Tafuta

Maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu kwa sababu yanahusiana na maisha ya binadamu na viumbe wengine wote. Maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu kwa sababu yanahusiana na maisha ya binadamu na viumbe wengine wote. 

Maji Ni Sehemu Ya Haki Msingi Za Binadamu: Tunzeni Vyanzo Vya Maji

Afya bora, maji safi na salama ni mahitaji msingi ya binadamu, lakini pia yana umuhimu wake kwa viumbe wote wanaoishi duniani. Kumbe, kuna umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na maboresho makubwa yatakayowawezesha walimwengu kufaidika na haki hii msingi katika maisha yao. Tunzeni vyanzo vya maji kwa usalama

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Uhaba wa maji safi na salama unaweza kuwa ni chanzo cha migogoro, kinzani na vita kwa siku za usoni, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa haitasimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza vyanzo vya maji pamoja na kutambua kwamba, maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Kumbe, huduma bora za maji safi na salama ni kichocheo kikuu cha maisha na afya bora zaidi. Dhana ya maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu ni agenda iliyoibuliwa hivi karibuni, lakini inaendelea kushika kasi kubwa sana katika Jumuiya ya Kimataifa kutokana na unyeti wake unaofungamanishwa na maisha ya binadamu. Ndiyo maana kuna haja ya kuwa na miundo mbinu ya kisheria, kiufundi, kijamii na kisiasa ili kuanzisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa utunzaji bora wa vyanzo vya maji. Kwa njia hii, amani duniani inaweza kuimarishwa kwa kuzuia vita, kinzani na migogoro inayoweza kufumbatwa katika mafao ya kisiasa na kiuchumi kwa kubeza: haki msingi, utu, heshima na maisha ya binadamu.

Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu
Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 30 Machi 2022 amesema maji safi na salama ni amana na utajiri mkubwa unaopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa. Baba Mtakatifu ameyasema haya wakati akitoa salam na matashi mema kwa wanachama wa Chama cha Kilimo Cha Umwagiliaji nchini Italia, akiwataka kuhakikisha kwamba, wanatunza maji kama “mboni ya jicho lao.” Maji ni muhimu sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maendeleo fungamani ya binadamu kwa siku za mbeleni yatategemea kwa kiasi kikubwa jinsi ambavyo Jumuiya ya Kimataifa itaweza kuyatunza na kuyatumia maji kwa ajili ya: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Afya bora, maji safi na salama ni mahitaji msingi ya binadamu, lakini pia yana umuhimu wake kwa viumbe wote wanaoishi duniani. Kumbe, kuna umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na maboresho makubwa yatakayowawezesha walimwengu kufaidika na haki hii msingi katika maisha yao.

Jengeni utamaduni wa kutunza vyanzo vya maji.
Jengeni utamaduni wa kutunza vyanzo vya maji.

Huduma ya afya bora, maji safi na salama ni wajibu wa Serikali husika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwani huu ni wajibu wa watu wote, ili kusaidia mchakato wa kijamii na maendeleo fungamani ya binadamu. Kumbe, maji safi na salama hayawezi kugeuzwa kuwa sawa na bidhaa nyingine yoyote kwa sababu ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, uratibu wa maji unaunganishwa na wajibu wa kijamii kwa kuwa na mwelekeo sahihi wa kiikolojia sanjari na ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu miongoni mwa nchi mbalimbali duniani. Kwa njia hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kufanikiwa kuwa na matumizi bora zaidi ya maji safi na salama pamoja na kudumisha utunzaji bora zaidi wa vyanzo vya maji. Baba Mtakatifu Francisko anasema, changamoto mbalimbali zinazomwandamana mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, zinahitaji umoja, ushirikiano na mshikamano, kwa kuendelea kutafuta njia bora na rafiki zitakazomsaidia mwanadamu kukabiliana na changamoto hizi katika uso wa dunia.

Haki Maji
30 March 2022, 14:29