Tafuta

 Papa akiwa katika mahojiano na Fazio, katika kipindi cha Che tempo fa Papa akiwa katika mahojiano na Fazio, katika kipindi cha Che tempo fa 

Papa Francisko:Kanisa linanisaidia kubeba mzingo wa mateso na uchungu!

Papa Francisko kwa kuunganishwa akiwa katika Nyumba ya Mtakatifu Marta kwenye kipindi cha “Che tempo che fa” amezungumza kwa mapana na marefu na mwendesha kipindi hicho Fabio Fazio ambaye amemuuliza jinsi gani anaweza kubeba uzito wa historia nyingi za mateso na uchungu usiolezeka.Papa amejibu "Kanisa zima linansaidia".

Na Angella Rwezaula – Vatican

Papa Francisko katika usiku wa Dominika tarehe 6 Februari 2022 ameunganishwa kutoka nyumba ya Mtakatifu Marta, Vatican katika kipindi cha  “Che tempo fa”, kinachoendeshwa na Fabio Fazio cha Rai3, ambapo amemwoji kuhusu mada nyingi sana kama vile vita, wahamiaji, ulinzi wa kazi ya  uumbaji, uhusiano kati ya wazazi na watoto, uovu na mateso, sala, mustakabali wa Kanisa, hitaji la kuwa na marafiki na msamaha. Papa amesema kwamba: "msamaha ni haki ya kibinadamu. Uwezo wa kusamehewa ni haki ya binadamu. Sote tuna haki ya kusamehewa ikiwa tutaomba msamaha".

Utamaduni wa kutojali na watoto wanaokufa

Kwa mwendesha kipindi amesema "mtazamo wetu unalenga kwanza kabisa mada inayopendwa na Papa ya uhamiaji. Kwa bahati mbaya, ni mada inayoibuka baada ya habari za hivi karibuni  za wahamiaji 12 waliopatikana wamekufa kwa sababu ya baridi kwenye mpaka kati ya Ugiriki na Uturuki. Kwa upande wa Papa Francisko amesema hii ni ishara kidogo ya utamaduni wa kutojali. Na pia ni tatizo la kuainisha kuwa vita, kwanza; watu, baadaye. Yemen ni mfano wa hilo. Yemen imekuwa na vita kwa muda gani na tumekuwa tukizungumza juu ya watoto wa Yemen kwa muda gani, ameuliza Papa. Kuna mambo ambayo ni muhimu na mengine yako chini kabisa: watoto, wahamiaji, maskini, wale ambao hawana chakula. Hao hawahesabiki , angalau kuwa wa kwanza, kwa sababu kuna hata watu wanaopenda watu hawa, ambao wanajaribu kuwasaidia, lakini katika mawazo ya ulimwengu ni nini muhimu? ni vita, uuzaji wa silaha. Fikiria kuwa, kwa mwaka bila kutengeneza silaha, unaweza kutoa chakula na elimu kwa ulimwengu wote, bure. Lakini hiyo haitazamwi, amesema Papa Francisko. Wazo lake amelielekeza pia kwa Alan Kurdi, mtoto Msiria aliyepatikana amekufa kwenye ufuko wa bahari na kwa ajili ya watoto wengine wengi kama yeye ambao hatuwajui na wanaokufa kwa baridi kila siku. Hata katika hali hii, vita bado ni kundi la kwanza, Papa ameongeza kusema “Tazama tuone jinsi uchumi unavyohamasishwa na kile ambacho ni muhimu zaidi leo, vita: vita vya kiitikadi, vita vya nguvu, vita vya biashara na viwanda vingi vya silaha”.

