Tafuta

Papa Francisko: Uongozi ni kielelezo cha huduma ya hali ya juu kabisa ya upendo kwa watu wa Mungu. Papa Francisko: Uongozi ni kielelezo cha huduma ya hali ya juu kabisa ya upendo kwa watu wa Mungu. 

Papa Francisko: Uongozi Ni Kielelezo Cha Juu Kabisa Cha Huduma ya Upendo

Papa Francisko: Uongozi ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo. Watoe kipaumbele cha kwanza kwa watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, aliyeteswa na hatimaye akafia nje ya kuta za mji wa Yerusalemu. Wawe mstari wa mbele kusimama kidete kulinda na kutetea amani jamii ambayo ni shirikishi na inawajibisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha Kitaifa cha Mameya wa Manispaa za Italia ANCI, “Associazione Nazionale Comuni Italiani, ANCI” kilianzishwa rasmi kunako mwaka 1901 na kinashirikisha Manisipaa 7, 041 kadiri ya takwimu zilizotolewa kunako mwaka 2018. Hii ni sawa na asilimia 90% ya idadi ya watu wote nchini Italia. Tangu tarehe 2 Oktoba 2016 Bwana Antonio Decaro ndiye Rais wake. Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 5 Februari 2022 amekutana na kuzungumza na Mameya wa Manisipaa za Italia, ambao wametoa mchango mkubwa sana katika mapambano dhidi ya janga la maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Wamekuwa chachu ya matumaini kwa watu wa Mungu kuendelea kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu licha ya changamko kubwa zilizosababishwa na UVIKO-19. Baba Mtakatifu anasema, Mameya wamekuwa mstari wa mbele ili kuhakikisha kwamba, sheria, kanuni na taratibu dhidi ya UVIKO-19 zinatekelezwa kwa dhati, kwa ajili ya usalama wa afya ya raia, kwa kuchukua maamuzi mazito kwa wakati muafaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ametumia fursa hii, kuwatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu wakijikita zaidi katika uongozi kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo.

Watoe kipaumbele cha kwanza kwa watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, aliyeteswa na hatimaye akafia nje ya kuta za mji wa Yerusalemu. Wawe mstari wa mbele kusimama kidete kulinda na kutetea amani jamii ambayo ni shirikishi na inawajibisha. Baba Mtakatifu anakiri na kutambua uzito wa kazi inayotekelezwa na Mameya wa Manisipaa na miji mbalimbali nchini Italia na ukaribu wao kwa watu wa Mungu ili waweze kuwahudumia. Lakini, wakati mwingine, ni viongozi wanaohisi upweke katika maisha yao kutokana na maamuzi magumu wanayopaswa kufanya, kwa watu kudhani kwamba, demokrasia ni sawa na “maji kwa glasi”. Lakini kimsingi demokrasia ya kweli inadai ushiriki mkamilifu wa wananchi ili kweli Manisipaa iweze kusimikwa katika uongozi bora. Wananchi wengi wanadhani kwamba, Meya ni suluhu ya kila tatizo na changamoto inayojitokeza kwenye mji au manisipaa yake na kwamba, kila jambo linawezekana, kwa kutumia rasilimali fedha, “sabuni ya roho”. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na mitandao ya mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo.

Viongozi wadumishe amani jamii kwa mafungamano ya watu
Viongozi wadumishe amani jamii kwa mafungamano ya watu

Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umeonesha udhaifu na mapungufu ya binadamu; umeamsha ukarimu na upendo kwa jirani pamoja na watu wengi kujitolea kwa ajili ya huduma kwa jirani zao kama wale wahudumu katika sekta ya afya na wafanyakazi wengi, waliojisadaka kwa ajili ya kupunguza makali ya machungu kwa jirani zao, hususan wazee na maskini. Huu ni mtandao wa Injili ya Huruma na Upendo unaopaswa kulindwa na kudumishwa, ili kukoleza mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika huduma. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu amependa kukazia mambo makuu matatu. Kwanza kabisa amewatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu wakijikita zaidi katika huduma kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo kama inavyoweza kutendeka ndani ya familia, kwa kukuza na kudumisha utamaduni wa kusikiliza watu na matatizo yao kwa makini, ili kutambua mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika huduma kwa watu wa Mungu.

