshimu Mikataba na Itifaki mbalimbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ilikuwa ni fursa ya kukutana na kuzungumza mubashara na Ayatollah Ali Sistani ambaye ni kiongozi mkuu wa kiroho na kisiasa nchini Iraq. Ilikuwa ni fursa ya kumwilisha kwa vitendo Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Hija hii ya kitume, itabaki imechapwa katika akili na nyoyo za watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Malengo ya Waraka wa Kitume, "Fratelli tutti" ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na mioyo ya watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) kuanzia tarehe 5-12 Septemba 2021, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Ilikuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu Francisko kuimarisha imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mungu nchini Hungaria.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cyprus kuanzia tarehe 2-4 Desemba 2021 ilinogeshwa na kauli mbiu “Tufarijiane Katika Imani”. Baba Mtakatifu katika hija hii ya kitume anapenda kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kufarijiana katika imani, kama sehemu ya nyenzo muhimu katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano, ujenzi wa madaraja ya watu kukutana sanjari na ukarimu; amali za jamii nchini Cyprus. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 4-6 Desemba 2021 alifanya hija ya kitume nchini Ugiriki kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Jiwekeni Wazi Kwa Mshangao wa Mungu.” Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali anasema, hija hii inaweza kufupishwa kwa kusema kwamba, ilijikita zaidi katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, majadiliano ya kiekumene; huduma makini kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kuanzia Oktoba 2021-Oktoba 2023 yanayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Awamu ya kwanza ni kwa ajili ya Makanisa mahalia pamoja na taasisi zote zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki ni kuanzia tarehe 17 Mwezi Oktoba 2021 hadi 15 Agosti 2022. Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ni kuanzia Mwezi Septemba 2022 hadi Machi 2023. Awamu ya Tatu, Kanisa la Kiulimwengu ni kuanzia mwezi Oktoba 2023. Lengo kuu ni kujenga utamaduni wa kusikilizana, kujadiliana, kung’amua na hatimaye, watu wote wa Mungu kutekeleza kwa pamoja. Hiki ni kipindi kusali, kutafakari Neno la Mungu na kusikilizana, ili kupyaisha maisha ya kimaadili na kiroho kwa njia ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Mwishoni, amemtakia Baba Mtakatifu Francisko heri na baraka kwa Sherehe za Noeli kwa mwaka 2021.

Kardinali Re

 

 

23 December 2021, 15:27