Papa akiwa katika mahojiano na mwendesha Kipindi cha Che Tempo Fa cha Rai3
Papa akiwa katika mahojiano na mwendesha Kipindi cha Che Tempo Fa cha Rai3

Kufanya vita ni fundi wa uharibifu

Na akizungumzia kuhusu vita, Papa Francisko  alipoulizwa kuhusu mvutano kati ya Ukraine na Urusi, amekumbuka mizizi ya ukweli huu wa kutisha, unaofafanuliwa kama mkanganyiko wa uumbaji, ambao ulizama katika Mwanzo na vita kati ya Kaini na Abeli, na mnara wa Babeli. “Vita kati ya ndugu ambavyo vilionekana muda mfupi mara baada ya Mungu kuumba mwanamume na mwanamke kwamba: “Kuna hisia ya kupinga kazi ya  uumbaji, hivyo vita daima ni uharibifu. Kwa mfano, Papa ametoa mfano kwamba kufanya kazi ya ardhi, kutunza watoto, kusaidia familia, na kufanya jamii ikue, hii ni kujenga. Kufanya vita ni kuharibu. Ni fundi wa uharibifu”.

Kambi za Libya na makaburi ya Mediterania:Ni lazima kufungamanisha

Katika utaratibu huo huo, Papa Francisko ameingiza matibabu ya kihalifu yaliyotengwa kwa maelfu ya wahamiaji, baadhi ya wafungwa wa kambi za mateso nchini Libya: “Ni kiasi gani wale wanaotaka kukimbia wanateseka mikononi mwa wafanyabiashara”, Papa ameshangaa. Kuna filamu nyingi zimehifadhiwa Kitengo cha Wahamiaji na Wakimbizi cha Baraza la Kipapa la  Maendeleo Fungamani ya  Binadamu. Wanateseka na baadaye kuhatarisha kuvuka Bahari ya Mediterania. Wakati mwingine, wanakataliwa, kwa mtu ambaye kwa wajibu wa ndani anasema: 'Hapana, hawaji hapa',  kuna meli hizi zinazozunguka kutafuta bandari, n zinazorudi au kufia baharini. Hili linatokea leo hii , Papa Francisko amesisitiza tena. Na, kama katika matukio mengine, amerudia kanuni kwamba "kila nchi lazima iseme ni wahamiaji wangapi wanaweza kuchukua kwa sababu "Hili ni tatizo la ndani la kisiasa ambalo linahitaji kufikiriwa na kusema 'ninaweza kufikia namba hiyo. Na wengine? Kuna Umoja wa Ulaya, unapaswa kufikia makubaliano, ili uweze kusawazisha, katika umoja. Hata hivyo, kwa sasa ni ukosefu wa usawa pekee unaoonekana kutokea: Wa kwenda Hispania na Italia, nchi mbili za karibu zaidi na hawawapokei kwingineko. Mhamiaji lazima kila wakati akaribishwe, asindikizwe, ahamasishwe na kufungamanishwa na jamii. Imekubaliwa kwa sababu kuna ugumu, wa kumsindikiza kumuamashisha  na kumuunganisha katika jamii”, Papa amesisitza.  Zaidi ya yote kufungamanisha ili kuepuka ubaguzi na wenye itikadi kali, kama ilivyotokea mkasa wa Zaventem, nchini Ubelgiji, na washambulizi wawili wa Ubelgiji, lakini ni watoto wa wahamiaji waliotengwa. Zaidi ya hayo, wahamiaji ni rasilimali katika nchi ambazo zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa idadi ya watu. Kwa hiyo, Papa Francisko amedokeza kwamba lazima tufikirie kwa akili kuhusu sera ya uhamiaji, sera ya bara. Na ni lazima itufanye tufikirie ukweli kwamba Mediterania ndio kaburi kubwa zaidi barani Ulaya leo".

Kugusa huzuni:haitoshi kuona ni muhimu kuhisi

Vivyo hivyo, Papa, akihojiwa juu ya mada ya mwendesha kipindi iliyosukuma kutafakari juu ya kile kinachoonekana kuwa mgawanyiko mkubwa duniani: sehemu iliyoendelea ambapo kuna uwezekano wa shule, chuo kikuu, kazi; sehemu nyingine na watoto wanaokufa, wahamiaji waliozama, tunaona pia dhuluma katika nchi zetu. Papa anasisitiza, jaribu baya sana ni yale ya kuangalia upande mwingine, si kutazama. Ndiyo, kuna vyombo vya habari vinavyoonesha kila kitu lakini kujitenga; ndio, “tunalalamika kidogo, ‘ni msiba!’ lakini ni kana kwamba hakuna kilichotokea. Haitoshi kuona, ni muhimu kuhisi, ni muhimu kugusa, Papa Francisko amesisitiza. Tunakosa kugusa majeraha nawakati  kugusa hutuongoza kwenye ushujaa. Ninawafikiria madaktari, wauguzi na wakunga ambao walitoa maisha yao katika janga hili: waligusa ubaya na wakachagua kukaa hapo na wagonjwa.

