Tafuta

Jumatano ya Majivu iwe ni siku ya kufunga na kusali ili kumlilia Mungu akomeshe vita sehemu mbalimbali za dunia. Jumatano ya Majivu iwe ni siku ya kufunga na kusali ili kumlilia Mungu akomeshe vita sehemu mbalimbali za dunia. 

Jumatano ya Majivu: Siku ya Kufunga na Kusali Dhidi ya Vita Duniani

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine, kama kielelezo cha udugu na ujirani mwema na watu wote wa Mungu nchini Ukraine. Ni siku ya kumlilia Mwenyezi Mungu, ili aweze kukomesha vita. Wale wote wanaoanzisha vita, kinzani na vurugu ni kwa ajili ya masilahi binafsi; ni kielelezo cha uchu wa mali na madaraka wamesahu utu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anakianza rasmi Kipindi cha Kwaresima tarehe 2 Machi 2022 kwa Ibada ya Jumatano ya Majivu, kielelezo cha toba na wongofu wa ndani. Hiki ni kipindi cha sala na kufunga; kusoma na kulitafakari Neno la Mungu linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.” Gal 6:9-10. Baba Mtakatifu Francisko akiwa na machungu pamoja na masikitiko makubwa sana moyoni mwake kutokana na Urussi kuivamia kijeshi Ukraine, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine ambayo kwa sasa inateseka sana baada ya kuvamiwa kijeshi na Urussi, tarehe 24 Februari 2022.

Jumatano ya Majivu Siku ya Kufunga na Kusali dhidi ya vita duniani.
Jumatano ya Majivu Siku ya Kufunga na Kusali dhidi ya vita duniani.

Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika, tarehe 27 Februari 2022 amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusali bila kuchoka kwa ajili ya kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine, kama kielelezo cha udugu na ujirani mwema na watu wote wa Mungu nchini Ukraine. Ni siku ya kumlilia Mwenyezi Mungu, ili aweze kukomesha vita. Wale wote wanaoanzisha na kuchochea vita wanasahau utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wanaoanzisha vita, kinzani na vurugu ni kwa ajili ya masilahi binafsi; ni kielelezo cha uchu wa mali na madaraka.

Ni watu wanaojiamini kwa kuwa na nguvu ya silaha, kiasi cha kuwafanya waende mbali sana na utashi wa Mungu katika maisha yao. Hawa ni watu wanaowageuzia kisgo maskini na wale wote wanaoteseka kutokana na madhara ya vita. Kimsingi watu wa kawaida kabisa wanahitaji haki na amani. Katika mapambano ya silaha wanaoumia sana ni wanawake, wazee na watoto, hao ndio wanaolipata gharama za kivita. Ni watu wanaolazimika kuyakimbia makazi na nchi zao ili kusamilisha maisha. Leo hii anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna msafara mkubwa wa watu wanaokimbia nchi na miji yao huku wakitafuta usalama wa maisha yao. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwafungulia malango na kuwakarimu. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, anaendelea bado kuteseka kutokana na vita na migogoro ya kijamii inayoendelea nchini Ukraine, Yemen, Siria na Ethiopia na Nigeria. Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wakuu wa nchi kusimamisha mashambulizi ya kijeshi na kuanza kujielekeza katika ujenzi wa msingi ya haki; amani na maridhiano. Watu wajenge utamaduni wa kupenda amani na kuchukia vita ambavyo ni uvunjifu wa uhuru wa watu wengine na hatimaye, kutumbukia katika kashfa za Kimataifa.

Kufunga na Kusali
28 February 2022, 16:28