Tafuta

Wajumbe na wadhamini wa Mfuko wa Papa "Papal Foundation " tarehe 28 Aprili 2022 wamekutana na kuzungumza na Papa Francisko Wajumbe na wadhamini wa Mfuko wa Papa "Papal Foundation " tarehe 28 Aprili 2022 wamekutana na kuzungumza na Papa Francisko 

Mfuko wa Papa Kielelezo Cha Mshikamano Na Huduma Ya Huruma Na Upendo

Taasisi imetekeleza dhamana na wajibu wake chini ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na sasa Papa Francisko. Tayari milioni 18 zimekwisha kutolewa kama msaada kwa Nchi za Kimisionari kwa ajili ya kugharimia: Ujenzi wa Makanisa 358, Seminari 170, nyumba za mapadre na watawa 404, shule 273 pamoja na hospitali 104. Imani katika matendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa Papa “Papal Foundation” ulianzishwa kunako mwaka 1988 kama kielelezo cha Imani tendaji, inayomwilishwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili kutoka kwa waamini wa Kanisa Katoliki nchini Marekani. Hiki ni kielelezo Madhubuti cha mshikamano katika huduma ya upendo inayotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Mfuko wa Papa ulianzishwa ukiwa na kianzio cha dola milioni moja. Ikumbukwe kwamba, hii ni Taasisi maalum iliyoanzishwa kwa ajili ya kumwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kutoa huduma ya upendo kwa wahitaji. Taasisi imetekeleza dhamana na wajibu wake chini ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na sasa Papa Francisko. Tayari milioni 18 zimekwisha kutolewa kama msaada kwa Nchi za Kimisionari kwa ajili ya kugharimia: Ujenzi wa Makanisa 358, Seminari 170, nyumba za mapadre na watawa 404, shule 273 pamoja na hospitali 104. Miradi yote hii imeidhinishwa na kupitishwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo madhubiti cha imani katika matendo.

Mfuko wa Papa ni kielelezo cha mshikamano wa huduma ya upendo.
Mfuko wa Papa ni kielelezo cha mshikamano wa huduma ya upendo.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, 28 Aprili 2022 amekutana na kuzungumza na wadhamini pamoja na wanachama wa Mfuko wa Papa katika hija ya upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza kwa kumwezesha kutoa msaada wa hali na mali kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia, hasa wale walioathirika kwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Wanafanya hija ya kiroho wakati huu, Mama Kanisa anapoendelea kusherehekea ushindi wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, iwe ni fursa ya imani na uaminifu wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mchango wao umekuwa na manufaa makubwa katika kuwajengea watu wa Mungu uwezo wa kukabiliana na changamoto katika sekta ya elimu, huduma ya upendo kwa maskini pamoja na shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Makanisa mahalia. Kwa njia hii, wanashiriki katika ujenzi wa utamaduni wa mshikamano na amani. Wajumbe wa Mfuko wa Papa wamesaidia sana kusoma alama za nyakati kwa kutoa msaada kwa waathirika wa vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urussi.

Mfuko huu ni kielelezo cha imani katika matendo
Mfuko huu ni kielelezo cha imani katika matendo

Kwa hakika, wamekuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo, matumaini na huruma kwa wale wote wanaoendelea kufaidika na huduma inayotolewa na Mfuko wa Papa. Huu ni utekelezaji wa mafundisho ya Kristo Yesu anayewataka waja wake kumwilisha Injili ya huruma na mapendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hiki ndicho kipimo siku ya hukumu ya mwisho. Rej. Mt 25: 40. Tangu mwanzo Mfuko wa Papa umejipambanua kama kielelezo makini cha mshikamano wa upendo. Baba Mtakatifu anasema, anawatumainia sana kwa sala na sadaka yao kwa ajili ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Amewaweka wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa.

Mfuko wa Papa
28 April 2022, 15:29