Chukua jukumu la Dunia ili kuisafisha

Kanuni hiyo hiyo inatumika hata kwa ajili ya Dunia. Kwa mara nyingine tena, Papa Francisko amerudia kutoa wito wake wa kutunza kazi ya uumbaji: “Ni elimu ambayo lazima tujifunze. Tahadhari inatoka Amazon na matatizo yake ya ukataji miti, ukosefu wa oksijeni, mabadiliko ya tabianchi: kwa njia hii tunahatarisha kifo cha viumbe hai, tunahatarisha kuua Mama Dunia”, amebainisha Papa Francisko. Ametoa mfano mwingine wa wavuvi wa Mtakatifu Benedikto wa Tronto, Italia ambao waliokota takriban tani milioni 3 za plastiki kwa mwaka na ambao walichukua hatua ya kuondoa taka zote baharini. Kwa maana hiyo amesisitiza kwamba: “Lazima tuweke hili katika vichwa vyetu: kuchukua jukumu la Mama Dunia”.

Uchokozi wa kijamii:kuna uchokozi chanya na hasi

Akiendelea  Papa ameomba kuwa na mtazamo huo wa kujali ambao unaonekana kushindwa pia kutoka katika mtazamo wa kijamii. Leo kile kinachotokea kiukweli ni shida ya uchokozi wa kijamii, kama inavyooneshwa na hali ya uonevu: “Uchokozi wetu huu lazima uelimishwe. Uchokozi wenyewe sio kitu hasi kwa sababu unahitaji kuwa mkali ili kutawala maumbile, kusonga mbele, kujenga, na hivyo kuna uchokozi hata ulio chanya. Lakini kuna uchokozi wa uharibifu ambao huanzia hata kwa kitu kidogo sana lakini ninataka kutaja hapa: huanzia na lugha, gumzo. Lakini gumzo, katika familia, katika vitongoji, huharibu”. Inaharibu utambulisho. Na hii hutokea kati ya watawala, kama kati ya familia. Kwa maana hiyo ninashauri ili lisituangamize ni kujikatalia kupiga soga: kwa maana Ikiwa una jambo moja dhidi ya mwingine au utafune au umwendee na kumwambia uso kwa uso, kuwa jasiri

Ushirikiano wa wazazi:wazazi kuwa na uhuru wa kucheza na watoto

Huku msisitizo ukiwa bado kwa vijana, ambao wakati mwingine ni wahanga wa hisia ya ajabu ya upweke, Papa Francisko amewashauri wazazi wa vijana, wale ambao wakati mwingine wanatatizika kuelewa mateso ya wengine. Papa amekazia kuhusu uhusiano kati ya wazazi na watoto kwamba unaweza kufupishwa kwa neno moja la ukaribu. Huo ni ukaribu na watoto. Wenzi wa ndoa vijana wanapokwenda kuungama au ninapozungumza nao, siku zote mimi ninawauliza maswali: 'Je, unacheza na watoto wako?' Wakati fulani ninasikia majibu ya uchungu: 'Lakini Baba, ninapotoka nyumbani kwenda kazini watoto wamelala na nikirudi usiku wamekwisha lala tena'. Kwa maana hiyo ameongeza kusema "hii ni jamii katili inayojitenga na watoto. Lakini kuwa na uhuru wa  bure na watoto wako: kucheza na watoto wako na sio kuwaogopa watoto, juu ya mambo wanayosema, dhana, au hata wakati mtoto ambaye tayari ni kijana, anateleza, kuwa karibu, kuzungumza kama baba na kama mama. Wale wazazi ambao hawako karibu na watoto wao hawana faida yoyote, lakini ili kukaa na utulivu wanachukua ufunguo wa gari na kwenda. Badala yake ni vizuri sana wakati wazazi wao wanakuwa karibu na watoto wao".

