Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, anaendelea kuwasindikiza kwa sala na sadaka yake watu wa Mungu nchini Perù wanaopitia kipindi kigumu cha historia na maisha yao Baba Mtakatifu Francisko anasema, anaendelea kuwasindikiza kwa sala na sadaka yake watu wa Mungu nchini Perù wanaopitia kipindi kigumu cha historia na maisha yao 

Mshikamano wa Papa Francisko Kwa Familia ya Mungu Nchini Perù

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwasindikiza kwa sala na sadaka yake. Anawasihi wadau wakuu katika mgogoro huu, kukaa kwa pamoja na kuanza kutafuta suluhu ya kudumu kutokana na changamoto ambazo zimejitokeza, kwa kujikita katika amani, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Perù. Haki za wananchi wanyonge zilindwe na kuheshimiwa na wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maandamano makubwa yaliyoambatana na vurugu pamoja na ghasia, yalianza kufuka moshi kunako mwezi Machi 2022, kufuatia mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma muhimu nchini Perù. Hali hiyo ilimlazimisha Rais José Pedro Castillo Terrones wa Perù kutangaza hali ya hatari nchini mwake. Wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema, hizi ni athari za uvamizi wa kijeshi uliofanywa na Urussi nchini Ukraine na matokeo yake ni kupanda kwa gharama ya maisha, wakati ambapo hali ya maisha ya wananchi wengi inaendelea kuporomoka sana kutokana na mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma. Hivi karibuni mjini Lima kumefanyika maandamano makubwa yaliyopelekea wananchi wenye hasira kali kutaka kuvamia Bunge pamoja na kuharibu ofisi za Mahakama kuu nchini Perù. Rais José Pedro Castillo Terrones ameendelea na jitihada zake za kukutana na wapinzani ili kutafuta muafaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Perù bila mafanikio.

Wananchi Perù wanaendesha maandamano na migomo kupinga kupanda kwa gharama ya maisha
Wananchi Perù wanaendesha maandamano na migomo kupinga kupanda kwa gharama ya maisha

Wakati juhudi zote hizi zinaendelea, tarehe 7 Aprili 2022 Bunge la Perù lilipiga kura ya kutokuwa na imani na Rais na hivyo wakamtaka kujiuzuru kutoka madarakani. Kura 43 ziliafiki Rais kujiuzuru kutoka madarakani, wakati ambapo kura 43 zilipinga wazo hilo na kura moja haikupigwa. Wananchi wanataka Bunge lifutwe na uchaguzi mkuu ufanyike upya. Kwa muda wa miaka miwili sasa wanafunzi hawakuweza kuhudhuria masomo darajani kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Shule zilifunguliwa kwa muda mfupi tu na sasa zimefungwa tena kutokana na sababu za ulinzi na usalama wa rais na mali zao.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Dominika ya Matawi, tarehe 10 Aprili 2022 akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alipenda kuonesha uwepo wa karibu sanjari na mshikamano wa udugu wa kibinadamu wakati huu ambapo Perù inapitia kipindi kigumu katika historia ya nchi kutokana na machafuko ya kisiasa nchini humo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, anaendelea kuwasindikiza kwa sala na sadaka yake. Anawasihi wadau wakuu katika mgogoro huu, kukaa kwa pamoja na kuanza kutafuta suluhu ya kudumu kutokana na changamoto ambazo zimejitokeza, kwa kujikita katika amani, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Perù. Haki za wananchi wanyonge zilindwe na kuheshimiwa sanjari na kusimamia haki msingi za binadamu pamoja na haki zote za kijamii.

Papa Peru

 

12 April 2022, 08:49