Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Makardinali ameongoza Kesha la Pasaka 2022 na Papa Francisko kutoa mahubiri. Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Makardinali ameongoza Kesha la Pasaka 2022 na Papa Francisko kutoa mahubiri. 

Papa Francisko Kesha La Pasaka 2022: Wanawake Mashuhuda Wa Fumbo La Pasaka

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri kwenye Ibada ya Mkesha wa Pasaka kwa Mwaka 2022 amegusia kuhusu giza nene ambalo linaendelea kusababishwa na vita kati ya Urussi na Ukraine. Amekazia kuhusu ushuhuda angavu wa wanawake walioambiwa kwamba, Kristo Yesu amefufuka kwa wafu. Wakaangalia, wakasikiliza na kutangaza Fumbo la Pasaka ya Bwana kwa ari na ujasiri.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, katika maadhimisho ya Kesha la Pasaka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 17 Aprili 2022 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko kutoa mahubiri ambamo amekazia utume na ushuhuda wa wanawake jasiri wa Injili: Wakaangalia, wakasikiliza na kutangaza Fumbo la Pasaka. Kesha la Pasaka ni Mama wa mikesha yote ya Liturujia inayoadhimishwa na Mama Kanisa kwani humo ndimo Kanisa linaadhimisha Fumbo la Pasaka, kiini cha imani yake. Kesha la Pasaka limegawanyika katika sehemu kuu nne: Sehemu ya kwanza ni: Kubariki Moto wa Pasaka, kielelezo cha ufufuko wa Kristo, mwaliko kwa watoto wa Kanisa kukesha katika: Sala, Neno la Mungu na Adhimisho la Sakramenti za Kanisa ili kudumisha imani na matumaini katika ushindi wa Kristo Mfufuka. Ni ushindi unaoshuhudiwa kwa kubariki Mshumaa wa Pasaka na hatimaye, Mbiu ya Pasaka huimbwa ili kutangaza sifa za Mshumaa wa Pasaka, ambaye ni Kristo Yesu mwenyewe! Sehemu ya Pili ni Liturujia ya Neno, ambamo waamini wanatafakari mchakato wa historia nzima ya ukombozi inayofumbatwa katika Agano la Kale linalopata utimilifu wake katika Agano Jipya kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu uletao wokovu.

Liturujia ya Mwanga: Kielelezo cha Kristo Mfufuka
Liturujia ya Mwanga: Kielelezo cha Kristo Mfufuka

Sehemu ya tatu ni Liturujia ya Ubatizo, ambamo waamini wanarudia tena ahadi zao za ubatizo na wakatekumeni walioandaliwa wanapokea Sakramenti za Kanisa. Na sehemu ya Nne ni Liturujia ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Katika Kesha la Pasaka, Jumamosi, tarehe 16 Aprili 2022 Baba Mtakatifu Francisko amewasha Mshumaa wa Pasaka kwa moto mpya ambao pole pole umelifukuza giza na kuwaangaza waamini waliokuwa wamehudhuria kwenye Ibada ya Misa Takatifu, Mkesha wa Pasaka Mwanga wa Kristo Mfufuka katika utukufu unafukuzia mbali giza la moyo na roho, ili wote waweze kuishi katika mang’amuzi ya wale wanawake shupavu wa imani, walioona, wakasikiliza na kutangaza Fumbo la Pasaka, kiini cha Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri kwenye Ibada ya Mkesha wa Pasaka kwa Mwaka 2022 amegusia kuhusu giza nene ambalo linaendelea kusababishwa na vita kati ya Urussi na Ukraine. Amekazia kuhusu ushuhuda angavu wa wanawake waliotoka asubuhi na mapema siku ya kwanza ya juma kwenda kaburini wakipeleka manukato yaliyokuwa tayari, lakini wakakutana na watu wawili waliokuwa wamevaa nguo za kumeta meta nao wakawaambia kwamba, Kristo Yesu amefufuka kwa wafu. Wakaangalia, wakasikiliza na kutangaza Fumbo la Pasaka; maneno muhimu sana katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana.