Mwambie ndugu:"Simama!"usimtazame kwa chini

Kuhusu ukaribu, Fazio amekumbuka maneno maarufu ya Papa: “Mtu anaweza kumtazama mtu mwingine kutoka juu hadi chini wakati tu anapomsaidia kuinuka”. Papa Francisko ameongeza wazo hili kwamba “Ni kweli katika jamii tunaona ni mara ngapi tunawatazama wengine kutoka juu hadi chini ili kuwatawala, kuwatiisha na sio kuwasaidia kuinuka. Hebu fikiria ni historia ya kusikitisha ngapi, lakini kila siku inatokea ya wale wafanyakazi ambao wanapaswa kulipa kwa utulivu wa kazi na miili yao, kwa sababu bosi wao anawaangalia kutoka juu hadi chini, lakini kuwatawala. Ni mfano wa kila siku, lakini kweli wa kila siku. Ishara hii, kwa upande mwingine ni halali tu kufanya kitendo cha kitukufu, yaani kunyoosha mkono wako na kusema amka kaka, inuka dada”. Mazungumzo hayo yalipanuka na kugusa dhana ya uhuru ambayo ni zawadi ya Mungu lakini ambayo ina uwezo pia wa kufanya madhara mengi. Kama Mungu alivyotuumba kuwa huru, sisi ni watawala wa maamuzi yetu na pia wa kufanya maamuzi mbaya” amesema Papa Francisko.

Uwezo wa Kusamehe ni haki ya binadamu

Swali la Fazio akikaa katika dhana ya Uovu: Je, kuna mtu yeyote ambaye hastahili msamaha na huruma ya Mungu au msamaha wa wanadamu? Papa amejibu jambo ambalo alisema labda amesema litamkashifu mtu. “Uwezo wa kusamehewa ni haki ya binadamu. Sisi sote tuna haki ya kusamehewa ikiwa tunaomba msamaha. Ni haki inayotokana kwa usahihi na asili ya Mungu na imetolewa kama urithi kwa wanadamu. Tumesahau kwamba mtu anayeomba msamaha ana haki ya kusamehewa. Ulifanya kitu, unalipa. Hapana! Una haki ya kusamehewa, na ikiwa una deni lolote na jamii, panga kulipa, lakini kwa msamaha”.

Uovu dhidi ya wasio na hatia:kwa nini watoto wanateseka?

Hata hivyo, kuna Uovu mwingine, usioelezeka ambao nyakati fulani huwapata wasio na hatia, na ambao tunashangaa kwa nini Mungu haingilii kati, amesema Fazio. Papa Francisko kwa kujibu amesema: “Maovu mengi sana huja kwa usahihi kwa sababu mwanadamu amepoteza uwezo wa kufuata sheria, amebadilisha asili, amebadilisha mambo mengi, na pia kwa sababu ya udhaifu wake wa kibinadamu. Na Mungu anaruhusu hili liendelee mbele. Bila shaka, maswali yanabaki wazi: “Kwa nini watoto wanateseka?". Papa amekiri kwamba: “Sipati maelezo kwa hili. Nina imani, ninajaribu kumpenda Mungu ambaye ni baba yangu, lakini najiuliza: 'Lakini kwa nini watoto wanateseka?' Na hakuna jibu. Yeye ni mwenye nguvu, naam, mwenye nguvu katika upendo. Badala yake, chuki, uharibifu, viko mikononi mwa mtu mwingine aliyepanda uovu duniani kwa kijicho”. Onyo la Papa Francisko ni kwamba "Katika uovu hakuna kuzungumza" na  kwamba "kufanya mazungumzo na Uovu ni hatari: Na watu wengi hupenda, kujaribu mazungumzo na Uovu, hata mimi pia nimejikuta katika hali kama hii mara nyingi, lakini ninajiuliza kwa nini, mazungumzo na Uovu, hilo ni jambo baya ... Mazungumzo na Uovu si mazuri, hii ni sawa sawa na majaribu yote. Na jaribu hili linapokujia, ‘kwanini watoto wanateseka?’, ninapata njia moja tu: kuteseka pamoja nao. Katika hili, mwalimu mkubwa alikuwa Dostoevsky".

