Papa Francisko: Iraq Iheshimiwe Na Isiwe Ni Uwanja wa Vita na Vifo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021 alifanya hija ya kitume nchini Iraq kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Baba Mtakatifu amekuwa ni hujaji wa toba, ili kumwomba Mwenyezi Mungu msamaha, tayari kuanza mchakato wa umoja na upatanisho wa Kitaifa. Baba Mtakatifu anasema, alikwenda nchini Iraq kama hujaji wa amani ili kukoleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu. Alipata nafasi ya kukutana mubashara na Kanisa la mashuhuda wa imani, ili kunogesha hija ya matumaini. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 28 Februari 2022 amekutana na kuzungumza na wawakilishi wa Makanisa mbalimbali kutoka nchini Iraq kama sehemu ya kumbukizi la mwaka mmoja wa hija yake ya kitume nchini Iraq. Hii ni nchi ambayo inasimikwa katika ut una uhuru wa watu wake, na kamwe haiwezi kugeuzwa kuwa ni “uwanja wa vita.”
Baba Mtakatifu katika hotuba yake amegusia umuhimu wa Iraq mintarafu Maandiko Matakatifu, changamoto ya wakimbizi na wahamiaji; umuhimu wa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha umoja wa Kitaifa hata katika tofauti zao msingi na watambue kwamba, daima anawakumbuka na kuwaombea katika sala na sadaka yake. Baba Mtakatifu amewakaribisha wawakilishi wa Makanisa mbalimbali kutoka nchini Iraq kwa kuwatakia neema na amani itakayo kwa Mungu Baba Mwenyezi. Amewakumbusha kwamba, Iraq ina umuhimu wa pekee katika historia ya wokovu inayopata chimbuko lake kutoka kwa Ibrahimu, Baba wa imani, mwanzo wa mchakato wa Uinjilishaji ulionogeshwa na Mtume Toma na wengine wote waliofuata baada yake. Ni mahali pa wakimbizi na wahamiaji hata katika nyakati hizi za Karne ya Ishirini na moja. Jumuiya za Wakristo nchini Iraq ni mashuhuda wa uaminifu wa Injili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu amechukua fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kurithisha imani, kiasi hata cha kuthubutu kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake.
Baba Mtakatifu anayapongeza Makanisa kwa kushirikiana na kushikamana katika huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo fungamani kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Iraq, kama kielelezo makini cha udugu wa kibinadamu. Iraq inapaswa kuwa ni mahali pa ujenzi wa haki, amani, upatanisho na maridhiano, kila mtu akipewa nafasi ya kuchangia kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kamwe wasiwepo “raia wa daraja la pili.” Viongozi wa Makanisa wawe ni mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa watu wa Mungu, kwa kuwaonesha ukarimu na ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Makanisa nchini Iraq yajielekeze katika mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali, ili wote kwa pamoja waweze kusimama kidete kulinda: utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kujenga udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika haki, amani na maridhiano; ili wote kwa pamoja waweze kuwa ni madaraja na wajenzi wa amani ndani na nje ya Iraq. Baba Mtakatifu mwishoni mwa hotuba yake, amependa kuwahakikishia kwamba, daima anaendelea kusali na kuwakumbuka katika sadaka yake, ili waweze kulinda na kudumisha ushirika wa Kanisa unaopata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili wote wawe wamoja!
Wakati huo huo, Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo katika hotuba yake ya utangulizi kwa Baba Mtakatifu Francisko, amewatambulisha viongozi wakuu wa Makanisa kutoka Iraq pamoja na wahusika wakuu katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Iraq. Huu ni ujumbe mzito uliofika mjini Vatican ili kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa hija yake ya Kitume nchini Iraq. Ni ujumbe, unaotamani kuendelea kushikamana na kutembea kwa pamoja kama sehemu ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu. Viongozi wakuu wa Makanisa wameridhishwa sana na hija hii ya kiroho, ambayo inaendelea kuwachangamotisha kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Iraq. Haya ni majadiliano yanayosimikwa katika udugu wa kibinadamu, ili wote waweze kudumisha umoja wa Kanisa licha ya tofauti zao msingi. Viongozi hawa wameonesha hamu kubwa ya kuweza kuadhimisha Pasaka ya Bwana kwenye tarehe moja. Ujumbe makini kwa viongozi wote wa Makanisa nchini Iraq ni kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.