Papa Francisko:Mama wa Mungu ni mfano wa mama wengi duniani
Na Sr. Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Jumamosi tarehe Mosi Januari 2022 katika Siku Kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, sambamba na siku ya ya Amani duniani. Kanisa likiwa na waamini waleI, makardinali, maaskofu, mapadre na watawa, Baba Mtakatifu Francisko ametoa mahubiri yake kwa kusema kuwa: Wachungaji walikwenda kwa haraka wakamkuta Maria na Yosefu, na yule mtoto mchanga amelala horini (Lk 2, 16). Hori ni ishara ya furaha kwa wachungaji. Ni uthibitisho wa kile walichosikia kutoka kwa Malaika (Lk 2,12) ni mahali ambapo walimkuta Mwokozi. Na pia ni jaribu ambalo Mungu alikuwa karibu yao; amezaliwa horini, ni jambao ambalo lilikuwa tayari linajulikana sana kwa kuonesha namna alivyo karibu nao na kifamilia. Lakini pia horini ni ishara ya furaha hata kwetu sisi. Yesu anatugusa moyo kwa kuzaliwa mdogo na maskini, anatupatia upendo badala ya woga.
Hori linatuonesha sisi kuwa litakua chakula chetu. Na umaskini wake unakuwa habari njema kwa ajili ya wote, hasa kwa wale ambao wako pembeni, waliokataliwa, kwa wale ambao dunia haiwajali. Mungu anakuja pale, hakuna njia nyingine ya upendo na wala mahali pa kutunzia! Kutunza ndiyo uzuri wa kumwona akiwa amelala katika hori. Lakini kwa upande wa Maria mama wa Mungu haikuwa namna hivyo. Yeye alistahimili kashfa la hori. Hata yeye kabla ya wachungaji, alikuwa amepata tangazo kutoka kwa Malaika, ambaye alikuwa amemwambia maneno makuu, akizungumzia kiti cha Daudi:“Utachukua mimba ya mtoto na utamwita Yesu. Atakuwa Mkubwa na ataitwa Mwana wa aliye juu: Bwana Mungu atamweka katika Kiti cha Daudi Baba yake (Lk 31-32). Na sasa anapaswa amlaze kwenye hori la wanyama. Je ni jinsi gani ya kuweka mambo haya mawili: ya kiti cha Mfalme na hori maskini? Baba Mtakatifu ametoa maswali na kuongeza kusema: Ni jinsi gani ya kuweka pamoja utukufu wa aliye juu na umaskini wa kutisha katika zizi la wanyama? Ka maana ameomba kufikiria hata aibu aliyoipata Mama wa Mungu. Ni kitu gani kilicho kigumu kwa mama ambaye anamwona mtoto wake anateseka katika mahangaiko? Kuna kuhisi kukosa nguvu, amejibu Papa. Isingewezekana kumkaripia Maria ikiwa angelalamika kwa kubaguliwa bila kutegemea. Lakini yeye hakati tamaa. Halalamiki bali anakaa kimya. Anachagua sehemu tofauti kulinganisha na kulalamika kwa maana: “ Maria kwa upande wake alikuwa anayatunza yote na kutafakari katika moyo wake kwa mujibu wa Injili (Lk 2,19).
Hiyo ni namna ya kufanya tofauti na kile ambacho walifanya wachungaji na watu. Wao walisimulia kwa wote kile walicho kiona: Malaika aliwatokea katikati ya usiku, na maneno yake kuhusu mtoto huyo. Na watu baada ya kusikia hayo walishikwa na mshangao( Lk 2,18). Lakini katika maneno ya mshangao Maria kinyume chake anaonekana kufikiria na kutafakari. Anatunza na kutafakari ndani ya moyo wake. Ni tabia mbili tofauti ambazo zinaweza kuonekana ndani mwetu pia. Simulizi na mshangao wa wachungaji unakumbusha mwanzo wa imani. Pale kila kitu ni rahisi na kinaelekeza, ni kufurahia mapya ya Mungu anayeingia katika maisha na kuleta kila mantiki ya hali ya mshangao. Wakati tabia ya kutafakari ya Maria ni kielelezo cha imani komavu na ya mtu mzima. Wa imani ambayo sio changa, bali imekomaa na kuzaa matunda. Kwa sabababu matunda ya kiroho yanapitia njia ya majaribu. Utulivu wa Nazareti na ushindi wa ahadi za Malaika, katika mwanzo wake Maria anaiukuta sasa katika giza la hori huko Bethlehemu. Lakini hapo ndipo Mungu anatoa zawadi kwa ulimwengu. Na wakati wengine mbele ya kashfa za hori, wangeweza kukosa nguvu na kukata tamaa, Yeye hapana, anatunza yote kwa kutafakari.
