Papa Francisko Asikitishwa na Mauaji ya Kigaidi Nchini DRC
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na mauaji ya kigaidi yaliyotokea tarehe 1 Februari 2022 huko kwenye Kambi ya wakimbizi na wahamiaji ya “Plaine Savo”, iliyoko Ituri, Kaskazini Mashariki mwa DRC na kusababisha watu 53 kupoteza maisha na wengine 36 kujeruhiwa vibaya sana. Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Rais Félix Antoine Tshilombo Tshisekedi wa DRC, anasema, anawaombea watu walipoteza maisha yao katika shambulio hili la kigaidi, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo aweze kuwapokea na kuwajalia mwanga wa milele ili waweze kupumzika katika usingizi wa amani. Awalinde na kuwafariji wale wote wanaoomboleza kutokana na msiba huu mzito.
Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea faraja na uponyaji wa haraka, wale wote walioathirika kutokana na shambulizi hili na anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa sala na sadaka yake. Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutumia fursa hii, kulaani vitendo vyote vya kigaidi ambao ni chanzo kikuu cha maafa na mateso kwa watu wasiokuwa na hatia kwa DRC ambayo bado ina majeraha makubwa ya vita. Baba Mtakatifu anapenda kuwaombea zawadi ya amani kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama sehemu ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Mwishoni mwa ujumbe huu, Baba Mtakatifu anamwomba Rais Félix Antoine Tshilombo Tshisekedi wa DRC kumfikishia salama zake za rambirambi kwa watu wa Mungu nchini DRC.