Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 28 Aprili 2022 alipokutana na kuzungumza na mahujaji kutoka Jimbo kuu la Łódź, nchini Poland. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 28 Aprili 2022 alipokutana na kuzungumza na mahujaji kutoka Jimbo kuu la Łódź, nchini Poland.  

Jubilei ya Miaka 100 ya Jimbo Kuu la Lodz Poland: Ushuhuda wa Huruma na Ujasiri wa Kiekumene

Ni kielelezo cha majadiliano ya kiekumene; fursa kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Łódź, kushukuru kwa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Jimbo kuu la Łódź, changamoto ni kuendelea kujikita katika mchakato wa majiundo ya Kikristo ili waweze kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, kwa kuunganisha ujasiri wa huruma na ujasiri wa kiekumene.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mahujaji kutoka Jimbo Kuu la Łódź, Poland wanafanya hija ya kiroho mjini Roma kama kielelezo cha imani baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Jimbo iliyowawezesha kupitia nyaraka mbalimbali za Kanisa kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Ni kielelezo cha majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika utume na maisha ya sala. Hii ni fursa kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Łódź, kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Jimbo kuu la Łódź, changamoto ni kuendelea kujikita katika mchakato wa majiundo katika tunu msingi za maisha ya Kikristo ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, kwa kuunganisha ujasiri wa huruma ya Mungu sanjari na ujasiri wa kiekumene. Huu ni wito wa kupyaisha na kuimarisha mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni muhtasari wa mawazo makuu yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 28 Aprili 2022 alipokutana na kuzungumza na mahujaji kutoka Jimbo kuu la Łódź, nchini Poland. Mtakatifu Petro, Mtume katika maisha na utume wake, alionesha upendo wa hali ya juu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kama ushuhuda wa mapambano ya imani. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inakazia ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; umuhimu wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama kielelezo makini cha imani tendaji!

Papa Francisko amewapongeza watu wa Mungu Jimbo kuu la Lodz Poland kwa utume wao
Papa Francisko amewapongeza watu wa Mungu Jimbo kuu la Lodz Poland kwa utume wao

Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inazingatia mambo yafuatayo: Ufahamu wa kina wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo. Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yanayoongozwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” kwa sasa yanafikia tamati kwa awamu yake ya kwanza. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini wanaendelea kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya kwa kuonja uzuri wa ushirika wa Kanisa; ushuhuda wa imani ya pamoja inayowasukuma kuwajibika barabara, ili hatimaye, kuwashirikisha watu wengine wa Mungu uzoefu na mang’amuzi yao ya imani hata wale wanaofikiri na kutenda tofauti na wao. Baba Mtakatifu amewapongeza waamini wa Jimbo kuu la Łódź kwa kuendelea kujikita katika majadiliano ya kiekumene, kielelezo cha ushirika katika tofauti na alama makini ya dhana ya Sinodi katika uhalisia wa maisha. Amewapongeza kwa kuhitimisha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Jimbo hili na kwamba, majadiliano ya kiekumene na dhana ya huruma ya Mungu ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wao.

Papa Francisko amekazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Makanisa mahalia
Papa Francisko amekazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Makanisa mahalia

Huu ni urithi na amana hata kwa vizazi vijavyo. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, maskini, wazee na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wao kwa hakika, ni kielelezo cha Msamaria mwema. Jimbo kuu la Łódź, nchini Poland limekuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa kuunganisha ujasiri wa huruma ya Mungu na ujasiri wa kiekumene kwa kutambua kwamba, majadiliano ya kiekumene ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Ni mwaliko wa kutembea pamoja katika majadiliano ya kitaalimungu na uinjilishaji; Sala na tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa kwenye ushuhuda wa udugu wa kibinadamu, ili kujenga jumuiya mahalia kwa ari na moyo mkuu. Maadhimisho ya Jubilei ni wakati muafaka wa kuwapatia pongezi, wa kuendelea kujipyaisha na kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni fursa ya kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya kidugu kati ya Makanisa tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Mahujaji Poland
28 April 2022, 15:51