Baba Mtakatifu anasema wanawake wanaona alama inayowapatia mvuto wa kufanya tafakari ya kina. Wanawake wakalikuta lile jiwe limeviringishwa mbali na kaburi, wakaingia, wasiuone mwili wa Bwana Yesu” Lk 24:2-3. Alama hii inakuwa ni chemchemi ya matumaini angavu, ambayo yanabeba ndani mwake changamoto nyingi. Kuna wakati ambapo, matumaini haya yanakosa nafasi katika sakafu ya nyoyo za waamini; yanasongwa na mashaka na hofu, kama ilivyokuwa kwa wale wanawake wanaosimulia katika Injili, lakini wanaingiwa na hofu na kuinama kifudifudi hata nchi. Katika hija ya maisha, kuna wakati ambapo waamini wanakata na kujikatia tamaa ya maisha. Wanajifunga katika ubinafsi na mahitaji yao; wanazama katika “litania ya malalamiko” mambo ambayo kamwe hayawezi kuleta mabadiliko katika maisha. Hali hii ni sawa na kusimama mbele ya Kaburi la Yesu kwa kujikatia tamaa na hatimaye, kufukia ile furaha ya kuishi. Kesha la Pasaka ni fursa ya kupata mwanga mpya katika maisha na kukiangalia kifo cha Kristo Yesu, kama chemchemi ya huruma na upendo wa upendo unaokumbatia ushindi wa kishindo. Kristo Yesu amefufuka kweli kweli. Ni wakati wa kuondoa uchungu, huzuni na masikitiko moyoni, ili hatimaye, kumfungulia Mungu malango ya matumaini.

Papa Mahubiri: Wakaangalia, wakasikiliza na kutangaza Fumbo la Pasaka
Papa Mahubiri: Wakaangalia, wakasikiliza na kutangaza Fumbo la Pasaka

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wanawake walisikiliza swali waliloulizwa na wale watu wawili waliovaa mavazi ya kumetameta wakisema “Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu? Hayupo hapa, amefufuka.” Haya ni maneno ya faraja kila wakati mwamini anapokosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha; wanapojikuta wakiwa wamefungwa katika maneno yao, mazoea na kanuni ya maisha. Lakini kwa bahati mbaya sana, waamini wanasahau kumtafuta Kristo Yesu katika giza na undani wa maisha yao; katika kilio na machungu ya maisha; katika mapambano, mateso na matumaini; Jibu la mkato ni kwamba, hayupo hapa! Waamini kamwe, hawawezi kuadhimisha Pasaka ya Bwana, huku bado wamejifungia katika kifo na maisha yao ya kale, kiasi cha kushindwa kuwa na ujasiri wa kumwavchia Mungu nafasi ya kuwasamehe, kutubu na kumwongokea, ili hatimaye, kuvunjilia mbali matendo ya giza. Na hivyo kuamua kutenda kwa ajili ya Kristo Yesu na upendo wake wa daima. Imani isigeuzwe na kuwa kama “uchawi” na hivyo kumfanya Mwenyezi Mungu kuwa ni kumbukumbu iliyopitwa na wakati. Waamini wanahimizwa kukutana na Mungu katika maisha yao, ili aweze kuwaletea mabadiliko katika maisha na ulimwengu katika ujumla wake. Ni wakati wa kuzika mazoea na utu wa kale kwa sababu hakuna Ukristo pasi na Pasaka ya Bwana aliyefufuka kwa wafu. Huu ni mwaliko wa kukutana na Kristo Yesu ambaye yuko hai na kujitahidi kumtafuta kati ya ndugu na historia; kati ya wale wanao tumaini; wale wenye ndoto; bila kuwasahau wanaolia, kuomboleza na kuteseka kwa sababu katika hali na mazingira kama haya hapo yupo Mwenyezi Mungu.

Papa Francisko amemshukuru Kardinali Giovanni Battista Re kwa kuongoza Kesha la Pasaka 2022.
Papa Francisko amemshukuru Kardinali Giovanni Battista Re kwa kuongoza Kesha la Pasaka 2022.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wanawake walitangaza na kushuhudia furaha ya Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Wakatangaza ushindi wa Mwenyezi Mungu dhidi ya dhambi na mauti. Mwanga wa Kristo Mfufuka ni mvuto kwa Mitume wamisionari wanaorejea Kaburini ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hawa ni wanawake waliomwona na kumsikiliza! Hawakujali sana kuhusu dhamana ya ushuhuda na hadhi yao kama wanawake wala maneno ya watu. Mama Kanisa hana budi kusimama kidete ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, ili Kristo Yesu aweze kuonekana tena, akitangazwa na kushuhudiwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Kristo Yesu, awe ni chemchemi ya amani, upatanisho, mahusiano na mafungamano kati ya watu, ili kukuza na kudumisha haki, usawa, ukweli, upendo na udugu wa kibinadamu. Waamini watambue na kukiri kwamba, Kristo Yesu ndiye chemchemi ya matumaini yao, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kristo Yesu anawakirimia waja wake maisha mapya kwa kugeuza maombolezo yao kuwa ni mchezo wa furaha. Huu ni mwaliko kwa waamini kuadhimisha Pasaka ya Bwana pamoja na Kristo Yesu aliye hai, ili aweze kuwaletea mageuzi na kuwaokoa. Dhambi na mauti hayana nguvu tena, kumbe, waamini wanaweza kuanza upya na kifo kiwe ni daraja na mwanzo mpya wa maisha. Hata katika usiku wa manane, Kristo Yesu, nyota angavu ya alfajiri anaendelea kung’aa.

Kesha la Pasaka

 

 

 

17 April 2022, 14:26