Maadhimisho ya Juma Kuu: Kufunika Msalaba na Sanamu: Maana Yake
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Dominika ya Matawi, Waamini wanamshangilia Kristo Yesu anapoingia mjini Yerusalemu kama Mfalme na Masiha, huku watoto wa Wayahudi wakitandaza nguo zao njiani na kuimba “Hosana, mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana” Mt 21:9. Dominika ya Matawi ni mwanzo wa Juma kuu, ambamo Mama Kanisa anaadhimisha Mafumbo makuu ya Kanisa yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, kiini cha imani, matumaini na mapendo ya Kanisa. Kristo Yesu kwa njia ya utii wake anatimiza sadaka yake Msalabani, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumstahilisha tena kuitwa mwana mpendwa wa Mungu. Maandalizi ya Juma Kuu yanatanguliwa kwa kiasi kikubwa na maadhimisho ya Dominika ya V ya Kipindi cha Kwaresima, Mama Kanisa anapoanza kuwaalika Watoto wake kujiweka tayari kuadhimisha Mafumbo makuu ya Wokovu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu uletao wokovu.
Mama Kanisa anayo desturi kwamba, kila mwaka katika maadhimisho ya Dominika ya V ya Kipindi cha Kwaresima, Msalaba na Sanamu mbalimbali zilizoko ndani ya Kanisa zinafunikwa kwa kitambaa. Msalaba utafunuliwa baada ya maadhimisho ya Ijumaa kuu, baada ya kuimba utukufu na ukuu wa Fumbo la Msalaba. Badala ya kashfa na utupu, Msalaba unakua ni chombo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Ni ishara ya mapendo, neema, sala, msamaha, upatanisho na matumaini. Ni kutokana na maana hii mpya, Mama Kanisa anaona fahari kuu kuutangaza utukufu na kuimba sifa kuu za Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Msalaba wa Kristo Yesu, unaendelea kumfunza mwamini kwamba, hakuna mapendo kamili yasiyokuwa na mateso na matumaini ya uzima wa milele. Changamoto kwa waamini katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ni kuuangalia, kuutafakari, kuushangaaa, kuusikiliza, kuuheshimu, kuutukuza na kuuabudu kwa imani, matumaini na mapendo, kwani ni kielelezo ambacho wokovu wa dunia umetundikwa juu yake!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu aliwaandaa Mitume wake kikamilifu kwa ajili ya kulipokea Fumbo la Msalaba, kwa kujionesha kuwa ni Mfalme na Masiha ambaye alikuwa ni Mtumishi mnyenyekevu na asiye na nguvu kinyume cha matarajio yao ya kuwa na Masiha: mtawala na mwenye nguvu; mtu wa kawaida asiyekuwa na utajiri ambao kimsingi ilikuwa ni alama ya baraka ya Mungu, bali mtu wa kawaida asiyekuwa hata na mahali pa kulaza kichwa chake; Mseja asiyekuwa na nyumba wala kiota; ufunuo wa Mungu uliowaacha watu wengi wakiwa wamepigwa na bumbuwazi na hasa zaidi kwa kashfa ya Msalaba. Ni kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Yesu ataweza kufikia kilele cha ufunuo wa: ukuu, utukufu na utakatifu wake ambao utadumu milele yote kwa njia ya Fumbo la Ufufuko wake. Yesu kwa kung’ara uso wake pale juu mlimani Tabor aliwafunulia wafuasi wake utukufu wake unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba, ili kuwaonesha Njia ya Msalaba inayowapeleka kwenye utukufu wake. Anayekufa na Kristo, huyo atafufuka pia pamoja na Kristo; anayeshikamana na Kristo katika mapambano, huyo atashinda pamoja na Kristo.
Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu yaani: Mateso, kifo na ufufuko wake ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake, changamoto kwa Wakristo ni kushikamana pamoja na Kristo Yesu katika mapambano ya maisha ya kila siku, ili siku moja waweze kushinda pamoja naye! Huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba, mwaliko kwa waamini kumtafakari Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ni msingi na kiini cha imani ya Kikristo. Kumbe Msalaba utafunuliwa wakati wa kutukuza Fumbo kuu la Msalaba. Lakini sanamu zitafunuliwa kabla ya Mkesha wa Dominika ya Pasaka, Mama wa Mikesha Yote. Misalaba na Sanamu zinafunikwa ili kuwaangalisha waamini kwamba, Mama Kanisa anajiandaa kuingia katika maadhimisho ya Juma kuu, kipindi cha kutafakari mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Ni mwaliko wa kujiandaa kushiriki kikamilifu na Kristo Yesu katika ile saa yake. Yn 11: 54.
“Basi mtu mmoja alikuwa hawezi, Lazaro wa Bethania, mwenyeji wa mji wa Mariamu na Martha, dada yake. Ndiye Mariamu yule aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake, ambaye Lazaro nduguye alikuwa hawezi. Basi wale maumbu wakatuma ujumbe kwake wakisema, Bwana, yeye umpendaye hawezi. Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo.” Yn 11:1-4. Hili ni tukio ambalo liliwafanya Wayahudi wengi kumwamini kiasi cha kuchochea chuki na uhasama kati ya Kristo Yesu na Wakuu wa Makuhani na Mafarisayo na hivyo wakaazimia kumkamata na hatimaye kumsulubisha Msalabani. Rej. Yn 11: 45-57. Matukio yote haya yanawasaidia waamini kujiandaa kuadhimisha ile “Saa ya Kristo Yesu.” Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kwaresima ni safari ya maisha ya kiroho inayowawezesha waamini kujiandaa kikamilifu ili kusherehekea Pasaka ya Bwana, huku wakiwa na nyoyo zilizotakaswa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Huu ni mwaliko kwa waamini kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha yao kwa: toba na wongofu wa ndani; kwa kufunga na kusali.
Msalaba wa Kristo Yesu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma, upendo na msamaha wa kweli. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha ujirani mwema na wale wote wanaoteseka: kiroho na kimwili. Hawa ni wale wanaohisi upweke hasi, wanodhulumiwa na kunyanyasika; wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii bila kuwasahau wale wasiokuwa na ulinzi. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.” Gal 6:9-10. Umefika wakati kwa waamini kujitahidi kujenga na kukuza utamaduni wa kufunika Msalaba na Sanamu katika familia zao, kama kielelezo cha maandalizi ya maadhimisho ya Mafumbo makuu ya Kanisa. Utamaduni huu, uanzwe kumwilishwa katika familia sanjari na Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, kwa wataalam kusaidia kufafanua maana ya alama hizi, ili kweli maadhimisho ya Fumbo la Pasaka yaweze kukita ujumbe wake katika sakafu ya nyoyo za waamini tayari kuutangaza na kuushuhudia kwa watu wa Mataifa.