Papa:vita kikatili viishe na kuwapo mchakato wa mazungumzo

Mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana,Papa ametoa wito kwa upya Ukraine ili wahakikishiwe msaada hasa wahudumu wa kibinadamu.Anashukuru wote ambao wamekubali kukaribisha wakimbizi na waandishi wa habari wanaosimulia kile kinachotokea cha ukatili wa mgogoro.Amezindua kwa upya matendo ya kidiplomasia ya Vatican na mchakato wa amani.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Papa Francisko amerejea kwenye mkasa wa vita nchini Ukraine na kutangaza kwa upya ombi lake la Amani. Ameonesha hayo kwa waamini na mahujaji waliofika katika uwanja wa Mtakatifu Petro kusali Sala ya malaika wa Bwana, Dominika tarehe 6 Machi 2022. Wazo la Papa mara moja limeenda kwenye majeraha ambayo yanawatesa watu wa Ukraine na kusema kwamba mito ya damu na machozi inatiririka nchini Ukraine.

 Vita wala sio operesheni ya wanajeshi

Sio tu operesheni ya kijeshi, lakini ni vita, ambayo inapanda kifo, uharibifu na taabu, Papa amesisitiza. Waathirika wanazidi kuwa wengi, sawa na watu wanaokimbia, hasa akina mama na watoto. Katika nchi hiyo inayoteswa hitaji la usaidizi wa kibinadamu linazidi kuongezeka kwa kasi kwa saa. Kwa maana hiyo, ulinzi lazima uhakikishwe mara moja kwa idadi ya raia, hii inathibitisha kwa nguvu: “Ninatoa ombi langu la dhati kwa njia za kibinadamu kulindwa kweli, na upatikanaji wa misaada katika maeneo yaliyozingirwa uhakikishwe na kuwezeshwa, ili kutoa msaada muhimu kwa kaka na dada zetu wanaokandamizwa na mabomu na woga.

Majadiliano yanatawala

Papa ametoa shukrani zake kwa walio wengi ambao wamehusika katika kuwakaribisha na anaomba kuanzishwa kwa upya kwa mchakato wa mazungumzo: “Ninawashukuru wale wote wanaowakaribisha wakimbizi. Zaidi ya yote, ninasihi kwamba mashambulizi ya silaha yakome na mazungumzo yatawale na busara pia itawale na kurudi kuheshimu sheria za kimataifa!

Papa atoa shukrani kwa waandishi wa habari

Wazo maalum pia limewaendea waandishi wa habari ambao, kwa kazi yao, wanaendelea kutoa habari ulimwengu wote ukweli wa kutisha wa vita: “Na pia ningependa kuwashukuru waandishi wa habari ambao wameweka maisha yao hatarini ili kuhakikisha kunawezekana kupata habari: asante, kaka na dada, kwa huduma yenu! Huduma ambayo inaturuhusu kuwa karibu na mchezo mbaya wa watu hao na wanaturuhusu kutathimini ukatili wa vita. Asante, kaka na dada. Na tuombe pamoja kwa ajili ya Ukraine: tunaona bendera zake mbele yetu. Tusali pamoja, kama ndugu, kwa Mama Yetu Malkia wa Ukraine”, Papa ameomba.

Vatican kutuma wawakilishi Ukraine

Vatican iko tayari kufanya kila kitu, kujiweka katika huduma ya amani hiyo. Katika siku hizi, makadinali wawili wamekwenda Ukraine kuhudumimia watu,  na kusaidia. Hao ni Kardinali Krajewski, Mkuu wa mfuko wa Kitume wa Papa kupelekea  msaada kwa wahitaji, na Kardinali Czerny, Mwenyekiti wa muda wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu. Uwepo huu wa makadinali wawili huko ni uwepo sio tu wa Papa, lakini wa watu wote wa Kikristo wanaotaka kukaribia na kusema: “Vita ni wazimu! Acha, tafadhali! Angalia ukatili huu! ”

WITO WA PAPA KUSITISHA VITA HUKO UKRAINE
06 March 2022, 14:53