Watawa Zingatieni: Umoja, Ushiriki na Utume Wenu Katika Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirika la Masista wa Mtakatifu Dorotea wa Frassineti hivi karibuni limeadhimisha Mkutano Mkuu XXII wa Shirika na kuwachagua viongozi wapya. Ijumaa tarehe 18 Machi 2022 wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Mkutano mkuu ni fursa ya kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa katika uhalisia wake. Ni muda muafaka wa kujenga ushirika na udugu wa kibinadamu; dhana ya kusikilizana na kujadiliana katika ukweli na uwazi, ili kufanya mang’amuzi na hatimaye kwa msaada na mwanga wa Roho Mtakatifu kutekeleza maamuzi yaliyofikiwa. Katika maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Shirika wamejadili jinsi kufuata njia nyingine inayowaelekeza katika mshangao, moyo wa shukrani, toba na wongofu wa ndani kwa kushindwa kuamini kwa haraka, lakini tayari kupokea neema na baraka kutoka kwa Kristo Mfufuka. Njia nyingine inawaondoa kutoka katika hofu na mashaka ya giza; kwa kushindwa kuwa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi kama ilivyokuwa kwa wale Mamajusi kutoka Mashariki. Rej. Mt 2: 1-12. Njia nyingine inawawezesha kama watawa kujenga na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi ili kunogesha udugu wa kibinadamu katika maisha ya kitawa.
Kimsingi anasema Baba Mtakatifu Francisko, Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume yana amana na urithi mkubwa wa kitamaduni kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Wanashirika tangu mwanzo wanajifunza kutembea kwa pamoja kama ndugu wamoja, huku wakiwa wanaongozwa na Kristo Yesu katika mwanga wa Roho Mtakatifu. Huu ni mwaliko kwa watawa kuhakikisha kwamba, daima wanajichotea utajiri huu, ili waongozwe na Roho Mtakatifu katika upendo, vinginevyo, uchoyo na ubinafsi vitawakepenyua na kuwaangusha. Baba Mtakatifu anawataka watawa kuondokana na tabia ya umbea na kusengenyana, mambo ambayo ni hatari sana kwa maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia ya Kristo Yesu, wajenge na kuimarisha umoja, ushiriki na utume wa Kanisa mambo msingi katika maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayoendelea kwa wakati huu.
Sinodi ya XVI ya Maaskofu inanogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Maadhimisho haya yamegawanyika katika awamu kuu tatu. Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine amekazia kuhusu: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa. Ni kutokana na upendo usiokuwa na mipaka uliokuwa unabubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Mtakatifu Paola Frassineti alijisadaka bila ya kujibakiza kujenga na kudumisha umoja kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu kwenye Mtaguso wa kwanza wa Yerusalemu. Mitume walijipambanua na kujitofautisha na makundi mengine ya kijamii kutokana na ushuhuda wa umoja wao. Mtakatifu Paola Frassinetti alijibidiisha kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini sauti za wafunga magerezani. Ingawa hakuwa ni msomi, lakini alianzisha Shirika la Kitawa ambalo limejielekeza zaidi katika sekta ya elimu, kwa kuwashirikisha watu wengi zaidi katika maisha na utume wa Kanisa. Haya ni matunda ya kazi ya Roho Mtakatifu aliyewawezesha kuvuka mipaka hadi kuwaendelea watu wenye kiu ya elimu sehemu mbalimbali za dunia. Huu ni usuhuda unaosimikwa katika ushiriki wa kielimu na kijumuiya kwa ajili ya kuinjilisha kwa kuelimisha na kuelimisha kwa ajili ya kuinjilisha. Haya ni mang’amuzi ya elimu yanayopata chimbuko lake kutoka katika ndani ya familia, shule na katika parokia.
Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” ni mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko, ili kujenga mfumo wa elimu unaojikita katika msingi wa elimu fungamanishi. Lengo ni kuwasaidia vijana kujizatiti zaidi katika elimu fungamanishi inayowataka vijana wa kizazi kipya kuwa wasikivu, wajenzi wa haki, amani, umoja na udugu wa kibinadamu katika usawa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, elimu maana yake ni mchakato unaowajengea wanafunzi matumaini ya kuondokana na ubinafsi wao; kwa kutambua, kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza, ili hatimaye kujenga na kudumisha: utamaduni wa ukarimu, mshikamano, mafungamano na hofu ya Mungu. Upyaisho wa mfumo wa elimu katika ulimwengu mamboleo utawasaidia watu wa Mungu kupambana na changamoto zinazojitokeza kwa wakati huu, ili kujenga leo na kesho yenye matumaini. Elimu ni upendo unaowajibisha na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, ili kuondokana na ubinafsi unaopelekea watu kutokuthaminiana. Kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano unaosimikwa katika kipaji cha kusikiliza, kujadiliana na maelewano. Mabadiliko ya mfumo wa elimu duniani yanapaswa kuwahusisha wadau mbali mbali katika sekta ya elimu, ili kuondokana na ukosefu wa haki jamii; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili hatimaye, kuweza kupambana na umaskini pamoja na tabia ya watu kutowajali wengine. Katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Baba Mtakatifu anawahamasisha Watawa wa Shirika la Mtakatifu Dorotea wa Frassineti kujikita zaidi katika njia upendo unaobubujika kutoka nyoyoni mwao, ili watu waweze kuwajibika zaidi katika hatma ya maisha yao.