Tafuta

Msalaba wa Kristo Yesu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma, upendo, msamaha na upatanisho wa Mungu na binadamu. Msalaba wa Kristo Yesu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma, upendo, msamaha na upatanisho wa Mungu na binadamu. 

Msalaba Ni Kielelezo Cha Huruma, Upendo Na Msamaha wa Mungu

Msalaba wa Kristo Yesu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma, upendo na msamaha wa kweli. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha ujirani mwema na wale wote wanaoteseka: kiroho na kimwili. Hawa ni wale wanaohisi upweke hasi, wanodhulumiwa na kunyanyasika; wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii bila kuwasahau wale wasiokuwa na ulinzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwaresima ni safari ya maisha ya kiroho inayowawezesha waamini kujiandaa kikamilifu ili kusherehekea Pasaka ya Bwana, huku wakiwa na nyoyo zilizotakaswa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Huu ni mwaliko kwa waamini kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha yao kwa: toba na wongofu wa ndani; kwa kufunga na kusali. Msalaba wa Kristo Yesu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma, upendo na msamaha wa kweli. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha ujirani mwema na wale wote wanaoteseka: kiroho na kimwili. Hawa ni wale wanaohisi upweke hasi, wanodhulumiwa na kunyanyasika; wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii bila kuwasahau wale wasiokuwa na ulinzi. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.” Gal 6:9-10.

Kwaresima ni wakati wa kupyaisha maisha ya kiroho na kiutu
Kwaresima ni wakati wa kupyaisha maisha ya kiroho na kiutu

Kwaresima ni kipindi cha safari ya Siku 40 katika jangwa la maisha ya kiroho, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani tayari kuadhimisha kiini cha Fumbo la Wokovu wa mwanadamu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu yaani Fumbo la Pasaka. Kipindi cha Kwaresima kinasimikwa katika nguzo kuu nne: yaani; Sala, Kufunga, Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2022 anakazia pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa kupanda na kuvuna mema katika familia ya binadamu kwa kuongozwa na Neno la Mungu; Waamini wasichoke katika kutenda mema maana watavuna kwa wakati wake. Wasichoke kusali, kung’oa maovu kutoka katika maisha yao sanjari na kuwatendea mema jirani. Baba Mtakatifu anasema Kwaresima ni kipindi muafaka cha toba na wongofu wa ndani, tayari kujikita katika kutenda mema, kwa kuondokana na tabia ya uchoyo, kiburi na tamaa ya kutaka kujikusanyia na kumiliki vitu.

Ni mwaliko wa kuondokana na tabia ya ulaji wa kupindukia, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani pamoja na kushirikishana mema ya nchi. Ni wakati wa kubadili mtazamo wa maisha kwa kuwekeza katika ukarimu na kushirikishana mema ya nchi, kama Mwenyezi Mungu tangu awali alivyoitendea familia ya binadamu. Hiki ni kipindi cha kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha, ili liweze kuwa ni chemchemi ya furaha pamoja na kuutumia vyema muda huu, ili kupanda mbegu ya wema, kama kielelezo cha neema na ushiriki wa mwanadamu katika wema wa Mwenyezi Mungu. Wale wote wanaojiaminisha kwa Mungu katika upendo watazaa matunda mema. Hakuna hata tendo moja la upendo kwa Mungu litakalopotea, juhudi ya ukarimu isiyokuwa na maana wala uvumilivu unaoumiza unafanyika bure na kwamba, kila mti utatambulikana kwa matunda yake Rej. Evangelii gaudium, 279.

Kwaresima
30 March 2022, 14:53