Kanisa la hija la wakati ujao

Wakati ujao wa ulimwengu na wa Kanisa pia umechukua nafasi pana katika mahojiano ya Papa. Mustakabali wa ulimwengu, kama inavyooneshwa katika Waraka wa ‘Fratelli tutti’ yaani wote ni ndugu huku mwanadamu akiwa ndiye kitovu cha uchumi na chaguzi. Hiki ni kipaumbele ambacho Papa amesema ameshiriki na wakuu wengi wa nchi ambao wana mawazo mazuri. Hata hivyo, maadili haya yanapingana na hali ya kisiasa na kijamii, ikiwa ni pamoja na yale ya siasa za dunia, ambazo huzuia nia nzuri, amebainisha. Kuhusu mustakabali wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko  amekumbuka sura ya Kanisa iliyoainishwa na Papa Paulo VI katika Waraka wake wwa kituma e Evangelii Nuntiandi, ambao amesema ni mwongozo wa  Waraka wake wa  Evangelii Gaudium: “Kanisa la Hija”. Papa  Francisko amerudia kusisitiza tena kuwa leo, uovu mkubwa zaidi wa Kanisa ni roho ya  ulimwengu ambayo, kwa upande mwingine, hufanya kukuza jambo baya,  la ukasisi, ambao ni upotovu wa Kanisa. Ukleri uliopo katika ugumu, na chini ya kila aina ya ugumu kuna uozo, siku zote, amerudia kusema Papa Fransisko, akihesabu miongoni mwa mambo mabaya katika Kanisa la leo hii kuhusu misimamo migumu, isiyobadilika na kiitikadi inayochukua nafasi ya Injili. Papa Francisko amesema “Katika mitazamo ya kichungaji nitataja mbili tu, ambazo ni za zamani: Pelagianism na Gnosticism. Pelagianism ni kuamini kwamba kwa nguvu zangu naweza kusonga mbele. Hapana, Kanisa linasonga mbele kwa nguvu za Mungu, huruma ya Mungu na nguvu za Roho Mtakatifu. Na Gnosticism, ile ya ufumbo, bila Mungu, hiyo ya roho  tupu ... hapana, bila mwili wa Kristo hakuna ufahamu unaowezekana, bila mwili wa Kristo hakuna ukombozi unaowezekana; Lazima turudi tena katikati : 'Neno lilifanyika mwili'. Katika kashfa hii ya msalaba, ya neno lililofanyika mwili, kuna mustakabali wa Kanisa”, amesema Papa.

Umuhimu wa kusali kama mtoto mdogo anayeuliza maswali

Papa Francisko katika mahojiano hayo ameleza umuhimu wa kusali: “Kusali  ni kama vile mtoto anafanya anapohisi kuwa na kizingiti, hana msaada, [anasema] ‘baba, mama’. Kuomba kunamaanisha kutazama mipaka yetu, mahitaji yetu, dhambi zetu .... Kusali ni kuingia kwa nguvu, nje ya mipaka, zaidi ya upeo wa macho, na kwetu sisi Wakristo kusali ni kukutana na 'baba'. Na mtoto huwa hamsubiri baba yake amjibu, baba akianza kujibu linaulizwa swali jingine. Anachotaka mtoto ni kwamba macho ya baba yawe juu yake. Haujalishi ufafanuzi, kilicho muhimu tu ni  kwamba baba anamtazama, na hii inampa usalama”.

