Salamu za rambi rambi na ukaribu wa kiroho wa Papa kwa waathirika wa ajali ya moto,Bronx
Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.
Jengo la ghorofa kumi na tisa ambalo kwa ghafla, kutokana na moto, liligeuka kuwa mtego wa kifo kwa wakazi wa ghorofa za kwanza. Ndicho kilichotokea Dominika tarehe 9 Januari 2022 mnamo saa 5.00 asubuhi huko Bronx, jijini New York, wakati moto huo uliposambaa kutoka katika ghorofa ya 120 inayounda jengo hilo, ambako wengi wao ni waamini wa jumuiya ya Kiislamu, huku kukiwa na wahamiaji wengi kutoka nchini Gambia.
Papa anawaombea wote wapate faraja na nguvu katika Bwana
Habari na picha zilienea ulimwenguni kote mara moja. Na katika telegramu iliyotiwa saini na Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, Papa Francisko anaelezea kwa Kardinali Timothy Dolan, askofu mkuu wa New York, masikitiko yake yote kutokana na hatari kubwa iliyoua watu wasiopungua 19, ikiwa ni pamoja na watoto 9. Papa Francisko amewahakikishia ukaribu wake wa kiroho kwa wale ambao wameguswa na janga hilo na anawakabidhi waathirika wote na familia zao kwa upendo wa huruma ya Mwenyezi Mungu huku akiomba faraja na nguvu katika Bwana.
Idadi ya vifo inaweza kuongezeka kati ya 63 majeruhi, 32 wako hatari ya kifo
Wakati huo huo, siku ya kuamkia Jumatatu wameendelea kufanya kazi katika eneo hilo na kujaribu kuelewa njia za kile kilichotokea. Kulingana na mkuu wa kikosi cha zima moto, amesema moto huo ulisababishwa na hitilafu ya hita ya umeme katika chumba cha kulala ambacho moto huo ulitokea na moshi ambao ulienea katika jengo hilo, na umesababisha idadi kubwa ya waathirika. Kwa bahati mbaya, idadi hiyo inaweza kuongezeka, kwani kati ya watu 63 waliojeruhiwa, 32 walitangazwa kuwa katika hatari ya maisha. Wazima moto 200 waliingilia kati papo kwa hapo na kujaribu kwa kila njia kuwaokoa wakazi wa jengo hilo, ambao wengi wao walishindwa kukimbia kwa sababu ya wingu kuu la moshi.