Jumatano ya Majivu, tarehe 2 Machi 2022, mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima kinachosimikwa katika toba na wongofu wa ndani. Jumatano ya Majivu, tarehe 2 Machi 2022, mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima kinachosimikwa katika toba na wongofu wa ndani. 

Papa Francisko: Jumatano ya Majivu Mwanzo wa Safari ya Imani

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, Jumatano ya Majivu, tarehe 2 Machi 2022, mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima kinachosimikwa katika toba na wongofu wa ndani amekazia kuhusu aina mbili za thawabu; Ibada ya kupakwa majivu, sala inayotoka katika undani wa mtu na kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili na mwishoni ni kufunga na kujinyima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ibada ya Jumatano ya Majivu kwa mwaka 2022 ilianza kwa maandamano ya toba kutoka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anselmo hadi kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Sabina, Jimbo kuu la Roma. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, Jumatano ya Majivu, tarehe 2 Machi 2022, mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima kinachosimikwa katika toba na wongofu wa ndani amekazia kuhusu aina mbili za thawabu, Ibada ya kupakwa majivu, sala inayotoka katika undani wa mtu na kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili na mwishoni ni kufunga. Mahubiri haya yamesomwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu ambaye kutokana na changamoto za kiafya, ameshauriwa na madaktari kupumzika kidogo. Baba Mtakatifu anasema, Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa safari ya imani ya Kipindi cha Siku 40 katika jangwa la maisha ya kiroho, ili hatimaye kuzima kiu na njaa ya kukutana na Kristo Yesu Mfufuka. Baba Mtakatifu amekazia kwa namna ya pekee thawabu inayotolewa na Mwenyezi Mungu kwa sababu hii ina uhakika wa maisha ya uzima wa milele.

Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa hija ya maisha ya kiroho.
Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa hija ya maisha ya kiroho.

Lakini thawabu inayotolewa na wanadamu, ni ya muda tu na inachakaa mapema na kumwacha mwamini mikono mitupu, na matokeo yake ni kumezwa na malimwengu na hivyo kukosa amani ya ndani pamoja na ari na mwamko wa kuragibisha amani ulimwenguni. Kumbe, waamini wanapaswa kuwa makini kamwe wasitende kwa unafiki ili kutazamwa na kupewa thawabu na watu. Ibada ya Kupakwa majivu kwenye paji la uso, ni ukumbusho wa udhaifu na dhambi zinazomwandama mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani. Lengo la maelekeo haya ni ugonjwa wa maisha ya kiroho wa kutaka kutazamwa na watu na matokeo yake, ni kugeuka na kuwa ni mtumwa wa mwonekano wa nje. Hii ndiyo ile tabia ya mtu kutaka kujimwambafai mbele ya wengine na kujikweza na matokeo yake ni masumbuko ya ndani yasiyoweza kupata kitulizo hata kidogo! Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata leo hii, kufunga, kusali na matendo ya huruma: kiroho na kimwili yanaweza kuwa na mwelekeo wa mtu kutaka kujimwambafai mbele ya watu, bila ya kuwa na hata chembe ya upendo kwa Mungu na jirani. Kwake ni kutaka kuonekana na kujipatia ujiko mbele ya watu. Liturujia ya Neno la Mungu, Jumatano ya Majivu ni mwaliko kwa waamini kuchunguza nafsi zao kwa mwanga na tunu za Kiinjili, ili hatimaye, kuvua unafiki unaowasonga na hivyo kukabiliana na ukweli uso kwa uso!

Mwanadamu katika fahari zake zote akumbuke kwamba ni sawa na majivu na atarudi udongoni. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kukuza na njaa na kiu ya maisha ya uzima wa milele, kwa kukutana na Kristo Yesu Mfufuka katika maisha yao. Ili kuweza kutibu magonjwa ya mwonekano wa nje, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujikita katika sala, mapendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na kufunga. Majivu waliyopakwa, yawakumbushe umuhimu wa kuuvua utu wa kale unaosimikwa katika unafiki, tayari kuanza kutembea katika mwanga mpya na nguvu mpya za maisha. Waamini wajifunze kusali kwa unyenyekevu, ile sala inayotoka katika undani wa maisha yao. Wajenge utamaduni wa majadiliano katika imani, ukweli na upendo kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, anaewafariji. Iwe ni fursa ya kusali na kutafakari Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Waamini wajitahidi kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, kielelezo cha upendo wa Mungu.

Mahubiri ya Papa Francisko yamesomwa na Kardinali Pietro Parolin.
Mahubiri ya Papa Francisko yamesomwa na Kardinali Pietro Parolin.

Ikumbukwe kwamba, sala makini ni ile inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Duniani kuna mambo! Si haba kuona watu wanafunga na kujinyima kwa ajili ya kutafuta ulimbwende, ili waonekane na kupendwa. Kuna watu wengi ambao duniani wanafunga kwa takribani mwaka mzima, kwa kupata mlo kiduchu; njaa na mateso kwao kimekuwa ni chakula cha kila siku, kufunga ni sehemu ya maisha yao kutokana na shida wanazokabiliana nazo. Lakini kwa Mkristo, anaalikwa kufunga na kujinyima wakati huu wa kipindi cha Kwaresima, ili kuwasaidia watu wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na baa la njaa na utapiamlo duniani. Wakristo wajifunze kujinyima kwa ajili ya kuwasaidia jirani zao wenye shida na mhangaiko zaidi. Ni kujisadaka kwa kuzingatia haki na kutenda wema. Kufunga maana yake ni kutoa uzito wa haki kwa mambo na vitu katika uhalisia wa maisha. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema: Sala, matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na kufunga ni dawa madhubuti kwa watu wote wa Mungu na kwa hakika ni mambo yanayoweza kugeuza historia ya maisha ya mwanadamu, kwa kumruhusu Mwenyezi Mungu kutenda katika maisha ya waja wake.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amesali na kuombea haki, amani na maridhiano nchini Ukraine. Yaani amani ambayo binadamu kwa nguvu na jeuri yake, hawezi kuipata na kuijenga, bali amani inayotolewa na Mwenyezi Mungu kama zawadi inayomwajibisha binadamu. Amemwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kusikiliza kwa wema sala inayotolewa na waja wake wanaojiaminisha kwake. Hawa ni watu ambao wanateseka kutokana na vita, wanalazimika kuikimbia nchi yao ili kusalimisha maisha yao. Wote, hawa Mwenyezi Mungu awakirimie amani ya ndani pamoja na kuwapatia watu wote amani ya kweli na inayodumu!

Papa Jumatano ya Majivu
03 March 2022, 16:09