Papa aonesha ukaribu kwa Madagascar na Brazil kutokana na dhoruba&mafuriko
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kwa mara nyingine tena Papa Francisko ameonesha ukaribu wake kwa watu waliokumbwa na majanga ya asili kwa siku za hivi karibuni. Ameonesha hayo mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana kwa waamini na mahujaji waliunganika katika uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 20 Februari 2022. Papa Francisko amefikiria kwa namna ya pekee watu wa Kusini Mashariki mwa kisiwa cha Madagascar, waliokumbwa na safu za dhoruba kali na sehemu za Petropolis nchini Brazil ambao wamekumbwa na mafuriko na maporomoko. Katika sala yake Papa amemwomba Bwana, aweze kuwapokea marehemu wote katika amani yake na kuwafariji familia zote huku akiwasaidia wale ambao wanatoa huduma ya kuwaokoa.
Katika majeraha yaliyosababishwa na dhoruba kwenye kisiwa cha Kiafrika kwa mfululizo wa dhoruba tatu Ana, Batsirai na baadaye Dumako, ambazo kwa wiki chache zilipelekea vifo na uharibifu mkubwa wa kisiwa, Papa Francisko alikuwa tayari amewakumbuka kwa uchungu mkubwa Jumamosi tarehe 19 Februari 2022. Ni katika Telegramu iliyotiwa saini na Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, aliyoielekeza kwa Rais wa Jamhuri ya Madagascar Andry Rajoelina, ambapo aliomba wafikiwe watu wote ukaribu wake kutokana na majanga ya kiasili ambayo yamesababisha hadi sasa vifo takribani watu 120 na kuwakumba kwa namna moja mamia elfu ya watu, ambao sasa wamebaki bila kuwa na nyumba, na wamerundikana na wakati huo wakitaabika kwa njaa. Kwa mujibu wa Shirika la Mpango na Chakula Duniani hatari zaidi inawezekana kufikia watu milioni moja na laki sita ambao katika kisiwa hicho maji yameharibu majaruba ya mpunga, kwa kuharibu mavuno yao, kitu msingi ambacho wanategemea kuishi.
Papa Francisko wakati huo huo tayari alikuwa ametazama hali mbaya ambayo inatawala eneo Petropolis la Brazil katika siku za hivi karibuni, kwa kutuma telegramu kwa Askofu Gregório Paixão Neto, wa jiji la Brazili, iliyotiwa saini na katibu wa Vatican Kardinali Pietro Parolin. Na katika siku hizi mbili, idadi ya watu, kwa bahati mbaya siya uhakika, ya mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyolikumba eneo la Petropolis la Brazil, Kusini Mashariki mwa nchi hiyo ya Amerika Kusini, na imeongezeka hadi watu 146 waliopoteza maisha. Kati ya hao, 26 ni watoto. Hata Jumamosi 19 Februari waokoaji waliendelea kuchimba matope kutwa nzima wakitarajia kuwapata waliopotea wakiwa hai.
Mvua kubwa iliyonyesha katika jiji hilo na vitongoji vyake katika siku za hivi karibuni, ambalo lina wakazi 300,000 na linapatikana takriban kilomita sitini kaskazini mwa Rio de Janeiro, zimesababisha maporomoko ya ardhi, kuporomoka na tope nyingi barabarani. Mamia ya wazima moto bado wako kazini, kwa msaada wa mbwa, helikopta na wachimbaji. Takriban nyumba themanini zilisombwa na matope katika kitongoji kimoja, Alto Serra, na hapo ndipo maiti za mwisho zilipatikana. Hata hivyo idadi ya watu waliopotea haijulikani na polisi walizungumza juu ya 218, lakini bila kutaja ikiwa idadi hiyo inajumuisha vifo vilivyothibitishwa.