Marafiki wa kweli:kila mmoja ana kasoro lakini marafiki ni muhimu

Maswali mengine yaligusa sehemu za kibinafsi zaidi: “Je! Una marafiki wa kweli? Papa amejibu “Nina kasoro zangu eh, lakini kama mtu wa kawaida ambaye ana marafiki; na ninapenda kuwa na marafiki wakati mwingine kuwaambia mambo yangu, kusikiliza yao, lakini kinyume chake nahitaji marafiki. Na ndito moja ya sababu, ya  kwa nini sikwenda kuishi katika ghorofa ya Kipapa, kwa sababu mapapa waliokuwa hapo awali walikuwa Watakatifu na mimi siwezi kusimamia peke yangu, mimi si mtakatifu sana. Ninahitaji mahusiano ya kibinadamu, ndiyo maana naishi katika hoteli hii ya Mtakatifu  Marta ambako kuna watu wanaozungumza na kila mtu, ninapata marafiki. Ni maisha rahisi kwangu, sijisikii kufanya maisha mengine, sina nguvu na urafiki hunanipatia nguvu. Hakika, ninahitaji marafiki, ni wachache eh, ni wachache lakini wa kweli”.

Utoto,uzoefu,muziki wa kizamani na televisheni kidogo

Wakati wa mahojiano hapakukosekana  marejeo ya zamani na utoto wake  huko Buenos Aires, kwa kushangilia Mtakatifu Laurenti , kwa  ajili ya wito, na tamanio la kuwa muuzaji wa nyama, kwa uzoefu katika maabara ya kemia, utafiti uliomshawishi sana lakini ambao ulishinda kwa  wito wa Mungu. Bado kuhusu  suala la usiri, Papa amekumbuka nadhiri aliyoitolea kwa Mama Yetu wa Mlima Karmeli, mnamo tarehe 16 Julai 1990, kutotazama TV na kwamba "Sitazami televisheni; hii si kwa sababu ya hukumu”. Upendo, kwa upande mwingine, ni katika muziki, hasa muziki wa kizamani na tango: "porteno ambaye hachezi tango sio porteno", amesema Papa . Baadaye amezungumumzia juu ya ucheshi ambayo, anasema, "ni dawa", na ameshauri kutafuta sala ya Mtatifu Thomas More kuomba ucheshi.

Kuomba sala 100

Kama ilivyo kila hotuba zake zote, Papa Francisko amemalizia akiomba sala kwa ajili yake. Amesema: “Ninaihitaji, na ikiwa yeyote kati yenu hajaomba kwa sababu haamini, hajui au hawezi lakini anaweza kuwa na mawazo mazuri, mawimbi mazuri. Nahitaji ukaribu wa watu”. Mahojiano hayo yaliisha kwa picha iliyochukuliwa kutoka katika filamu ya baada ya vita: "Ili kukamilisha mazungumzo, Papa amesema ninadhani alikuwa ni Vittorio De Sica ambaye alikuwa mtabiri, na alisoma mikono yake kwamba  'asante 100 lire', nami ninawaambia  kwamba 'sala 100',  '100 lire, sala 100'.  Asante”.

Sala nzuri ya ucheshi ya Mtakatifu Thomas More aliyoshauri Papa wakati wa mahojiano na mwandishi Fabio Fazio wa kipindi cha “Che Tempo Fa”katika TG3

Bwana, nipe usagaji wa chakula vizuri na pia kitu cha kusagia. Nipe afya ya mwili, na ucheshi mzuri unaohitajika kuudumisha.

Nipe, Ee Bwana, roho takatifu, ambayo huweka hazina iliyo nzuri na safi, ili isiogope dhambi, lakini itafute njia mbele zako ya kurekebisha mambo tena.

Nipe roho isiyojua kuchoshwa, kunung'unika, kuguna na kuomboleza, na usiniruhusu nihangaike sana juu ya kitu hicho cha kuvamia kinachoitwa “mimi”.

Nipe, Ee Bwana, hali ya ucheshi, nipe neema ya kuelewa mzaha, ili nijue furaha kidogo maishani na niweze kuwa sehemu yake kwa wengine pia.

06 February 2022, 21:50