Papa Francisko Juma la 55 ya Kuombea Umoja wa Wakristo: Kipaumbele ni Uekumene wa wa Injili ya upendo, huduma na ukarimu kwa watu wa Mungu. Papa Francisko Juma la 55 ya Kuombea Umoja wa Wakristo: Kipaumbele ni Uekumene wa wa Injili ya upendo, huduma na ukarimu kwa watu wa Mungu. 

Juma la 55 la Kuombea Umoja wa Wakristo: Huruma, Upendo na Huduma

Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo kuondokana na tabia ya ubaguzi, chuki, uhasama na kinzani na badala yake, wajielekeze zaidi katika mchakato wa ujenzi na ushuhuda wa Injili ya huruma, upendo na huduma, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake. ili hatimaye, matunda ya amani, ushirikiano na umoja uweze kutangazwa na kushuhudiwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Juma la 55 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18-25 Januari 2022 linanogeshwa na kauli mbiu “Tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Mt 2:2. Tafakari ya kuombea umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2022 imeandaliwa na Baraza la Makanisa Mashariki ya Kati na linahitimishwa kwa Sikukuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa hapo tarehe 25 Januari 2022 kwa Masifu ya Jioni yatakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko. Hili ni tukio linalonogeshwa na majadiliano ya kiekumene, yaani majadiliano kati ya Makanisa ya Kikristo na Madhehebu ya Kikristo, ili Wakristo wote waweze kuwa wamoja chini ya Kristo Yesu, Mchungaji mkuu.

Majadiliano ya kiekumene anasema Baba Mtakatifu yanawahusu watu wa imani moja kwa Kristo Yesu kutoka kwa watu wa Mataifa mbalimbali, lugha, jamaa na kabila. Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo kuondokana na tabia ya ubaguzi, chuki, uhasama na kinzani na badala yake, wajielekeze zaidi katika mchakato wa ujenzi na ushuhuda wa Injili ya huruma, upendo na huduma, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake. Wakristo wa Makanisa na Madhehebu yote, waunganike kwa pamoja katika jina la Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, ili hatimaye, matunda ya amani, ushirikiano na umoja uweze kutangazwa na kushuhudiwa katika familia, jamaa, ndugu na marafiki.

Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo wote kushiriki katika sala kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo, ili Wakristo wote waweze kujikita katika hija ya umoja wa wafuasi wa Kristo Yesu na hatimaye, siku moja, waweze kuwa chini ya Kristo Yesu, Mchungaji mwema. Uekumene wa sala ni dhamana na wajibu wa kila mbatizwa, ndiyo maana Kristo Yesu katika sala yake ya Kikuhani, anawahimiza kuwa wamoja kama wao walivyo wamoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ni kwa njia hii, Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema wataweza kuonja kwa karibu zaidi katika maisha yao: huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka!

Umoja wa Wakristo

 

19 January 2022, 15:29