Watakatifu wapya kutangazwa rasmi tarehe 15 Mei 2022 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Watakatifu wapya kutangazwa rasmi tarehe 15 Mei 2022 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. 

Watakatifu Wapya 11 Kutangazwa Rasmi tarehe 15 Mei 2022: Imani

Hawa ni: Mwenyeheri Titus Brandsma, Maria Rivier na Maria wa Yesu. Wengine Mwenyeheri Lazzaro aliyejulikana kama Devasahayam, Cèsar de Bus, Luigi Maria Palazzolo, Giustino Maria Russolillo, Charles de Foucauld, Maria Francesca di Gesù pamoja Maria Domenica Mantovani. Hawa walipitishwa kwenye Mkutano wa Makardinali uliofanyika tarehe 10 Novemba 2021.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) anasema, watakatifu ni watu wanaotia shime pamoja na kuwasindikiza waamini wenzao kama vyombo na mashuhuda wa imani na matumaini kama ilivyokuwa katika Agano la Kale. Hata leo hii hawa ni watu wanaoweza kuwa ni ndugu, jamaa na marafiki; watu wanaosadaka maisha yao, mashuhuda wa upendo wa Kristo na wale wanaoendelea kujitosa kwa ajili ya umoja wa Kanisa. Hawa ni majirani wanaotangaza na kushuhudia utakatifu wa maisha katika uhalisia wa maisha ya kila siku pasi na makuu.

Watakatifu wapya 11 wanatangazwa tarehe 15 Mei 2022
Watakatifu wapya 11 wanatangazwa tarehe 15 Mei 2022

Watakatifu ni watu wanaoshuhudia unyenyekevu katika maisha, kiasi hata cha kuacha alama za mvuto na mashiko katika uekumene wa damu kama unavyofafanuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Wakristo wote wanahamasishwa kuwa watakatifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mtakatifu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata wewe unaitwa kuwa mtakatifu katika maisha yako kama mtu wa ndoa, maisha ya kuwekwa wakfu, mfanyakazi na mhudumu wa upendo kwa jirani zako! Neema ya utakaso inaweza kuwasaidia waamini kuambata njia ya utakatifu, kwa kukumbatia matunda ya Roho Mtakatifu. Waamini kwa njia ya maisha na ushuhuda wao, wasaidie kuyatakatifuza malimwengu kama vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu: kiroho na kimwili.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 4 Machi 2022 ameongoza Mkutano wa Makardinali ili kupitisha majina ya wenyeheri wanaotarajiwa kutangazwa kuwa watakatifu tarehe 15 Mei 2022. Hawa ni: Mwenyeheri Titus Brandsma, Maria Rivier na Maria wa Yesu. Siku hiyo pia, Mama Kanisa atawatangaza wenyeheri wafuatao kuwa watakatifu: Mwenyeheri Lazzaro aliyejulikana kama Devasahayam, Cèsar de Bus, Luigi Maria Palazzolo, Giustino Maria Russolillo, Charles de Foucauld, Maria Francesca di Gesù pamoja Maria Domenica Mantovani. Hawa ni Wenyeheri waliopitishwa kwenye Mkutano wa Makardinali uliofanyika tarehe 10 Novemba 2021.

Watakatifu 2022
05 March 2022, 16:32