Papa Francisko anawaalika Maaskofu, Mapadre na Waamini wote katika ujumla wao, kuungana pamoja naye tarehe 25 Machi 2022 kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani. Papa Francisko anawaalika Maaskofu, Mapadre na Waamini wote katika ujumla wao, kuungana pamoja naye tarehe 25 Machi 2022 kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani. 

Urussi na Ukraine Kuwekwa Wakfu Kwa Moyo Safi Wa B. Maria: Mwaliko Kwa Wote

Papa anawaalika Maaskofu mahalia, mapadre pamoja na waamini wote katika ujumla wao, kuungana naye katika Siku hii maalum kwa ajili ya kuziwekwa Urussi na Ukraine wakfu kwa maombezi ya Moyo Mtakatifu wa Maria. Inashauriwa na kuhimizwa pale ambapo inawezekana, Maaskofu na mapadre, waungane na Papa kama kielelezo cha ushirika katika imani, karama na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 25 Machi 2022 majira ya Saa 11: 00 Jioni kwa Saa za Ulaya, Kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ataadhimisha Ibada ya Toba na Maondoleo ya Dhambi sanjari na kuiweka Urussi na Ukraine wakfu kwa maombezi ya Moyo Safi wa Bikira Maria. Siku hiyo hiyo Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka Mkuu wa Kipapa, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ataadhimisha Ibada kama hiyo kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, nchini Ureno. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu mahalia, mapadre pamoja na waamini wote katika ujumla wao, kuungana naye katika Siku hii maalum kwa ajili ya kuziwekwa Urussi na Ukraine wakfu kwa maombezi ya Moyo Mtakatifu wa Maria. Inashauriwa na kuhimizwa pale ambapo inawezekana, Maaskofu na mapadre, waungane na Baba Mtakatifu kwa Ibada hii ambayo itaadhimishwa Saa 11: 00 za Jioni kwa Saa za Ulaya sawa na Saa 1: 00 Jioni kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati, kama kielelezo cha ushirika katika imani, karama na mapendo.

Papa Anawaalika Maaskofu, Mapadre na waamini kusali ili kuombea amani duniani.
Papa Anawaalika Maaskofu, Mapadre na waamini kusali ili kuombea amani duniani.

Mababa wa Kanisa wanasema, hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala afaye kwa nafsi yake. Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho; na kiungo kimoja kikitukuzwa viungo vyote hufurahi pamoja nacho. Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo na kiungo kila mmoja peke yake. Upendo hautafuti mambo yake. Lililo dogo kati ya matendo yenu, ambalo limefanywa katika upendo, huleta faida kwa wote katika mshikamano na upendo wa udugu wa kibinadamu.  Rej. KKK 946 – 959. Ushirika huu unaweza kudhihirishwa katika Ibada ya Misa Takatifu na Ibada ya Kuabudu Sakramenti Kuu na ndani mwake, Sala ya kuiweka Urussi na Ukraine wakfu kwa maombezi ya Moyo Safi wa Bikira Maria yatatolewa. Pale ambapo itashindikana kutokana na sababu za kichungaji, basi Ibada hii inaweza kufanyika kwenye Ibada ya Misa Takatifu katika saa mbalimbali. Dhamana ya utekelezaji wa mwaliko huu kutoka kwa Baba Mtakatifu inawaangukia Maaskofu mahalia pamoja na Maparoko katika Parokia zao, Vituo vya hija na Madhabahu.

Itakumbukwa kwamba, tarehe 25 Machi ya kila mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria Kupashwa Habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mkombozi. Wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, yaani: Francis, Yacinta na Lucia. Mtakatifu Paulo VI alikwenda kuhiji mjini Fatima nchini Ureno. Lakini, Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa na uhusiano na ibada ya pekee kabisa kwa Bikira Maria wa Fatima katika maisha na utume wake, kiasi cha kujikabidhi kwa huyu Mama. Kwa namna ya pekee kabisa, waamini wanaalikwa kudumisha Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili; ili kujiachilia wazi mbele ya Mwenyezi Mungu, tayari kujazwa na upendo wake usiokuwa na kifani.

Ushirika katika imani, karama na mapendo
Ushirika katika imani, karama na mapendo

Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa tangu awali sana. Hii ni Ibada inayobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa. Watakatifu na waungama imani, wakaiendeleza Ibada hii kwa ari na moyo mkuu zaidi, kiasi hata Mababa wa Kanisa kuivalia njuga na kuitangaza kwa ajili ya Kanisa zima. Tarehe 13 Julai 1917, Bikira Maria aliwatokea Watoto wa Fatima, wakati walimwengu walipokuwa wanateseka kutokana na madhara ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Bikira Maria akawapatia ujumbe wa matumaini uliokuwa unafumbatwa kwa namna ya pekee katika: toba, wongofu wa ndani pamoja na sala na kwamba, Mwenyezi Mungu daima anatembea katika historia ya maisha ya waja wake, mwaliko kwa waamini ni kumtumainia Kristo Yesu kwani yeye ameushinda ulimwengu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Kumbe, kuna uhusiano wa pekee kabisa katika Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Maria kama chemchemi ya toba, wongofu wa ndani, upendo kwa Mungu na jirani na amani duniani.

Moyo Safi Maria
21 March 2022, 15:19