Kumbukizi la Miaka Miwili ya Wosia wa Kitume "Querida Amazonia"
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019 yalinogeshwa na kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ikolojia fungamani.” Baba Mtakatifu Francisko tarehe 2 Februari 2020 alitoa Wosia wa Kitume mara baada ya Sinodi unaojulikana kama “Querida Amazonia” yaani “Amazonia Mpendwa.” Katika Wosia huu wa Kitume, Baba Mtakatifu anaelezea maana ya wosia huu kuwa ni muhtasari ya mambo mazito yaliyojadiliwa katika Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia unaoziunganisha nchi tisa. Lengo ni kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kulinda na kuendeleza utunzaji bora wa mazingira bora nyumba ya wote. Ni ndoto ya kutaka kuona kwamba, Ukanda wa Amazonia unalinda uoto wa asili sanjari na kujikita katika ukarimu wa watoto wa Ukanda wa Amazonia ili kulipyaisha Kanisa na kulipatia watoto wapya. Baba Mtakatifu anagusia kuhusu ndoto za kijamii zinazokita ujumbe wake katika msamaha na ujenzi wa jumuiya ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia.
Kitamaduni, Baba Mtakatifu anaonesha kwamba, Ukanda huu ni mali ya watu wengi, udhaifu wa taasisi za Ukanda wa Amazonia; umuhimu wa majadiliano ya kijamii, kwa kulinda na kutunza mizizi ya kitaifa, ili kuendeleza mchakato wa ujenzi wa majadiliano na watu kukutana sanjari na kulinda tamaduni za watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia ambao wako kwenye hatari ya kutoweka. Ndoto ya Kiikolojia inajihusisha na rasilimali maji; umuhimu wa kusikiliza na kujibu kilio cha watu wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kufanya tafakari ya kinabii. Ndoto ya Kikanisa kwa ajili ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia ni kutangaza na kushuhudia Injili kama sehemu ya imani tendaji. Hii ni changaoto inayokwenda sanjari na mchakato wa utamadunisho wa maisha ya kiroho, Liturujia ya Kanisa, utume wa viongozi wa Kanisa, Jumuiya za Kikristo zinazoshuhudia uhai, nafasi na dhamana ya wanawake; ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano sanjari na kukazia mchakato wa majadiliano ya kiekumene, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anauweka Wosia wa Kitume mara baada ya Sinodi unaojulikana kama “Querida Amazonia” yaani “Amazonia Mpendwa” chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa.
Ni katika muktadha huu, Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, kama sehemu ya mchakato wa kumbukizi la miaka miwili tangu kuchapishwa kwa Wosia huu wa Kitume, anasema, unakita ujumbe wake kwa watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia; kwa kuheshimu na kuthamini sauti zao, kama mwelekeo sahihi wa wongofu wa kweli na matunda yake yataonekana kwa wakati muafaka. Ni wosia muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia, unaoongozwa na Roho Mtakatifu kama eneo la kitaalimungu, ili kuamsha nyoyo za walimwengu na Kanisa katika ujumla wake. Ni Wosia unaobeba ndoto za Baba Mtakatifu Francisko katika medani mbalimbali za maisha ya watu wa Mungu. Huu ni ufunuo wa Fumbo la maisha ya Mungu na ushuhuda wa Kanisa ambalo lina sura mbili ya dhambi na utakatifu. Mwenyezi Mungu anaendelea kujifunua kwa waja wake licha ya woga na wasi wasi wa mabadiliko au baadhi ya watu kutaka kupandikiza sera na mitazamo yao binafsi.
Huu ni Wosia unaowalenga watu wa Mungu wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii; hawa watu wa Mungu kwa sasa wamekuwa ni mawe hai ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Hapa ni mahali pa toba, wongofu wa ndani na uponyaji wa kweli, ili kuliwezesha Kanisa kuweza kuibuka tena kidedea na kuwa ni chemchemi ya Injili ya uhai. Hili ni Kanisa linalotaka kujikita katika umoja, ushiriki na utume kama kielelezo cha mpango mkakati wa shughuli za kichungaji kwa Kanisa Ukanda wa Amazonia na Ulimwengu katika ujumla wake. Ukanda wa Amazoni ni mahali pa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana, ili kuhakikisha kwamba, watu wote wa Mungu wanadumisha umoja, ushiriki na utume, kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kwa mwaka 2021 hadi mwaka 2023.
Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, anasema, Baba Mtakatifu Francisko kutokana na busara za kichungaji, ameanzisha kwa majaribio “Ad experimentum” Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, “The Ecclesial Conference of the Amazon, CEAMA” linalojikita katika njia ya umisionari. CEAM inaunganisha miundo mbinu ya: Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Amerika ya Kusini na Caribbean, CLAR, Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean pamoja na “Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini”, (Pan-Amazon Ecclesial Network of the Latin American Church, REPAM). Tume na Makundi mbalimbal yaliyoundwa kumwilisha Wosia wa Baba Mtakatifu yanaendelea kufanya kazi mintarafu mwanga wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Roho Mtakatifu anaendelea kutoa changamoto nyingi katika maisha na utume wa Kanisa Ukanda wa Amazonia na matunda na zawadi za Roho Mtakatifu zinaanza kujionesha ili kuchipusha maisha mapya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo!