Baba Mtakatifu Francisko Barua Binafsi “Motu proprio Fidem servare” yaani “Kulinda Imani” Rej. 2 Tim 4:7. Baba Mtakatifu Francisko Barua Binafsi “Motu proprio Fidem servare” yaani “Kulinda Imani” Rej. 2 Tim 4:7.  

Papa Francisko Barua Binafsi "Fidem Servare": Kulinda Imani

Barua Binafsi “Motu proprio Fidem servare” yaani “Kulinda Imani” Rej. 2 Tim 4:7. Amefanya mabadiliko makubwa kwenye Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, kwa kutenganisha muundo wa Baraza. Kwa sasa kutakuwa na vitengo vikuu viwili: Mafundisho Sadikifu ya Kanisa: Imani, Maadili na Utu wema. Pili Nidhamu na masuala maalum yaliyotengwa kwa ajili ya ofisi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa Barua Binafsi “Motu proprio Fidem servare” yaani “Kulinda Imani” Rej. 2 Tim 4:7. Amefanya mabadiliko makubwa kwenye Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, kwa kutenganisha muundo wa Baraza. Kwa sasa kutakuwa na vitengo vikuu viwili: Mafundisho Sadikifu ya Kanisa na Nidhamu. Kila kitengo kitakuwa na Katibu wake. Kitengo cha Mafundisho Tanzu ya Kanisa itajihusisha na masuala ya imani ya Kanisa pamoja na kanuni maadili na utu wema. Kitengo cha pili kitajielekeza zaidi na masuala ya nidhamu yaliyotengwa maalum kwa ajili ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na kutakuwa na ushirikiano mkubwa na Mahakama Kuu ya Kitume “Segnatura Apostolica” iliyoanzishwa kwa madhumuni haya. Baba Mtakatifu Francisko katika Barua Binafsi “Motu proprio Fidem servare” yaani “Kulinda Imani” Rej. 2 Tim 4:7, anasema, kulinda imani ni kigezo muhimu sana kinachopaswa kufuatwa ndani ya Kanisa, dhamana inayotekelezwa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, kama ambayo imendelezwa na viongozi wakuu wa Kanisa waliomtangulia. Mtakatifu Paulo VI aliwahi kufanya mabadiliko makubwa kwenye Baraza hili katika Barua yake Binafsi “Integrae servandae” na Mtakatifu Yohane Paulo II katika Katiba ya Kitume ya “Pastor bonus” inayofafanua malengo na majukumu yake katika maisha na utume wa Kanisa.

Kulinda Imani, Maadili na Nidhamu ya Kanisa
Kulinda Imani, Maadili na Nidhamu ya Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko kwa kusoma alama za nyakati amefanya mabadiliko makubwa kwenye muundo wa Baraza na hivyo kuwa na vitengo vikuu viwili, vitakavyokuwa na Makatibu wake wake wakuu, Makatibu waambata na wakuu wa ofisi. Kitengo cha Mafundisho Sadikifu ya Kanisa kitashughulikia masuala ya imani, kanuni maadili na utu wema. Kitengo hiki kitakuwa pia na dhamana ya kuboresha akili na urithishaji wa imani kama sehemu ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda. Ni kitengo kitakachokuwa mstari wa mbele, ili kukabiliana na changamoto za maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Kitengo hiki, kitahariri nyaraka mbalimbali zitakazokuwa zinachapishwa na Mabaraza ya Kipapa; machapisho yenye utata wa kiimani na maoni yanayokinzana na imani ya kweli. Kitengo kitakuwa na dhamana ya kuanzisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi na makundi haya tata na kuangalia jinsi ya kurekebisha hali na mitazamo kama hii mintarafu Sheria, kanuni na taratibu zinazobainishwa na “Agendi ratio in doctrianum examine.” Kitashughulikia pia masuala yote yaliyobainishwa kwenye Katiba ya Kitume ya “Anglicanorum coetibus” pamoja na masuala ya Sakramenti ya Ndoa mintarafu Sheria, Kanuni na taratibu za “Privilegium fidei” yaani “Upendeleo wa imani.”

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kitengo cha Nidhamu kitajielekeza zaidi na masuala ya nidhamu yaliyotengwa maalum kwa ajili ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na kutakuwa na ushirikiano mkubwa na Mahakama Kuu ya Kitume “Segnatura Apostolica” iliyoanzishwa kwa madhumuni haya kwa kushirikiana na idara na vikao maalum. Ni kitengo kitakachojielekeza zaidi katika masuala ya malezi na majiundo kwa wadau katika Sheria za Kanisa, ili kuzifahamu na hatimaye, kuzitekeleza kikamilifu. Kitengo kitakuwa na Pango hifadhi za nyaraka na kitaendelea kusimamia na kuratibu Pango hifadhi za nyaraka za “Baraza la Kipapa la “S. Uffizio na Indice.” Barua Binafsi “Motu proprio Fidem servare” yaani “Kulinda Imani” Rej. 2 Tim 4:7 inaanza kufanya kazi rasmi kuanzia tarehe 14 Februari 2022 baada ya kuchapishwa kwenye Gazeti la L’Osservatore Romano na “Acta Apostolicae Sedis.”

Papa Linda Imani
15 February 2022, 15:13