Mwitikio wa Mabaraza ya Maaskofu Kwa Ajili ya Wahamiaji na Wakimbizi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake tarehe 5 Desemba 2021 alipotembelea kambi ya wakimbizi wa Lesvos nchini Ugiriki alikazia kuhusu: Utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji na kwamba, hii ni changamoto inayopaswa kushughuliwa na wote. Miaka mitano imegota, lakini hali ya wakimbizi na wahamiaji inazidi kuwa mbaya zaidi kila kukicha, kiasi kwamba, haya ni mazingira ambayo hayafai kwa maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu alitajapia tunu na amali za jamii zinazosigana kiasi kwamba, leo hii Bahari ya Mediterrania imekuwa ni “Bahari ya Kifo”: “Mare mortuum”, changamoto na mwaliko wa kujenga na kudumisha Injili ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Huu ni wakati wa kuona ukweli kwa macho makavu na kuwajibika kikamilifu bila kuwarushia wengine changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Kinachozingatiwa hapa ni utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi kuwa kama kipimo kwa mambo yote. Miaka mitano imegota tangu viongozi wakuu wa Makanisa walipotembelea Kisiwa cha Lesvos na kujionea hali halisi ya wakimbizi na wahamiaji, lakini hali bado imebaki vile vile kama ilivyokuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Baba Mtakatifu alitumia fursa hii, kuwashuruku wadau wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Kwa hakika nchi ya Ugiriki imeelemewa na wimbi kubwa la wakimbizi na inaonekana kana kwamba, kwa baadhi ya nchi za Ulaya hili si tatizo linalowahusu. Inasikitisha kuona kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanaishi katika mazingira yasiyofaa kabisa na badala yake, serikali zinaomba fedha kwa ajili ya kujenga kuta za nyaya za umeme ili kudhibiti wimbi la wakimbizi na wahamiaji Barani Ulaya. Ni katika muktadha huu, kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu wakati wa Katekesi yake kuhusu Historia ya Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Jumatano tarehe 22 Desemba 2021 ametoa wito kwa viongozi wa Mabaraza ya Maaskofu, viongozi wa Makanisa mahalia pamoja na taasisi mbalimbali zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki kuonesha ukarimu, upendo na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi.
Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linahitaji jibu la pamoja kwa sababu hii ni changamoto ya Kimataifa. Baba Mtakatifu amewashuruku viongozi wa Serikali ya Italia ambao wameruhusu baadhi ya wakimbizi na wahamiaji kurejea na Baba Mtakatifu Francisko baada ya hija yake ya Kitume nchini Cyprus na Ugiriki na hii ni changamoto pevu kwa Nchi za Ulaya kutenda kwa haki. Kanisa litaendelea kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji hawa. Baba Mtakatifu amewapongeza wale wote ambao wamejitokeza kuunga mkono jitihada hizi kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Taarifa zinaonesha kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Slovakia tayari limekwisha kuwapokea wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Ni wakati muafaka wa kutafakari kuhusu biashara haramu ya silaha duniani, mashambulizi ya silaha pamoja na sera na mikakati ya kisiasa na kiuchumi inayokwenda kinyume cha haki, usawa, amani na maendeleo fungamani ya binadamu. Huu ni wakati wa kutafuta suluhu ya kweli katika migogoro ya kivita; kushikamana kwa ajili ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Utu, heshima na haki msingi za binadamu ziwe ni kipimo cha Sherehe za Noeli kwa mwaka 2021.
Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linasema, Caritas Poland itajielekeza zaidi kutoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Huu ni wakati muafaka kwa Poland kutekeza kwa vitendo sera hii. Wakati huo huo, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, COMECE linasema, linaunga mkono juhudi za Baba Mtakatifu katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji kama kielelezo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Waamini wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa wakimbizi na wahamiaji. Huu ndio msimamo pia uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani, linalotaka kuwapokea wakimbizi na wahamiaji kama kielelezo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kuwatendea, huku wakizingatia utu, heshima na haki zao msingi. Kwa upande wake, Shirika la Wayesuit la kuhudumia Wakimbizi, JRS linasema, litaendelea kusimama kidete kuwasindikiza, kuwahudumia na kuwatetea wakimbizi na wahamiaji kama kielelezo cha ukarimu, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.