Tafuta

Kardinali Luigi de Magistris amefariki dunia tarehe 16 Februari 2022 Kardinali Luigi de Magistris amefariki dunia tarehe 16 Februari 2022 

Hayati Kardinali Luigi De Magristris Chombo Cha Huruma ya Mungu

Kardinali Luigi De Magistris alizaliwa mwaka 1926 huko Cagliari. Tarehe 12 Aprili 1952 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Alianza kutoa huduma yake ya kichungaji mjini Vatican kuanzia mwezi Februari, 1969. Tarehe 11 Aprili 1979 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Hakimu ya Idara ya Toba ya Kitume. Tarehe 6 Machi 1996 akateuliwa kuwa Askofu na kuwekwa wakfu Apr. 1996.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Luigi De Magistris, Mhudumu mkuu mstaafu wa Toba ya Kitume, amefariki dunia tarehe 16 Februari 2022 huko Cagliari, Kusini mwa Italia, akiwa na umri wa miaka 96. Hayati Kardinali Luigi De Magistris alizaliwa tarehe 23 Februari 1926 huko Cagliari. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 12 Aprili 1952 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Alianza kutoa huduma yake ya kichungaji mjini Vatican kuanzia mwezi Februari, 1969. Tarehe 11 Aprili 1979 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Hakimu ya Idara ya Toba ya Kitume. Tarehe 6 Machi 1996 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu na kuwekwa wakfu tarehe 28 Aprili 1996.

Kardinali Luigi De Magistris
Kardinali Luigi De Magistris

Tarehe 22 Novemba 2001 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu mkuu na Mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume na tarehe 4 Oktoba 2003 akang’atuka kutoka madarakani. Tarehe 14 Februari 2015 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Kardinali. Kwa muda wote huo aliendelea kutoa huduma za maisha ya kiroho hasa kwa Sakramenti ya Upatanisho.Tarehe 16 Februari 2022 akafariki dunia na kuzikwa tarehe 17 Februari 2022. Baba Mtakatifu Francisko amepokea taarifa ya msiba wa Kardinali Luigi De Magistris, Mhudumu mkuu mstaafu wa Toba ya Kitume kwa masikitiko na majonzi makubwa. Ametumia fursa hii, kutuma salam zake za rambirambi kwa watu wa Mungu wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito.

Baba Mtakatifu Francisko anamkumbuka Hayati Kardinali Luigi De Magistris kutokana na ari na moyo wake wa sadaka ya kikuhani, iliyomfanya kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Anamshukuru kwa moyo wake wa ukarimu na majitoleo kwa ajili ya huduma kwa Kanisa la Ulimwengu. Kwa hakika alikuwa ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, daima alitanguliza mafao ya roho za waamini. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kwa ajili ya kuiombea roho ya Hayati Kardinali Luigi De Magistris, kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Imani iweze kupokelewa huko Yerusalemu ya mbinguni, ili hatimaye, apate kufurahi na watakatifu wa Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko alitoa baraka zake za kitume kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema walioshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maziko ya Kardinali Luigi De Magistris.

Kardinali Luigi
22 February 2022, 14:57