Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Vijana Nchi Takatifu: Msiikimbie Nchi Yenu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya Kitume ya 35 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Cyprus kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 4 Desemba 2021 ilinogeshwa na kauli mbiu “Tufarijiane Katika Imani.” Akiwa nchini Cyprus, Baba Mtakatifu aliandaa ujumbe kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya Nchi Takatifu na kwa namna ya pekee vijana kutoka mjini Bethlehemu, akiwashauri kukita mizizi ya maisha yao katika Nchi Takatifu, mahali ambapo Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu alipozaliwa. Kamwe wasikate wala kukatishwa tamaa, bali wawe na mtazamo na mwelekeo mpana zaidi katika maisha yao kwani kamwe Mwenyezi Mungu hawezi kuwahadaa watu wake hata kidogo! Na kwa njia hii, wanaweza kutenda mambo makuu katika maisha yao. Baba Mtakatifu katika salam zake kwa vijana aliwahakikishia kwamba, yuko karibu nao. Nchi Takatifu ni mahali pa hija ya maisha ya kiroho, lakini kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO -19, watu wameteseka sana. Wakati mwingine inakuwa ni vigumu kwa vijana kuamua ni kitu gani cha kutenda, kiasi cha kujikatia tamaa ya maisha kwa kuona kwamba nchini mwao hakuna msaada wowote, kiasi cha kuona kwamba, hakuna matumaini kwa siku za usoni. Wazo kuu kwa vijana wengi ni kuikimbia nchi yao ili kutafuta maisha bora zaidi ughaibuni. Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ni mawazo potofu.
Vijana wanapaswa kuwa na mawazo na mwelekeo mpana zaidi, kwa kuwa na mawazo chanya, yatakayowawezesha kubaki katika Nchi yao, ili hatimaye, waweze kupokea ahadi za Mwenyezi Mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu hawezi kamwe kuwahadaa kama yalivyopia matumaini. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kuonesha uzalendo kwa kujikita katika nchi na historia ya maisha yao, ili kusongesha mbele wito ambao Mwenyezi Mungu katika huruma na upendo wake, amewakirimia. Kamwe wasipoteze ile ndoto ya ujenzi wa nchi na maendeleo ya watu wao ili hatimaye, kuzamisha mizizi katika amali na utajiri wa kitamaduni na maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anakiri wazi kwamba, “si lelemama wala maji kwa glasi” kijana kujiundia familia, lakini hata katika muktadha huu, vijana hawana sababu ya kukata wala kujikatia tamaa ya matumaini, kwani matumaini hayawezi kumwadaha mtu. Katika mkesha wa Noeli, ni mtu gani ambaye angefikiri kwamba, yule Mtoto mchanga aliyezaliwa kule mjini Bethlehemu angekuwa ni Mtoto wa Mungu?
Mamajusi kutoka Mashariki ya Mbali walikuwa wamekwisha kupata mang’amuzi haya kutokana na utaalamu wao wa nyota, kiasi cha kuthubutu kuhatarisha maisha yao kwa kufunga safari kwenye kumtafuta Mfalme wa Wayahudi. Baba Mtakatifu anakaza kusema hata katikati ya umaskini, nyakati za vita na ukosefu wa uhuru, angalieni Pango la Noeli alimolazwa mtoto Yesu. Hata vijana katika hali ya umaskini wao, bado wana uwezo wa kufanya makubwa zaidi na Mwenyezi Mungu atabariki juhudi zao. Baba Mtakatifu anawatakia vijana wote Noeli Njema.