Baba Mtakatifu ameomba kujifunza kutoka kwa Mama wa Mungu tabia hiyo ya kutunza wakati wa kutafakari. Kwa upande huo hata sisi inatokea kushuhudia baadhi ya kashfa za hori. Wakati mtu anatarajia mambo yaende vizuri, ndipo inafika kama radi kutoka mbingu tulivu, ya matatizo yasiyotarajiwa. Na kuundwa ule uchungu kati ya matarajio na uhalisia. Inatokea hata katika imani, katika wakati furaha ya Injili, inawekwa majaribu ya hali ngumu ambayo tunakumbana nayo katika safari ya maisha. Lakini mama Maria leo hii anatufundisha kujifunza kuondokana na pigo hilo. Anatufundisha kuwa ni lazima kupitia maisha membamba ili kufikia kilele, na msalaba bila majaribu si rahisi kufufuka. Ni kama kuzaliwa kwa uchungu ambao unatoa maisha na imani iliyokomaa zaidi, Papa Francisko amesisitiza. Je ni jinsi gani ya kutimiza hatua hiyo, kushinda hali hiyo kati ya wazo na uhalisia? Kwa kumtazama Maria ambaye alitunza na kutafakari, Maria awali ya yote alitunza na hakuangaika. Hasukumi kile kinachotekea. Anatunza ndani ya moyo wake kila kitu, alichoona na kusikia. Mambo mazuri kama aliyokuwa ameambiwa na Malaika na yale aliyosimuliwa na wachungaji. Lakini pia hata mambo magumu ya kukubali kama ile hatari aliyokumbana nayo kwa sababu ya kupata mimba kabla ya ndoa na sasa, upweke wa kukaa kwenye hori mahali alipojifungua mtoto. Tazama Maria anafanya nini, hachagua, bali anatunza. Anapokea uhalisia unavyomjia, na hajaribu kuukimbia, na kujaribu kuishi maisha ya ujuu huku akihifadhi katika moyo wake.
Papa Francisko vile vile ameeleza kwamba kuna mtazamo wa pili, jinsi ambavyo Mari anatunza? Anatunza kwa kutafakari. Neno lililotumiwa na Injili linaibua kuunganishwa kwa mambo: Maria anaweka uzoefu tofauti, kwa kutafuta mambo yaliyofichwa ambayo yanafungamana. Moyoni mwake, katika maombi yake anatimiza operesheni hii isiyo ya kawaida: anaunganisha mambo mazuri na mabaya; hayatenganishi, bali anayaunganisha. Na kwa sababu hiyo Maria ni mama wa ukatoliki, na ambapo tunaweza kulazimisha lugha kwa kusema kwamba ndiyo maana Maria ni mkatoliki, kwa sababu anaunganisha, hatenganishi. Na hivyo anafahamu maana kamili na mtazamo wa Mungu. Katika moyo wa mama yake anaelewa kwamba utukufu wa Aliye Juu unapitia unyenyekevu; anakaribisha mpango wa wokovu, ambao ilimbidi Mungu atulie kwenye hori. Anamwona Mtoto wa kimungu aliye dhaifu na anayetetemeka, na anakaribisha upatanisho wa ajabu wa kimungu wa ukuu na udogo. Kwa maana hiyo anatunza akitafakari. Mtazamo huu wa kujumuisha, Papa Francisko amesema, unashinda mivutano kwa kutunza na kutafakari moyoni, ni mtazamo wa mama ambao hawatengani katika mivutano, wanatuza mivutano na hivyo maisha yanakua. Ni mtazamo ambao akina mama wengi hukubali hali za watoto wao. Ni mtazamo halisi, ambao haukati tamaa, ambao haupoozi mbele ya matatizo, lakini huwaweka katika upeo mpana zaidi. Na hivyo Maria, hadi Kalvario, alikuwa akitafakari na kutunza. Papa Francisko kutokana na hilo amekumbuka nyuso nyingi za akina mama wanaotunza watoto wagonjwa au wenye shida.
