Tafuta

Baba Mtakatifu anayataka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kuhakikisha kwamba, yanaweka sera na mikakati kwa ajili ya majiundo endelevu ya mapadre walezi seminarini. Baba Mtakatifu anayataka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kuhakikisha kwamba, yanaweka sera na mikakati kwa ajili ya majiundo endelevu ya mapadre walezi seminarini. 

Papa Francisko Dumisheni Malezi Endelevu Kwa Walezi Seminarini

Semina hii inaongozwa na kauli mbiu “Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.” Yn 8:36. Hawa ni Mapadre waliopewa dhamana ya kulea wito wa Kipadre, kumbe, wanapaswa kuwasaidia Majandokasisi kukua na kukomaa katika uhuru wa kweli. Hii imekuwa ni fursa ya kufafanua maana halisi ya uhuru, ili kuwafunda waseminarikatika dhana ya uhuru unaowawajibisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utambulisho wa: wito, maisha na utume wa Kipadre unafumbatwa katika ufuasi wa Kristo Yesu, huduma makini ndani ya Kanisa na ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Malezi, makuzi na majiundo ya kipadre ni changamoto pevu inayomtaka Jandokasisi kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zake, daima akijitahidi kujiandaa ili kuwa ni Baba mwema na mhudumu wa Jumuiya inayomzunguka. Hiki ni kielelezo cha Ubaba katika maisha ya Kipadre kwa ajili ya kusaidia mchakato wa ukuaji wa maisha sanjari na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika maisha ya kijumuiya, dhamana inayotekelezwa kwa ujasiri, nguvu na upendo unaotangazwa na kushuhudiwa na walezi Seminarini. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 2 Februari 2022 ametambua uwepo wa Mapadre walezi wa seminari waliokuwa wanashiriki katika semina maalum kwa ajili ya malezi ya Majandokasisi. Kuna Mapadre wema na watakatifu ambao wameshiriki kikamilifu katika mchakato wa historia ya wokovu ambayo inaendelea kuandikwa hadi leo hii, mwaliko ni kuhakikisha kwamba hata wao wanarithisha kwa wengine utamaduni huu, kwa kutambua majina ya watu wao! Baba Mtakatifu anasema, familia ya Mungu inakabiliwa na changamoto nyingi za maisha, kumbe, ni wajibu wa Mapadre kuwasaidia watu wao.

Sera jna mikakati ya majiundo endelevu ni muhimu kwa walezi seminarini
Sera jna mikakati ya majiundo endelevu ni muhimu kwa walezi seminarini

Chuo Kikuu cha Kipapa cha “Santa Croce” mjini Roma kuanzia tarehe 31 Januari hadi tarehe 4 Februari 2022 kimeendesha awamu ya Saba ya Malezi na Majiundo kwa Walezi Seminarini. Semina hii imeongozwa na kauli mbiu “Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.” Yn 8:36. Hawa ni Mapadre waliopewa dhamana ya kulea wito wa Kipadre, kumbe, wanapaswa kuwasaidia Majandokasisi kukua na kukomaa katika uhuru wa kweli. Hii imekuwa ni fursa ya kufafanua maana halisi ya uhuru, ili kuwafunda Majandokasisi katika dhana ya uhuru unaowawajibisha na utakaowawezesha kuishi vyema kama Mapadre. Askofu mkuu Lazarus You Heung-sik Mwenyekiti wa Baraza la Wakleri pamoja na Mheshimiwa Padre Luis Felipe Navarro Marfà wameshiriki kutoa mada katika semina hii. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Majandokasisi wasikimbilie Seminarini ili kupata elimu bora zaidi itakayowasaidia kuupatia umaskini kisogo, kwani mwelekeo huu ni potofu! Wanapaswa kujisadaka na kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza, kwa kuwa maskini kwa ajili ya maskini. Seminari ziwe ni Mama na kuta za kulinda wito na maisha yao ya Kipadre; kwani umaskini unakuwa ni chemchemi ya maisha na ngao ya maisha na utume wa Kipadre. Mapadre wajifunze na kujenga utamaduni wa kuwasikiliza na kukaa na watu wao; kwa kuwajali na kuwahudumia wagonjwa, wazee, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Nguzo za malezi seminarini zipewe kipaumbele cha pekee.
Nguzo za malezi seminarini zipewe kipaumbele cha pekee.

Ukaribu wa wakleri kwa watu wao ni msaada mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia! Changamoto hii inakwenda sanjari na kujitaabisha kumfahamu Kristo Yesu kwa njia ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, Sala binafsi na za Kijumuiya kama sehemu ya mwendelezo wa maisha hata katika hali ya mchoko! Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu anasema ni vyema kusinzia mbele ya Tabernakulo kuliko kupitiliza siku bila ya kwenda kumsalimia Yesu wa Ekaristi Takatifu, anayewaita na kuwatuma kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu yaani Neno la Mungu. Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji haina budi kujikita katika mchakato wa majadiliano endelevu na fungamani kwa kumtumainia Roho Mtakatifu mhimili mkuu katika azma ya Uinjilishaji, tayari kung’amua kile ambacho Roho Mtakatifu anataka kwa ajili ya watu wake. Wakleri wanapaswa kujenga fadhila ya unyenyekevu mbele ya Roho Mtakatifu. Kumbe, Seminari iwe ni mahali pa kujifunza: kusoma na kusali ili kupata ujuzi, maarifa na stadi za maisha. Majandokasisi wajitahidi kusoma kwa bidii, juhudi na maarifa ili kujiandaa kikamilifu na changamoto zilizoko mbele yao kama Mapadre!

Maisha ya Kijumuya na kazi za kitume ni mambo muhimu sana katika majiundo ya Kikasisi; mihimili hii mikuu ya maisha na wito wa Kipadre ipewe uzito unaostahili. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Majandokasisi kumkimbilia Roho Mtakatifu ili aweze kuwajalia karama zake, ari na moyo wa kimisionari, tayari kutoka kimasomaso ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Mapadre wawe na ujasiri wa Kibaba kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wazee na wagonjwa walioko kufani; kwa ajili ya kuwapatia Sakramenti wanaohitaji! Huu ni ushuhuda wa Padre anayejisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zake. Majandokasisi wanapaswa kuonesha ukomavu na kamwe wasiwe ni watu kupika majungu, “kwani kama majungu si mtaji, yangekuwa mtaji, wengi wangetajirika wengi!

Malezi Endelevu

 

05 February 2022, 14:42