Tafuta

Hija ya Kitume ya 36 ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa nchini Malta kuanzia tarehe 2-3 Aprili 2022 . Hija ya Kitume ya 36 ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa nchini Malta kuanzia tarehe 2-3 Aprili 2022 . 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Malta: Injili ya Amani Na Upendo

Hija hii ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Malta kuanzia tarehe 2-3 Aprili inafumbatwa katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma, upendo na ukarimu kama sehemu ya ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu! Mkazo ni: haki, amani na mshikamano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya 36 ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa nchini Malta kuanzia tarehe 2-3 Aprili 2022 inanogeshwa na kauli mbiu “Wenyeji wakatufanyia fadhili zisizokuwa za kawaida.” Mdo 28: 2. Huu ni ushuhuda wa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa baada ya kunusurika katika dhoruba kali na hatimaye kuwasili salama salimini Kisiwani Melita. Hija hii ya kitume inafumbatwa katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma, upendo na ukarimu kama sehemu ya ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikuwa na kuendeshwa na Vatican anasema, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Malta inapania pamoja na mambo mengine kutangaza na kushuhudia Injili ya amani na ukarimu; kwa kuendelea kusoma alama za nyakati ili kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya: haki, amani na maridhiano, pamoja na kuhakikisha kwamba, vita kati ya Urussi na Ukraine vinakoma, ili watu wa Mungu waweze kurejea katika maisha yao ya kawaida.

Pango ya Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa.
Pango ya Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa.

Katika kipindi hiki cha vita, watu wameonesha mshikamano wa udugu wa upendo kwa wakimbizi wa vita kutoka Ukraine, ingawa kuna baadhi ya watu wamelalamika kwamba, kumekuwepo na “ndago za ubaguzi” kwa baadhi ya wakimbizi, hususan kutoka Barani Afrika. Kardinali Parolin anasema, kuna haja ya kuendelea kujikita katika uwajibikaji pamoja na ukarimu sio tu kwa wakimbizi wa kivita kutoka Ukraine ambao kwa sasa wanaendelea kupewa kipaumbele cha pekee! Hii ni changamoto ya kuokoa maisha ya watu wanaofariki dunia kila siku kwenye Bahari ya Mediterrania huku wakitafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi Barani Ulaya. Ili kuokoa maisha, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujielekeza zaidi katika utekeleza wa sera na mikakati ya utawala bora unaosimikwa katika sheria, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni mwaliko wa kuwekeza katika shughuli za kiuchumi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni wajibu wa serikali husika kwa kusaidiana na wadau mbalimbali wa maendeleo fungamani ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anatekeleza hija hii ya kitume kama sehemu ya mapambazuko ya miaka kumi ya uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anapenda kufuata nyayo za Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa kwa kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa kutambua kwamba, Wakristo wote wanaitwa na kutumwa kuwa ni Wamisionari mitume ili kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya watu. Hii ni changamoto kwa waamini kujikita katika wongofu wa kimisionari, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo! Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea nchini Malta kunako mwaka 1990 na Mwaka 2001. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alifanya hija ya kitume nchini Malta kunako mwaka 2010. Hiki ni kisiwa chenye kumbukumbu hai katika maisha na utume wa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa kama ilivyoandikwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume na Baba Mtakatifu Francisko anakuwa ni Papa wa tatu kutembelea Malta.

Hii ni nchi ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Inajipambanua kwa huduma, ustawi na maendeleo kwa watu wote wa Mungu kama chemchemi ya Injili ya upendo na mshikamano. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kuendelea kujikita katika wongofu wa kimisionari, daima wakijitahidi kuwa ni wamisionari mitume wanaohamasishwa kuendeleza majadiliano ya kitamaduni, kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Takwimu zinaonesha kwamba, walau asilimia 85% ya wananchi wote wa Malta ni Wakristo. Baba Mtakatifu anatembelea nchini Malta ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo, ili waendelee kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa.

Papa Malta 2022

 

01 April 2022, 14:46