Tafuta

Papa Francisko, Sherehe za Noeli ni kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Papa Francisko, Sherehe za Noeli ni kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. 

Sherehe za Noeli ni Kielelezo Cha Huruma na Upendo wa Mungu

Sherehe za Noeli ziwakumbushe waamini na watu wote wenye mapenzi mema upendo na huruma ya Mungu iliyomfanya Neno wa Mungu akatwaa mwili na kukaa kati ya waja wake. Changamoto ni kwa waamini kumfungulia Kristo Yesu, malango ya nyoyo zao, ili Kristo Yesu aweze kupata maskani katika uhalisia wa maisha yao; katika nyumba, familia na mahali pa kazi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake kuhusu historia ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu, Jumatano tarehe 22 Desemba 2021 anasema, hili ni tukio muhimu sana linalowagusa na kuwaambata watu wote kama inavyojidhihirisha katika simulizi za Injili. Sherehe za Noeli ziwakumbushe waamini na watu wote wenye mapenzi mema upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka, iliyomfanya Neno wa Mungu akatwaa mwili na kukaa kati ya waja wake. Changamoto kwa wakati huu ni kwa waamini kumfungulia Kristo Yesu, malango ya nyoyo zao, ili Kristo Yesu aweze kupata maskani katika uhalisia wa maisha yao; katika nyumba, familia na mahali pa kazi. Sherehe za Noeli ni mwaliko wa kujikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, lakini inapendeza ikiwa kama kipaumbele cha kwanza kitatolewa kwa maskini, wagonjwa, wazee na wahitaji zaidi, kwani kwa kutenda hivyo, ni sawa na kumhudumia Kristo Yesu, ambaye amejifananisha na kujitambulisha nao!

Baba Mtakatifu anawaalika kwa namna ya pekee, vijana kujibidiisha kumtafuta Mwenyezi Mungu katika maisha yao, lakini watambue kwamba, Mwenyezi Mungu amejifunua kama mwingi wa huruma na mapendo kwa njia ya Uso wa Kristo Yesu. Noeli ni muda muafaka wa kutafuta: furaha ya kweli, amani na maridhiano kwani amani ni zawadi kubwa inayotolewa na Mwenyezi Mungu wakati huu wa Kipindi cha Noeli. Upendo wa Mungu usambae na kukita mizizi yake katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu, lakini zaidi anasema Baba Mtakatifu Francisko ukite mizizi yake katika familia, kwa sababu Noeli ni Sherehe kubwa ya familia. Watu kutoka sehemu mbalimbali wanakutana katika Kipindi cha Noeli, kumshukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake wa daima. Ni muda wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Lakini, watu wanapaswa kukumbuka kwamba, bado kuna maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kumbe, hii ni fursa ya kuendelea kumwomba, Mtoto Yesu ili aweze kuwalinda na kuwaokoa na Ugonjwa wa UVIKO-19. Awalinde dhidi ya mabaya yote katika maisha. Waamini wajiandae zaidi kiroho, ili kuweza kumpokea Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu. Iwe ni fursa ya kuutambua Umungu wa Mtoto Yesu aliyezaliwa katika mazingira duni, ili awakirimie neema na wokovu.

Noeli

 

22 December 2021, 14:59