Wasanii Tangazeni na Kushuhudia Kiu ya Uzuri na Utakatifu wa Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, Sanaa takatifu zinaheshimika kwa namna ya pekee, kwa sababu zinahusiana na uzuri wa Mungu usioweza kupimika, kwa kumpatia Mungu sifa na kumtukuza. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, amejitahidi sana kuwalea wasanii, ili mambo ya Ibada takatifu yapewe kweli heshima na uzuri, kwani hayo ni alama na ishara za yale mambo ya mbinguni. Rej. Sacrosanctum concilium, 122-130. Ilikuwa ni mwaka 2011 Daniel na Anne Facérias chini ya usimamizi wa Askofu Dominique Rey wa Jimbo Katoliki Frejus-Toulon, nchini Ufaransa walipozindua Chama cha Kitume cha “Diacone de la Beauté” “Diaconia della Bellezza” yaani “Huduma ya Uzuri”, kilicho wakusanya wasanii kutoka nchini Ufaransa, ili kupyaisha tena utambulisho, utume na ujumbe wao kwa watu wa Mungu, mintarafu mchango wa Kanisa katika ulimwengu wa sanaa. Ni wasanii walioweza kuufikisha ujumbe wa Fumbo la Umwilisho kwa njia ya sanaa na muziki wao, kiasi cha kusaidia mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho wa Injili. Wanachama wa Chama cha “Diacone de la Beauté” yaani “Huduma ya Uzuri” wanapania kutangaza na kushuhudia ukuu, uzuri na utakatifu wa Mwenyezi Mungu kwa njia ya: Sala, Ushuhuda, Mshikamano sanjari na kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa maneno na matendo yao ya kisanii.
Katika muktadha wa kumbukizi la miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Huduma ya Uzuri, Alhamisi, tarehe 17 Februari 2022, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na baadhi ya wajumbe wa Chama hiki mjini Vatican. Amewapongeza kwa kuwasaidia watu wa Mungu kujikita katika njia ya uzuri: “Via pulchritudinis” ili kuyajaza maisha kwa mwangaza mpya wa furaha kuu. Uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji unafanya rejea kwa Mungu Muumbaji wa vyote. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni wasanii na wajenzi wa uzuri wa kazi ya uumbaji inayopata chimbuko lake kutoka katika imani, ili hatimaye, waweze kumpenda na kumtukuza Mwenyezi Mungu asili ya uzuri na utakatifu wote. Baba Mtakatifu amewapongeza kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika kipindi cha miaka kumi tangu kuanzishwa kwake. Kwa hakika wameonesha na kushuhudia upendo na ari ambayo imewasaidia kwa hakika kutumia karama na mapaji yao kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama njia ya kutangaza na kushuhudia imani, sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji mpya. Sanaa hii inatoa mwaliko na mvuto wa kumwendea Mwenyezi Mungu, kwa watu wa nyakati zote na kwamba, kazi zao za kisanii kamwe haziwezi kupitwa na wakati, kwani ni msaada mkubwa kwa waamini wanaotaka kuzima kiu yao kwa Mwenyezi Mungu.
Uzuri wa kweli unaweza kuwa njia inayowaelekeza watu kukutana na Kristo Yesu ambaye ni ufunuo wa uzuri usio na mipaka, anayewavuta watu kwake kwa njia ya upendo. Ni vyema kukuza na kudumisha: ukweli, wema na uzuri unaomwezesha Kristo Yesu Mfufuka kuangaza ndani yake. Rej. Evangelii gaudium, 167. Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema, ili Mama Kanisa aweze kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia anahitaji sanaa, ili kuweza kumfikia Mwenyezi Mungu, ili kwa wale wanaoona na kusikiliza waweze kuguswa na uwepo wa Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza wasanii kujibidiisha kuzungumza na watu wa Mungu katika lugha inayofahamika kwa urahisi katika maisha yao, kwa kugusa mambo mazuri zaidi. Kanisa linawategemea wasanii ili waweze kuwasaidia watoto wa Kanisa kuwa na huruma na upendo kwa jirani zao na ulimwengu katika ujumla wake. Kwa bahati mbaya sana, leo hii walimwengu wamekumbwa na huzuni na hofu nyoyoni mwao, lakini ikumbukukwe kwamba, sanaa daima ni chemchemi ya furaha inayowawezesha waamini kuonja wema, huruma na upendo wa Mungu. Uzuri unawainua juu watu wa Mungu na kuwasukuma kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Mwishoni, mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewashukuru wasanii kwa mchango na huduma yao ya upendo na weledi kwa watu wa Mungu. Bikira Maria Mama wa Mungu awasaidie na kuwaingiza katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kamwe wasisahau kumwomba Roho Mtakatifu katika maisha na utume wao.