Kusikiliza ni kipaji na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, shukrani kwa Mameya ambao wametoa nafasi ya pekee kusikiliza na kujibu shida na matamanio halali ya raia wao. Utamaduni wa kusikiliza unapaswa kusindikizwa na ujasiri katika uongozi, kwa kutumia vyema rasilimali fedha sanjari na kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu ambako ni chimbuko la majanga ya kijamii. Shule inapaswa kuwa ni mahali pa mchakato wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya kijami, lakini kwa bahati mbaya, pamegeuka kuwa ni uwanja wa fujo na ghasia. Shule ni mahali ambapo, sheria, taratibu na kanuni za maisha zinafundishwa na kurithishwa, lakini leo hii, sekta ya elimu katika ujumla wake, imegeuka kuwa ni “chaka la rushwa na ufisadi wa mali ya umma.” Ili kutekeleza ndoto ya kuwa na manisipaa bora inayokidhi mahitaji ya raia wake, ndoto hii haina budi kuwashirikisha wadau mbalimbali katika manisipaa au mji husika, kama ujenzi wa mafungamano ya kijamii.

Maskini ni amana na utajiri wa jamii.
Maskini ni amana na utajiri wa jamii.

Pili, anasema Baba Mtakatifu Mameya wa manisipaa watoe kipaumbele cha kwanza kwa watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, aliyeteswa na hatimaye akafia nje ya kuta za mji wa Yerusalemu. Pembezoni mwa vipaumbele vya jamii ni chanzo kikuu cha ghasia na uvunjifu wa sheria, taratibu na kanuni za jamii. Huko ni mahali ambapo watu wanahisi kutokukubalika wala kupendwa. Changamoto ni kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, ili hatimaye, watu wote waweze kupata huduma makini. Ikumbukwe kwamba, maskini ni amana na utajiri wa jamii, wanaopaswa kuonjeshwa mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Mshikamano ni kati ya mambo msingi katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, yaliyoibuliwa na kuendelezwa kwa namna ya pekee na Mtakatifu Yohane Paulo II. Kutokana na maambukizi makubwa ya UVIKO-19 kuna watu wamepoteza fursa za ajira; wazee na wagonjwa wameonja upweke hasi katika maisha yao, vijana wengi wametumbukia katika ugonjwa wa sonona kiasi cha kujikatia tamaa ya maisha. Pengo kati ya matajiri na maskini limeongezeka maradufu, kiasi kwamba, familia nyingi zinakabiliana na kiwango kikubwa cha umaskini wa hali na kipato. Watu wanaoishi pembezoni mwa jamii, wanapaswa kugeuzwa na kuwa ni maabara ya uchumi na jamii mpya, kwa kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kazi ni mafuta ya utu, heshima na haki msingi za binadamu anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Tatu, anasema Baba Mtakatifu ni Amani Jamii, inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu, kwa sababu hiki ni kipimo makini cha mahusiano na mafungamano mema ya kijamii ndani ya mji. Kumbe, kuna haja ya kupambana kikamilifu na tofauti za kitamaduni na kijamii zinazoweza kusababisha amani jamii kutoweka. Jambo la msingi ni kujenga utamaduni wa kujadiliana katika ukweli na uwazi na kwamba, umoja na mshikamano hushinda vurugu na ghasia. Panapotokea mgogoro kuna watu huutaza bila kufanya jambo lolote na kuendelea na shughuli zao. Wengine wanaukumbatia kiasi cha kugeuka na kuwa ni wafungwa wake, kwa kupoteza dira na mwelekeo, kiasi cha kugumisha mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano. Njia bora ya kushughulikia migogoro ni utayari wa kukabiliana na mgogoro uso kwa uso, kuutatua na kuufanya kuwa kiungo katika mnyororo wa mchakato mpya kwani, heri wapatanishi. Rej.  Evangelium gaudium, 227. Amani Jamii ni matunda ya mchakato wa kuweka pamoja miito, uwezo na rasilimali mbalimbali. Mahusiano na mafungamano ya kijamii ni muhimu sana katika katika kujenga na kudumisha amani jamii inayosimikwa katika maisha ya kila siku, kwa kutambua pia kanuni auni inayoweza kusaidia mchakato wa maendeleo hata katika ngazi ya mtu binafsi. Kumbe, kuna haja kwa viongozi kuwa karibu zaidi na raia wao, ili kutekeleza vyema wajibu na dhamana yao, kamwe wasiwakimbie watu wao, bali wawe na ujasiri wa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao yao kama anavyokazia Mtakatifu Yohane Paulo II. Hii ni hazina na mafundisho yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu.

Papa Uongozi Huduma
05 February 2022, 15:42