Papa Francisko: Vita ina madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jengeni utamaduni wa haki, amani na maridhiano. Papa Francisko: Vita ina madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jengeni utamaduni wa haki, amani na maridhiano. 

Vita Ina Madhara Makubwa! Jengeni Utamaduni Wa Kulinda Amani Duniani

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana tarehe 27 Machi 2022 amesikitika kusema tena kwamba, vita hii ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu wote. Kuna haja ya kushinda kishawishi cha kukimbilia mapambano ya silaha kama njia ya kutatua migogoro ya Jumuiya ya Kimataifa. Kimsingi vita ni uwanja wa vifo na maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tangu Urussi ilipoivamia Ukraine kijeshi kumekuwepo na athari kubwa sana katika medani mbalimbali za maisha ya watu katika Jumuiya ya Kimataifa. Kumekuwepo na athari za kiuchumi, ambako kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta kumepelekea mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma. Tatizo kubwa zaidi kiuchumi ni kwamba sasa nchi nyingi zinalazimika kutumia fedha nyingi zaidi za kigeni kuagiza nishati ya mafuta kuliko kawaida na hili huathiri akiba ya fedha za kigeni ya nchi nyingi na hivyo kupunguza matumizi ya fedha ambazo zingetumika kwenye mambo mengine muhimu. Urussi na Ukraine ni wazalishaji na wasambazaji wakuu wa ngano na mazao mengine ya nafaka duniani. Vita hii imesababisha bei ya chakula kuongezeka maradufu. Vita inaendelea kutishia kuporomoka kwa ukuaji wa uchumi duniani. Mabilioni ya rasilimali fedha iliyokuwa inatumika katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga, maradhi na athari za mabadiliko ya nchi kwa sasa yanaelekezwa katika mapambano ya kivita huko nchini Ukraine. Hali hii imepelekea kushuka kwa kiwango cha ubora wa huduma katika sekta ya elimu, afya, mapambano dhidi ya umaskini, ustawi na maendeleo ya jamii.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinabainisha kwamba, hadi kufikia tarehe 26 Machi 2022 idadi ya wakimbizi wa kivita kutoka Ukraine imeongezeka hadi kufikia wakimbizi 3, 821, 049. Wengi wao wanapewa hifadhi nchini Hungaria, Poland, Slovakia na Italia. Zaidi ya watu 50, 000 wamehama kutoka Majimbo ya Donetsk na Luhansik kwenda Urussi kati ya tarehe 21 hadi tarehe 23 Februari 2022. Kumbe ni wajibu wa kimaadili na kiutu ili kuwasha moto wa: haki amani; Upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kurejea tena kwa ari na nguvu mpya katika majadiliano yanayofumbata ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 27 Machi 2022 amesikitika kusema tena kwamba, vita hii ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu wote. Kuna haja ya kushinda kishawishi cha kukimbilia mapambano ya silaha kama njia ya kutatua migogoro ya Jumuiya ya Kimataifa. Kimsingi vita ni uwanja wa vifo na maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Idadi ya wakimbizi kutoka Ukraine inazidi kuongezeka maradufu
Idadi ya wakimbizi kutoka Ukraine inazidi kuongezeka maradufu

Inasikitisha kuona ndugu wamoja wanapigana na kuuwana bila hata pengine kupatana nafasi ya kuonana uso kwa uso. Haya ni maamuzi ya “Vigogo” wa Kimataifa yanayopelekea maskini kuendelea kupoteza maisha, wakati “Vigogo” wakiponda maisha na askari walioko mstari wa mbele wakiendelea “kupukutika kama nyasi kavu.” Kuna watoto ambao kwa sasa wamebaki yatima kwa sababu wazazi wao wamefariki dunia. Kuna watoto ambao wamelazimika kuikimbia nchi yao na sasa wanaishi kama wakimbizi wasiokuwa na wazazi wao. Ndoto ya maisha ya watoto wao kwa sasa na kwa siku za usoni “imeingia mchanga.” Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni unyama, ukatili na kufuru ya kivita. Jumuiya ya Kimataifa isizoee kamwe mapambano ya silaha kwani vita ina madhara makubwa kwa binadamu. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuongoka na kuanza kujibidiisha kujenga utamaduni wa amani kwa sasa na kwa siku za usoni. Vita hii inawahusisha watu wote na kwamba, madhara makubwa ya vita yanayoendelea kujitokeza kwa sasa, ni kielelezo kwanza, umefika wakati wa kufuta vita kutoka katika historia ya mwanadamu, kabla ya vita yenyewe haijamfyekelea mbali mwanadamu na kumfuta kutoka katika historia ya dunia.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwakumbuka na kuwaombea wanasiasa, huku akiwasihi kutafakari kuhusu madhara ya vita na umuhimu wa kuanza kujielekeza katika ujenzi wa haki, amani, maridhiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kwa kuangalia hali halisi ya vita nchini Ukraine, inaonekana wazi kwamba, kila kukicha hali inaendelea kuwa mbaya kwa nchi zote mbili. Ni katika hali na mazingira kama haya, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa tena mwaliko kwake kwa nchi zote mbili: Kusikitisha vita, kunyamazisha silaha za vita na kuanza kujielekeza katika mchakato wa amani. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusali bila kuchoka wala kukata tamaa kwa ajili ya amani duniani. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru Maaskofu, Mapadre, Watawa, Waamini na watu wote walioungana pamoja naye tarehe 25 Mei 2022 kwa ajili ya kuziweka wakfu Urussi na Ukraine kwa maombezi ya Moyo Mtakatifu wa Bikira Maria.

Madhara ya Vita

 

28 March 2022, 15:15