Nia za Papa Francisko Kwa Mwezi Februari 2022: Shukrani Kwa Watawa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za jumla kwa Mwezi Februari 2022 anapenda kuchukua fursa hii, kuwashukuru watawa na wanawake wote waliojiweka wakfu, kwa uwepo wao, kile wanachotenda na jinsi wanavyotenda. Baba Mtakatifu katika nia hizi zinazosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anawashukuru watawa kutokana na mchango wao mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Anawaalika kuendelea kujisadaka zaidi, ili kuleta mabadiliko katika maisha ya maskini, wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na wale wote wanaotumbukizwa katika mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Baba Mtakatifu anakiri na kutambua kwamba, kuna wakati watawa wanatendewa kinyume cha haki, hata ndani ya Kanisa lenyewe. Lakini yote haya kamwe yasiwakatishe tamaa, bali wasonge mbele kwa ari na moyo mkuu katika utekelezaji wa utume wao. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wawaombee watawa ili waweze kupata majibu muafaka kwa changamoto zinazo waandama watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo. Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa, “International Union of Superior General, UISG” linayaunganisha Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume yapatayo 1, 900 yaliyo enea sehemu mbalimbali za dunia.
Baba Mtakatifu anakiri kwamba, watawa na wanawake waliojiweka wakfu wanayo dhamana na mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa, bila watawa, Kanisa haliwezi kutambulika vyema. Takwimu zilizochapishwa na Shirika la Habari za Kimisionari, Fides kwa mwaka 2021 zinaonesha kwamba, kuna watawa zaidi ya 630, 000 walioenea sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu anaendelea kuwachangamotisha watawa na wanawake waliojiweka wakfu kujisadaka zaidi kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbalimbali. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya video unaonesha jinsi ambavyo watawa wanawahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Jinsi wanavyojisadaka kuwahudumia wagonjwa na wenye njaa vijijini; bila kuwasahau wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na fursa za ajira mijini. Ni watawa wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa: watoto, wanawanake na wasichana wanaotumbukizwa katika mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo.
Ikumbukwe kwamba, licha ya matendo hayo ya huruma, lakini watawa pia wamechangia kwa kiasi kikubwa katika taaluma, ujuzi na mang’amuzi yao kwa kufundisha kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu; kwa kushiriki katika mikutano ya kitaifa na kimataifa kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote bila kusahau mchango wao katika kutafuta suluhu ya haki, amani na maridhiano katika migogoro ya kitaifa na Kimataifa. Baba Mtakatifu anawataka watawa na wanawake waliojiweka wakfu kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mungu kama: Makatekista, Wanataalimungu na Walezi wa maisha ya kiroho katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa.
Kwa upande wake, Sr. Jolanda Kafka, Rais wa Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa, “International Union of Superior General, UISG” anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatia shime ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika maisha na utume wao, licha ya changamoto nyingi zinazowaandama watawa katika ulimwengu mamboleo. Waendelee kuwasindikiza kwa sala na sadaka zao za kila siku, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni vyombo vya furaha ya Injili na Matumaini kwa kushuhudia uzuri, wema na utakatifu wa maisha ya kitawa, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu, huku wakifuata mfano wa Kristo Yesu.
Wakati huo huo, Padre Frédéric Fornos, Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anasema, watawa na wanawake waliojiweka wakfu wanachangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa sehemu mbalimbali za dunia. Ni wanawake ambao wako mstari wa mbele katika shughuli za kichungaji, katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii, tayari kujibu kilio cha mahangaiko ya watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo. Kuna wanawake waliojiweka wakfu ambao wanaendelea kuchangia sana katika malezi na makuzi ya vijana, kwa ajili ya huduma ya Injili, haki na ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Mwezi Februari, ni wakati muafaka kwa watu wa Mungu, kuonesha ukaribu wao kwa njia ya sala kwa watawa na wanawake waliojiweka wakfu. Waamini wajitahidi kutambua umoja na utofauti wa karama na maisha yao, ili kwa pamoja, watu wote wa Mungu waweze kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa uwepo na mchango wa watawa na wanawake waliojiweka wakfu.