Papa awashukuru wahudumu wa Afya,mashujaa wa Uviko
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Papa Francisko mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana Dominika tarehe 20 Februari 2022 kwa mahujaji na waamini waliofika katika kiwanja cha Mtakatifu Petro amesema:“Katika magonjwa tunahitaji mtu wa kutuokoa, atusaidie: tuwapigie makofi na shukrani kubwa kwa wahudumu wa afya shujaa ambao walionesha ushujaa huu wakati wa Uviko lakini ushujaa unabaki kila siku. Amesema hayo katika siku ya Kitaifa nchini Italia ya Wahudumu wa kiafya, ambao wanasaidia wagonjwa, wanawatibu na kuwafanya wahisi vizuri. Papa amesema kuwa "hakuna anayejiokoa mwenyewe. Na katika magonjwa sisi tunahitaji mtu ambaye aweze kutuokoa. Daktari mmoja aliniambia asubuhi ya leo kwamba mtu alikuwa akifa wakati wa Covid na akamwambia: “Nishike mkono ninakufa na ninahitaji mkono wako”.
Katika uwanja wa Mtakatifu Petro, wakati wa salamu za mwisho, Papa Francisko amewatia moyo kikundi cha “Progetto Arca”, yaani “Mpango wa safina” waliokuwapo kwenye uwanja huo, ambacho katika siku za hivi karibuni kilizindua shughuli zake za kijamii jijini Roma, kwa ajili ya kutoa msaada wa watu wasio na makazi.
Katika siku ya II ya Kitaifa kwa ajili ya Wahudumu wa Kiafya, iliyoanzishwa na Serikali ya Italia wakati wa kufanya kumbu kumbu ya mwaka wa kwanza tangu kuzuka kwa janga la UVIKO, hasa baada ya kugundua mgonjwa wa kwanza huko Codogno,katika wilaya ya Lodi, hata Rais wa Jamhuri ya Italia Bwana Sergio Mattarella ameshukuru maandalizi ya kitaaluma na roho ya kujitoa sadaka kwa wafanyakazi wa kiafya. Ni kutokana na sifa hizi, ambapo anakumbusha katika ujumbe, kwamba iliwezekana kuzuia hatari ya hasara kubwa zaidi kuliko zile ambazo ziliwahi kuleta uchungu sana na ambazo kwa walio wengi waliteseka.
Na kwa upande wa Askofu Mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha, katika fursa ya Siku ya II ya Kitaifa amethibitisha kuwa kusindikiza mtu mdhaifu ni njia ya kufuata kwa ajili ya wakati ujao wa ubinadamu mpya, kwa sababu somo kuu la kwanza la janga hili lilikuwa ni kugundua kuwa sisi sote ni watu dhaifu, watu na taasisi, pamoja na sayansi. Kwa hivyo, muungano na walio dhaifu zaidi, na wagonjwa ni muhimu kwa sababu ndio njia pekee ya ubinadamu mpya, ambayo kwanza kabisa sio kumwacha mtu yeyote nyuma, hasa dhaifu.