Askofu mstaafu Remi Joseph De Roo wa Jimbo la Victoria British, Columbia amefariki dunia tarehe 1 Februari 2022 Askofu mstaafu Remi Joseph De Roo wa Jimbo la Victoria British, Columbia amefariki dunia tarehe 1 Februari 2022 

Askofu Mstaafu Remi Joseph De Roo: Mtaguso Mkuu II wa Vatican

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Ibada hii, anaungana na watu wote wa Mungu kuomboleza kifo cha Askofu mstaafu Remi Joseph De Roo. Anamshukuru Mungu kwa kulijalia Kanisa viongozi waliosimama kidete katika maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kudumisha ujirani mwema, umoja, ushiriki na mshikamano wa udugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mstaafu Remi Joseph De Roo wa Jimbo la Victoria British, Columbia, Canada alizaliwa tarehe 24 Februari 1924 kwenye Jimbo kuu la “Sancti Bonifacii”, nchini Canada. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 8 Juni 1950 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre na kuingizwa kwenye Jimbo Katoliki la St. Boniface, Manitoba, Canada. Akiwa na umri wa miaka 38 ya kuzaliwa, Mtakatifu Yohane XXIII akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Victoria British Columbia na kuwekwa wakfu tarehe 14 Desemba 1962. Na ilipogota tarehe 18 Machi 1999 akang’atuka kutoka madarakani baada ya ombi lake kuridhiwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Tarehe 1 Februari 2022 akafariki dunia, huku akiwa amemtumikia Mwenyezi Mungu na Kanisa lake kama Padre kwa kipindi cha miaka 71 na kama Askofu mwenye dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa muda wa miaka 59. Takwimu zinaonesha kwamba, ni kati Maaskofu waliopewa Daraja ya Uaskofu wakiwa na umri mdogo sana ulimwenguni na hivyo kubahatika kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika vikao vyake vyote vinne.

Huyu ni kati ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican waliokuwa bado wako hai, huku wakiendelea kuliombea Kanisa la Kristo ambalo kwa sasa linajielekeza katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kwa kujikita katika: Umoja, Ushiriki na Utume.” Ni katika muktadha huu, tarehe 12 Februari 2022 huko Victoria, kwenye Kisiwa cha Vancouver, nchini Canada, Kardinali Michael F. Czerny, S.J. Mwenyekiti wa muda wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na fungamani ya Binadamu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Askofu mstaafu Remi Joseph De Roo wa Jimbo la Victoria British, Columbia, Canada. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Ibada hii, anaungana na watu wote wa Mungu kuomboleza kifo cha Askofu mstaafu Remi Joseph De Roo. Anamshukuru Mungu kwa kulijalia Kanisa viongozi waliosimama kidete katika maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kujenga na kudumisha ujirani mwema, umoja, ushiriki na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Ametoa baraka zake za kitume kwa wale wote walioshiriki katika msiba na Ibada hii ya Misa Takatifu. Ni kiongozi wa Kanisa aliyejikita katika majadiliano yanayosimikwa katika misingi ya ukweli na uwazi; akarutubisha maisha ya watu wa Mungu kwa “cheche za Injili ya Kristo Yesu.”

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unasonga mbele
Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unasonga mbele

Kwa upande wake Kardinali Michael F. Czerny, S.J. katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa ujenzi wa ushirika na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na watu mahalia. Amesema, ni kiongozi wa Kanisa aliyejipambanua katika ujenzi wa haki jamii, changamoto nzito aliyoibeba katika maisha na utume wake, kiasi hata cha Baraza la Maaskofu Katoliki la Canada, kumteuwa kwa miaka mingi kuwa ni Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Canada. Alipenda kukazia umuhimu wa kujikita katika haki na wajibu; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete. Alitambua na kuwaheshimu wabatizwa wote, kwani wakiwa wana wa Mungu kwa kuzaliwa upya, wabatizwa wana wajibu kukiri mbele za watu imani ambayo wameipokea kwa Mungu kwa njia ya Kanisa na hivyo kushiriki utendaji wa kitume na wa kimisionari wa Taifa la Mungu. Rej. KKK 1269-1270. Alisimamia, utu, heshima na haki msingi za wanawake na akasimama kidete kupinga mifumo mbalimbali ya ubaguzi uliokithiri katika jamii wakati ule kwa kusema kwamba, Kanisa ni Mama wa wote.

Msimamo, sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji ilimjengea maadui wengi hata ndani ya Kanisa, lakini baadhi ya watu wa Mungu walimuunga mkono, kiasi kwamba, mwandishi mmoja akaandika kitabu kuhusu msimamo wake wa shughuli za kichungaji kijulikanacho kama “Political Sea-change in the Catholic Church.” Kardinali Michael F. Czerny, S.J. amewataka waombolezaji kuchunguza maisha na dhamiri zao, ili kuangalia ikiwa kama misimamo yao inakwenda kadiri ya Mafundisho makuu ya Kristo Yesu, au wanatawaliwa na vionjo vyao binafsi. Ikumbukwe kwamba, Siku ile ya Mwisho, watu watahukumiwa kadiri ya jinsi walivyowatendea jirani zao, na kipimo kikuu ni matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Katika mchakato wa uinjilishaji mpya, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walikazia pamoja na mambo mengine ushuhuda unaofumbatwa katika Urika wa Maaskofu. Imani, Uaminifu na Upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, daima, waamini wakijitahidi kusoma alama za nyakati, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu atakayekuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho.

Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume
Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume

Mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, hauna budi kumwilishwa na kupata mwitikio wake katika: Katekesi, Kiturujia ya Kanisa, Familia, Ajira, Haki, Amani sanjari na Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, daima waamini wajitahidi kudumisha umoja, ushiriki na utume wa Kanisa. Ni katika hali na mazingira ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana pamoja na kuthamini karama mbalimbali za wanajumuiya kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Kristo. Ni wakati muafaka wa ujenzi wa Kanisa la Kimisionari tayari kutoka ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika ushuhuda wa maisha adili na matakatifu. Kardinali Michael F. Czerny, S.J. anakaza kusema, huu ni muda muafaka wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu, ili kupandikiza mbegu ya imani, matumaini na mapendo kwa watu wote wa Mungu, lakini vijana wakipewa kipaumbele cha kwanza. Waamini wakuze utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, tayari kupokea mawazo ya watu wengine, ili kujenga Jumuiya ya Wasamaria wema, ambao wako tayari kuwaganga na kuwahudumia wale wote waliovunjika na kupondeka moyo kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini.

Hayati Askofu Remi
13 February 2022, 15:16