Tafuta

Papa Francisko ameadhimisha Sherehe ya Bikira Maria kwa kutoa heshima yake kwa Sanamu ya Bikira Maria iliyowekwa kwenye Uwanja wa Spagna, Roma na kusali kwa ajili ya watu wa Mungu. Papa Francisko ameadhimisha Sherehe ya Bikira Maria kwa kutoa heshima yake kwa Sanamu ya Bikira Maria iliyowekwa kwenye Uwanja wa Spagna, Roma na kusali kwa ajili ya watu wa Mungu. 

Papa Francisko: Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili

Papa amewaombea wote wanaoteseka kwa vita na kinzani pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Amewaombea watu toba na wongofu wa ndani, ili watu watubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa kuondoa ndani mwao moyo wa jiwe. Amewakumbuka pia wale wote wanaojenga kuta za utengano, waguswe na mateso na mahangiko ya wengine! Moyo wa Jiwe Hatari!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, tarehe 8 Desemba 2021, asubuhi na mapema alikwenda kwenye Uwanja wa Spagna, mjini Roma ili kutoa heshima zake kwa Sanamu ya Bikira Maria inayoheshimiwa sana na familia ya Mungu mjini Roma. Kwa mwaka huu, Baba Mtakatifu ameamua kutoa heshima zake kwa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kwa faragha, tofauti na miaka mingine. Baada ya kusali na kuwaombea watu wa Mungu, wakati ambapo mji wa Roma ulikuwa bado ni giza, aliweka shada la maua meupe na kuwaombea watu wa Mungu katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baba Mtakatifu amewaombea watu wote wanaoteseka kwa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Amewaombea watu toba na wongofu wa ndani, ili watu watubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa kuondoa ndani mwao moyo wa jiwe. Amewakumbuka pia wale wote wanaojenga kuta za utengano, waguswe na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wengine.

Baadaye, Baba Mtakatifu amekwenda moja kwa moja hadi kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu Jimbo kuuu la Roma, kutoa heshima zake kwa Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani.” Saa 1:00 kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko alikuwa amerejea tayari mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, tangu mwaka 1953, viongozi wakuu wa Kanisa wamekuwa wakienda kutoa heshima zao kwa Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Bikira Maria alipata upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyemkirimia karama na neema nyingi ili aweze kuwa ni Mama wa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu. Karne kwa karne Mama Kanisa ametambua kwamba, Bikira Maria aliyejazwa neema na Mwenyezi Mungu, alikombolewa tangu mwanzo alipotungwa mimba! Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba 1854 akatangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria!

Papa Piazza Spagna
08 December 2021, 15:20