Watakatifu Cyril na Method: Upatanisho, Udugu na Amani ya Kweli Barani Ulaya
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Watakatifu Cyril na Method, Wasimamizi wa Bara la Ulaya, wanaheshimiwa sana na familia ya Mungu huko Czech na Slovakia, kutokana na mchango wao katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho, amana na utajiri mkubwa ulioachwa na ndugu hawa pacha katika maisha na utume wa Kanisa! Ni ndugu ambao wameacha urithi mkubwa wa tunu msingi za maadili, kiasi kwamba, Ukristo umekuwa ni chemchemi ya matumaini hasa wakati wa giza na mahangaiko ya watu! Walichangia kutafsiri Biblia ambayo ni msingi wa maisha ya kiroho na maendeleo ya kitamaduni; rejea ya sheria katika nchi mbalimbali duniani. Watakatifu hawa pacha wanakumbukwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Februari ya kila mwaka. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuhitimisha Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Mtakatifu Yosefu, 16 Februari 2022, amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja naye, ili kuwaomba watakatifu hawa pacha, ili kuziombea nchi za Bara la Ulaya kwa Mwenyezi Mungu. Nchi hizi ziweze kutambua mizizi ya Ukristo, ili kuamsha na kupyaisha ari na mwamko wa upatanisho, mshikamano na udugu wa kibinadamu sanjari na amani.
Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema, Ukristo umeendelea kutangazwa na kushuhudiwa katika maisha na maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa na kwamba, uinjilishaji ni utume uliotekelezwa na Mtakatifu Cyril na ndugu yake Method kwa ari na moyo mkuu. Wakati huu, Kanisa linaadhimisha kumbukumbu ya Miaka 1150 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Cyril na kwamba, mchango wake bado ni endelevu katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho; unaoisaidia familia ya Mungu katika nchi hizi, kujikita katika kutafuta mafao ya wengi, ukweli na uzuri. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 22 Machi 2019 alipokutana na kuzungumza na wawakilishi wa Wabunge kutoka Czech na Slovakia kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1150 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Cyril. Huu ni mwaliko kwa wanasiasa hawa kutambua uhusiano wa ndani uliopo kati ya Injili na tamaduni zao, kwa kuthamini mizizi ya Ukristo inayojenga jamii zao, ili kukuza ukarimu na mshikamano. Mtakatifu Cyril katika maisha na utume wake, alifanikiwa kuwa kweli ni kiungo thabiti kati ya tamaduni na Mapokeo mbali mbali ya Kikanisa.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, amana na urithi huu wa maisha ya kiroho na kitamaduni, utasaidia mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu wa nchi hizi mbili kukutana na hatimaye kuishi kwa pamoja hata katika tofauti zao msingi. Wawe na ujasiri wa kujenga madaraja yanayowakutanisha watu, kwa kubomolea mbali kuta za utengano, maamuzi mbele na hali ya kutoaminiana. Kwa njia hii, wataweza kuwa kweli ni mashuhuda wa mshikamano na wajenzi wa amani. Baba Mtakatifu anawataka wanasiasa katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao ya kila siku, wawe kweli ni wadau wa ujenzi wa udugu, wasimamizi na wawajibikaji wa mafao ya wengi, ili kuwapatia watu waliowachagua matumaini katika maisha, wanapotekeleza majukumu yao ya uongozi wa ngazi ya juu katika jamii! Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 13 Septemba 2021 katika hija yake ya kitume nchini Slovakia, baada ya kukutana na kuwahutubia viongozi wa Serikali, Vyama vya kijamii, Mabalozi na Wawakilishi mbalimbali waliko nchini Slovakia alipata bahati ya kuzungumza na Wakleri, Watawa, Waseminari na Makatekista kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Martin, Jimbo kuu la Bratislava.
Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake alikazia umuhimu wa Kanisa kuambata fadhila ya unyenyekevu katika ulimwengu mamboleo kwa kujikita katika mchakato wa uhuru kamili unaowajibisha na kudumu. Kipaji cha ubunifu katika uinjilishaji na utamadunisho kinahitajika sana! Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni muhimu ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu amewashukuru watu wa Mungu nchini Slovakia kwa matamanio na matumaini waliyo nayo kwa Kanisa nchini mwao kama ilivyokuwa kwa Kanisa la Mwanzo waliokuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali na kutenda yote kwa umoja. Rej. Mdo1:2-14. Kanisa linahitaji kufanya hija ya pamoja ili kuwasha moto wa Injili. Kanisa ni jumuiya ya waamini ambao wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, upendo na amani duniani. Kanisa halina budi kufuata mfano wa Kristo Yesu katika unyenyekevu. “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” I Kor 8:9. Ni katika muktadha huu, Kanisa litakuwa na uwezo wa kufahamu na kushiriki matatizo, changamoto, matumaini na matarajio ya walimwengu. Hii ni changamoto kwa Kanisa kutoka katika hali ya kujitafuta lenyewe na kuanza kuhangaikia matatizo ya watu wa Mungu. Je, watu wa Mungu wanatarajia nini kutoka kwa Mama Kanisa? Baba Mtakatifu anajibu swali hili msingi kwa kusema ni uhuru kwani binadamu katika hulka yake ameumbwa kuwa huru.
Lakini historia ya maisha ya mwanadamu inaonesha kwamba, kumekuwepo na mashambulizi dhidi ya uhuru, utu, heshima na haki msingi za binadamu zikasiginwa, kiasi kwamba, uhuru wenyewe ukatoweka. Uhuru ni mchakato unaopaswa kupyaishwa kila wakati kwa kuwajibika kwa maamuzi yanayotolewa; kwa kufanya mang’amuzi pamoja na udumifu. Hii ndiyo historia ya Waisraeli katika Agano la Kale, walipopewa uhuru, wakakinai na kuanza kukumbuka “masufuria ya nyama na vitunguu swaumu utumwani Misri”. Kanisa linaweza kujikuta katika hali na mazingira haya hususan katika maisha yake ya kiroho na hivyo, waamini kuwa wagumu na kuanza kujifungia katika ubinafsi wao. Hatari hii ni kubwa sana kwa vijana wa kizazi kipya ambayo wanaonekana kutovutwa sana na mambo ya imani, hali inayowakosesha uhuru wa ndani. Mama Kanisa anapaswa kuwahamasisha waamini kukuza na kuimarisha uhuru wao kwa kujenga mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu. Misimamo mikali ya kidini na kiimani haina budi kurekebishwa, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu, chemchemi ya ukombozi wa mwanadamu. Kanisa halina budi kuwa ni alama ya uhuru na ukarimu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Familia ya Mungu nchini Slovakia ina urithi mkubwa katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho wa imani katika uhalisia wa maisha ya watu. Watakatifu Cyril na Method walitangaza na kushuhudia Injili kiasi cha kuanzisha herufi kwa ajili ya kutafsiri Biblia, Liturujia na Mafundisho ya Kanisa na hivyo wakawa ni Mitume wa Utamadunisho wa imani kati ya watu wa Mungu nchini Slovakia!
Huu ndio ubunifu unaotakiwa hata kwa watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo. Kanisa halina budi kutafuta njia na mbinu mpya ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, ili watu waweze kuonja ile furaha ya Injili. Watakatifu Cyril na Method walishtakiwa kwa kosa la ukanimungu kwa sababu waliweza kutafsiri imani yao katika Maandiko! Uinjilishaji maana yake ni mchakato wa utamadunisho, matunda ya upya wa maisha na karama ya Roho Mtakatifu anayepyaisha mambo yote! Kanisa linalowawezesha waamini kuwa na uhuru wa ndani na kuwajibika ni Kanisa ambalo haliwezi kushindwa kujitosa kikamilifu katika historia na tamaduni za watu, kwa kujikita katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, ili kutangaza Injili ya upendo, ushirika na urafiki kati ya watu! Ushirika, muungano na majadiliano katika ukweli na uwazi ni mambo ambayo yanahitaji kuangaliwa kwa jicho la pekee kabisa, ili kuondokana na utamaduni wa kutaka kulipizana kisasi. Hii ni changamoto kwa waamini kusali na kuwaombea huruma na upendo wa Mungu watesi na wale wote wanao wadhulumu! Hivi ndivyo Injili inavyotamadunishwa kwa kujikita katika unyenyekevu na upendo kamili. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewatakia watu wa Mungu nchini Slovakia ujasiri wa kudumu katika safari ya uhuru wa Injili; Ubunifu wa imani na majadiliano yanayobubujika kutoka katika huruma ya Mungu, ili kujenga haki, amani na maridhiano kati ya watu.