Hati ya Udugu wa Kibinadamu: Haki, Amani Na Utulivu Msumbiji
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu walitia mkwaju kwenye “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu.” Hii ni changamoto kwa waamini wa dini mbalimbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema majadiliano ya kidini si alama ya udhaifu, bali ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Majadiliano ya kidini hayana mbadala, kwani waamini wa dini zote wanapaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha utamaduni wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, ili hatimaye, familia ya binadamu iweze kukua na kukomaa katika mchakato wa upatanisho, kwa kuwakirimia watu matumaini yanayobubujika kutoka katika huduma ya upendo. Dini mbalimbali duniani zina uwezo wa kujenga utamaduni wa kuwakutanisha watu ili kuimarisha umoja na udugu wa kibinadamu. Hati hii ni kikolezo cha ujenzi wa misingi ya usawa, haki, amani na maridhiano duniani. Waamini wa dini mbalimbali wanapaswa kushikamana ili kulinda na kuendeleza mazingira nyumba ya wote; kudumisha haki msingi za binadamu; kwa kutoa majibu muafaka dhidi ya vita, kinzani na migogoro sehemu mbalimbali za dunia. Waamini na watu wenye mapenzi mema wakishirikiana kwa dhati wanaweza kukomesha pia vita, rushwa na ufisadi; kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema; kwa kubainisha na kutekeleza sera na mikakati ya uchumi fungamani pamoja na kuwakirimia watu wa Mungu matumaini katika hija ya maisha yao.
Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu inakazia pamoja na mambo mengine, ujenzi wa utamaduni wa majadiliano ya kidini; umuhimu wa waamini wa dini mbalimbali kufahamiana, ili kushirikiana na kushikamana, kwa kutambua na kuheshimu tofauti zao msingi. Udugu wa kibinadamu ni sehemu ya utu wa mwanadamu unaowasukuma watu wa Mataifa kusumbukiana katika maisha na kusimikwa katika matendo. Lengo ni kuondokana na vizingiti vinavyowatenganisha watu kwa misingi ya udini pamoja na vita vya kidini. Hii ni changamoto ya kushikamana ili kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu sehemu mbalimbali za dunia. Ikumbukwe kwamba, majadiliano ya kidini yanapata chimbuko lake katika majadiliano kati ya Mungu na waja wake. Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu itaendelea kupokelewa kwa mikono miwili na Jumuiya ya Kimataifa, ili kujenga jamii stahimilivu inayosimikwa katika misingi ya haki, amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Ni katika muktadha huu, hivi karibuni viongozi wa kidini kutoka katika mkoa wa Cabo Delgado nchini Msumbiji, walikutana ili kutafakari kwa pamoja “Mchango wa dini kama suluhu ya kinzani mkoani Cabo Delgado”, Pemba. Huu ni mkoa ambao kwa miaka ya hivi karibuni umegeuka kuwa ni uwanja wa vita na vurugu kutokana na kukithiri vitendo vya kigaidi pamoja na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hali tete inachangiwa pia na ukosefu wa usawa wa kijamii; kiwango kikubwa cha watu wasiojua kusoma na kuandika; kuporomoka kwa tunu msingi za kimaadili na kiutu; udini na ukabila ni kati ya mambo ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kusiginwa kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Viongozi wa kidini kutoka Mkoa wa Cabo Delgato katika tamko la Pemba wanasema wanapenda kujenga mshikamano wa nguvu ili kukabiliana na changamoto za vitendo vya kigaidi vinavyotishia haki na amani, ili kudumisha amani na udugu wa kibinadamu. Wanataka kuendeleza maana halisi ya dini ili kudumisha amani na hatimaye, kuondokana na maamuzi mbele na waathiarika wakuu hapa ni waamini wa dini ya Kiislam. Watu watambue kwamba, lengo kuu la dini ni kuwawezesha watu wa Mungu kupata furaha na amani ya kweli na upatanisho kwa kuondokana na vitendo vinavyovunja amani, ili hatimaye, kuanza kuaminiana na kuheshimiana kama ndugu wamoja.
Huu ni mwaliko wa kukuza majadilino ya kidini yanayosimikwa katika: ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini wa dini mbalimbali wajenge madaraja yanayowakutanisha waamini wao, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja licha ya tofauti zao msingi, kumbe, wanapaswa kusimama kidete kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu. Waamini wafundishwe sayansi ya kutafsiri vitabu vitukufu, ili kupata tafsiri ya kweli. Vijana waelimishwe umuhimu wa kudumisha amani kwa kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani; ili kwa pamoja waweze kupata amani ya kudumu. Watu wa Mungu nchini Msumbiji wapewe ushauri nasaha ili kukabiliana na changamoto na athari za vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu muda mrefu nchini Msumbiji, ili hatimaye kukoleza mchakato wa upatanisho na ushiriki wao wa kijamii. Viongozi hao wanasema umefika wakati wa kushirikiana na Serikali, taasisi pamoja na watu wenye mapenzi mema, ili kusaidia mchakato wa uanzishaji wa amani ya kudumu mkoani Cabo Delgado na hatimaye Msumbiji nzima.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 10 Januari 2022 amekutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican kama sehemu ya utamaduni wa kutakiana matashi mema mwanzoni mwa mwaka mpya wa 2022. Pamoja na mambo mengine, amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujenga utamaduni wa majadiliano na udugu wa kibinadamu, ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Kumbe, kuna haja ya: kuheshimiana na kuaminiana; Kusikilizana na kushirikishana mawazo na mang’amuzi katika ukweli na uwazi, ili hatimaye, kuweza kufikia muafaka, utakaotekelezwa na wahusika wote katika ujumla wao.