Kuna upendo kiasi gani machoni mwao, ambao huku wakilia wanajua jinsi ya kutoa sababu za kuwa na matumaini! Kwa upande wao ni mtazamo wa utambuzi bila udanganyifu, lakini zaidi ya maumivu na matatizo wanatoa mtazamo mpana zaidi, ule wa kujali, wa upendo ambao unaleta matumaini. Hivyo ndivyo akina mama hufanya: wanajua jinsi ya kushinda vikwazo na migogoro, wanajua jinsi ya kuimarisha amani. Kwa hivyo wanaweza kubadilisha shida kuwa fursa za kuzaliwa upya na fursa za ukuaji. Wanafanya hivyo kwa sababu wanajua kutunza, akina mama wanajua kulinda, wanajua kuweka pamoja maisha ya kila mtu. Kwa maana hiyo Papa amesema kuna haja ya watu ambao wanaweza kusuka kwa pamoja muungano ambao hutofautisha misukano mingi ya migawanyiko. Lakini mama hawa kwa hakika wanajua jinsi ya kufanya. Mwaka mpya unaanza kwa ishara ya Mama Mtakatifu wa Mungu, katika ishara ya Mama. Mtazamo wa mama ni njia ya kuzaliwa upya na kukua. Akina mama, wanawake hutazama ulimwengu sio kuunyonya, lakini ili uwe na uzima: wakiutazama kwa moyo, wanaweza kuweka ndoto na ukweli pamoja, huku wakiepuka kuteleza katika mambo yasiyojenga. Na Kanisa ni mama, ni mama namna hiyo, Kanisa ni mwanamke, ni mwanamke wa namna hiyo, Papa amesisitiza.
Kwa sababu hiyo amesema hatuwezi kupata nafasi ya mwanamke katika Kanisa bila kumuakisi katika moyo huo wa mwanamke yaani mama. Hapo ndipo mahali pa wanawake katika Kanisa, mahali pazuri, ambapo uhalisi zaidi upo na wa pili zaidi hutokea. Lakini Kanisa ni mama, Kanisa na mwanamke. Na wakati mama wakitoa uhai na wanawake wakilinda dunia, sisi sote tufanye kazi ya kuwahamasisha akina mama na kuwalinda wanawake. Je, ni unyanyasaji kiasi gani dhidi ya wanawake uliopo! Inatosha! Papa amesisitiza na kuongeza:“ Kuumiza mwanamke ni kumkasirisha Mungu, ambaye alichukua ubinadamu kutoka kwa mwanamke, sio kutoka kwa malaika, sio moja kwa moja, ni kutoka kwa mwanamke. Kama ilivyo kutoka kwa mwanamke, Kanisa mwanamke linachukua ubinadamu wa watoto. Baba Mtakatifu Francisko amesema katika mwanzoni mwa mwaka mpya, tujiweke chini ya ulinzi wa mwanamke huyo, Mama Mtakatifu wa Mungu ambaye ni mama yetu. Atusaidie kutunza na kutafakari juu ya kila kitu, bila hofu ya majaribu, katika uhakika wa furaha kwamba Bwana ni mwaminifu na anajua jinsi ya kubadilisha misalaba kuwa ufufuko. Leo hii pia tumwombe kama watu wa Mungu walivyofanya kule Efeso, na sote tusimame, tumtazame Mama Yetu, na kama watu wa Mungu walivyofanya huko Efeso, turudie mara tatu wasifu wake Mama wa Mungu, wote kwa pamoja: “Mama Mtakatifu wa Mungu, Mama Mtakatifu wa Mungu, Mama Mtakatifu wa Mungu!”. Amina. Papa amehitimisha.