Washiriki wa Mkutano wa 95 wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki Washiriki wa Mkutano wa 95 wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki  

Baba Mtakatifu Francisko Asema Tena Vita Ni Mauaji Yasiyo na Maana

Papa amegusiakuhusu: Mauaji yasiyo na maana “Inutile strage, frustra caedem”, ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kama chemchemi ya uinjilishaji. Neno la Mungu ligange na kuponya udhaifu na madonda ya binadamu pamoja na Kongamano la maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Mwongozo wa Sheria za Kanisa Kuhusu Liturujia utolewe kunako mwaka 1996.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki kuanzia tarehe 16-18 Februari 2022 limekuwa likiendesha mkutano wake 95 wa mwaka kwa faragha, sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Mwongozo wa Sheria za Kanisa Kuhusu Liturujia utolewe na Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 6 Januari 1996. Ijumaa tarehe 18 Februari 2022 Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na hatimaye, wajumbe kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Katika hotuba yake, amegusia kuhusu mauaji yasiyo na maana “Inutile strage, frustra caedem” kama yalivyofafanuliwa na Papa Benedikto XV kama yanavyoendelea kushuhudiwa hata katika nyakati hizi, ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kama chemchemi ya uinjilishaji. Neno la Mungu ligange na kuponya udhaifu na madonda ya binadamu pamoja na Kongamano la maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Mwongozo wa Sheria za Kanisa Kuhusu Liturujia utolewe kunako mwaka 1996.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amewapongeza wajumbe wa Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki kwa kushiriki Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na hivyo kupata nafasi ya kuungama imani ya Kanisa, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro alipokiri kwamba, “Wewe ndiwe Kristo Mwana wa Mungu aliye hai” Mt 16:16. Kielelezo cha umoja na utofauti wa Kanisa pasi na ubaguzi wa lugha wala utaifa. Ni Papa Benedikto XV, miaka mia moja iliyopita tangu alipofariki dunia alipotangaza kwamba, “Vita ni mauaji yasiyo na maana” “Inutile strage, frustra caedem.” Lakini, angalisho lake, likagonga mwamba na wala wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa hawakumsikiliza kama ilivyokuwa hata kwa mwaliko uliotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa Vita ya Ghuba ya Uajemi, huko Iraq. Huo ni wito ambao umekuwa ukirudiwa mara nyingi na viongozi wa Kanisa huko Mashariki ya Kati, Siria na Iraq, Ethiopia na Tigray na kwa wakati huu, ambapo kuna hofu kubwa ya uvamizi na mashambulizi ya kivita huko nchini Ukraine.

Kuna watu wanateseka sana kutoka na vita inayoendelea duniani.
Kuna watu wanateseka sana kutoka na vita inayoendelea duniani.

Bado watu wanateseka sana huko nchini Lebanon kwa kukosa mahitaji msingi. Matumaini ya watu wa Mungu yametoweka na kuyeyuka kama “umande wa asubuhi” na matokeo yake, watu wamejaa hofu na wasi wasi, lakini huko ndiko ambacho kuna utajiri na amana kubwa la tamaduni za watu na kwamba, wajumbe wa Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki ni mashuhuda na warithi wa tunu hizi. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza Wakristo wa Makanisa ya Mashariki kwa ushuhuda wa imani wanaoendelea kuutolea maisha kwa kupandikiza mbegu ya imani sehemu mbalimbali za dunia. Kumbe, jambo la msingi ni kuendelea kujikita katika mchakato wa katekesi makini na endelevu. Ushiriki wa wakleri, watawa na waamini walei ni muhimu sana, ili kutoa mwanya kwa watawa wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kuweza kuchangia karama na utume wa Mashirika yao, mambo ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee wakati wa maadhimisho ya Mkutano wa 96 wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki.

Vita ina madhara makubwa katika maisha ya watu.
Vita ina madhara makubwa katika maisha ya watu.

Baba Mtakatifu Francisko amesema, udhaifu na mapungufu ya kibinadamu yanagangwa na kuponywa kwa Neno la Mungu na Roho wa Kristo Yesu Mfufuka anayejidhihirisha na kujifunua katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Liturujia ni mahali pa kuwakutanisha watu wa Mungu, tayari kujikita katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Liturujia inawasaidia waamini kukutana na Kristo Yesu aliyekuja hapa ulimwenguni. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Mwongozo wa Sheria za Kanisa Kuhusu Liturujia utolewe na Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 6 Januari 1996 iwe ni fursa ya Tume mbalimbali za Liturujia ya Makanisa ya Mashariki kufahamiana na Mabaraza ya Kipapa pamoja na washauri wake, mintarafu Mwongozo ulitolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Pili, kwa kuendelea kutunza na kudumisha utajiri wa umoja na utofauti, kwa kuwa na mwelekeo wa majadiliano ya kiekumene kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa zima la Kristo Yesu katika Liturujia, hata kama bado, hakuna umoja kamili unaoonekana miongoni mwa wafuasi wa Kristo Yesu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Ulimwengu una kiu ya ushuhuda wa ushirika, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, chimbuko la umoja wa Kanisa.

Makanisa ya Mashariki
18 February 2022, 15:59