Rambi rambi za Papa kufuatia na kifo cha Sassoli,Rais wa Bunge la Ulaya
Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumanne tarehe 11 Januari 2022 ametuma salamu za rambi rambi zilizotiwa saini na Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin. Papa anaonesha ukaribu wa kiroho katika wakati huu wa uchungu kufuatia na kifo cha mapema cha Rais wa Bunge la Umoja wa Ulaya, Bwana David Sassoli. Ni salamu zilizoelekezwa kwa Mkewe na watoto wake Livia na Giulio akiwakikishia ukaribu wake na sala zake katika msiba mkubwa ambao umeikumba Italia na Ulaya nzima. Rais wa Bunge la Umoja wa Ulaya Bwana David Sassoli ameaga dunia tarehe 11 Januari akiwa na umri wa miaka 65 na ambaye ameacha mke na watoto wawili. Tangu Septemba iliyopita alipata nimonia iitwayo Legionella. Jumatatu tarehe 10 Januari walitangaza kuhusiana na hali yake na kwamba alikuwa na shida kubwa iliyomfikisha kwenye kituo cha saratani cha Aviano.
Alikuwa mkarimu na mshikamano kwa walio wa mwisho
Papa Francisko anamkumbuka Bwana Sassoli alivyokuwa mwamini na aliyeongozwa na matumaini na upendo, mtaalam wa uandishi wa habari na ambaye alisifiwa na Taasisi ambazo kwa shauku kubwa na heshima katika uwajibikaji wake alifunika kwa ajili ya wema wa pamoja na ukarimu mkubwa. Katika ujumbe huo, aidha amemkumbuka marehemu ambaye alihamasisha katika mwanga na shauku ya maono ya mshikamano wa Jumuiya ya Ulaya kwa kujikita kwa kina kwa namna ya pekee kutetea walio wa mwisho. Papa Francisko anainua sala zake kwa ajili ya roho ya marehemu na kumwomba Bwana Mfufuka apumzike roho yake kwa amani na kuwapatia faraja ya moyo wale wote ambao wanaomboleza kwa kifo chake na hatimaye amewatumia baraka ya kitume mke wake na familia zima.
Mazishi na ujumbe wa CEI
Mazishi ya Bwana David Sassoli yatafanyika Ijumaa tarehe 14 Januari 2022, saa sita mchana katika Kanisa la Mtakatifu Maria wa Malaika, jijini Roma. Siku moja kabla ya maziko jeneza lake litawekwa kwenye chumba cha cha Kitaifa kwa ajili ya kuaga kuanzia saa 4.00 asubuhi hadi saa 12 Jioni. “Katika kujitolea kwake kitaaluma kama mwandishi wa habari na baadaye kama mtu wa taasisi, amekuwa akifanya kazi katika jamii inayounga mkono zaidi na kuzingatia mahitaji ya vijana na walio wa mwisho”. Hiki ni kifungu kutoka katika ujumbe wa salamu za rambirambi wa Baraza la Maaskofu Italia (CEI), uliotiwa saini na Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Italia. “Alikuwa anaamini kwamba waamini na walei wote wanaweza kwa pamoja kujenga upya madaraja ili kuendelea kupambania na kubomoa kuta, kwa kujenga madaraja, na kutoa umuhimu kwa ajili ya ubinadamu mpya, kama alivyosisitiza katika hotuba yake huko Bari, kwenye tukio la mkutano wa “Mpaka wa amani wa Mediteranean' mnamo 2020”, amesisitiza tena Kardinali Bassetti.