Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuomba msamaha wa dhati kutokana na nyanyaso, dhuluma na ukatili ambao Watu Asilia wa Canada wamekumbana nao katika maisha yao. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuomba msamaha wa dhati kutokana na nyanyaso, dhuluma na ukatili ambao Watu Asilia wa Canada wamekumbana nao katika maisha yao. 

Mshikamano Wa Kanisa Na Watu Asilia Canada: Haki & Upatanisho

Mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Watu Asilia wa Canada yanapania: Kufungua mchakato wa uponyaji wa madonda ya ndani, tayari kujikita katika mchakato wa ukweli, haki na upatanisho. Amewashukuru kwa sala, tafakari na ushuhuda wao wa pamoja, ambao wanataka kuutekeleza katika uhalisia wa maisha kwa kutembea pamoja kama ndugu wamoja. Upatanisho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Watu Asilia wa Canada “Mètis National Council, MNC” liliundwa kunako mwaka 1983 kwa lengo la kuragibisha haki msingi za watu asilia ndani na nje ya Canada. Hili ni Baraza ambalo limekuwa mstari wa mbele kulinda, kutetea na kuragibisha haki msingi za Watu Asilia wa Canada mintarafu sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu pamoja na kuweza kujiendeleza wenyewe kama raia wa Canada. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 28 Machi 2022 hadi tarehe 1 Aprili 2022 amekuwa akikukutana na kuzungumza na kundi la “Mètis, Inuits na First Nations, Premières Nations”. Haya ni makundi ya Watu Asilia wa Canada. Baba Mtakatifu Francisko ametia nia ya kuwatembea Watu Asilia wa Canada panapo majaliwa yake Mwenyezi Mungu, ili kushuhudia maeneo wanakoishi, kukutana na kusalimiana na familia zao kama ushuhuda wa uwepo wake wa karibu katika maisha na utume wao. Tarehe 1 Aprili 2022 amekutana na makundi haya matatu katika ujumla wake.

Mifumo mbalimbali ya ukokini ni hatari kwa utu, heshima na haki msingi.
Mifumo mbalimbali ya ukokini ni hatari kwa utu, heshima na haki msingi.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuomba msamaha wa dhati kutokana na nyanyaso, dhuluma na ukatili ambao Watu Asilia wa Canada wamekumbana nao katika maisha yao ya kila siku. Amependa kuwahakikishia kwamba, daima Kanisa litaendelea kuwa upande wa maskini, wanyonge na wale wote wanaoendelea kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Watu Asilia wa Canada yanapania pamoja na mambo mengine kufungua malango ya mchakato wa uponyaji wa madonda ya ndani, tayari kuanza kujikita katika mchakato wa ukweli, haki na upatanisho wa Kitaifa. Amewashukuru kwa mchango wao wa sala, tafakari na ushuhuda wao wa pamoja, ambao wanataka kuutekeleza katika uhalisia wa maisha kwa kutembea pamoja kama ndugu wamoja.

Baba Mtakatifu amewataka kujenga, kudumisha na kuimarisha mafungamano ya kijamii kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, lengo ni kutunza kumbukumbu endelevu na utambulisho kwa ajili ya maboresho ya maisha ya watu. Amewapongeza kwa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni watu waliokirimia tamaduni, sanaa na lugha; tunu msingi zinazopaswa kuendelezwa. Baba Mtakatifu amesikitika sana na madhara yaliyosababishwa na mifumo mbalimbali ya ukoloni nchini Canada, yaliyopelekea nyanyaso, dhuluma na uonevu sanjari na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote kwa ajili ya mafao ya watu binafsi. Ukoloni amepelekea pia kupandikizwa kwa utamaduni wa kifo, usiojali wala kuthamini: utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Hata leo hii, bado kuna ukoloni wa kiitikadi, kiuchumi na kisiasa. Hii ni mifumo inayosimikwa katika uchu wa mali, madaraka na faida kubwa kwa gharama ya maisha na historia ya watu mahalia. Ni mifumo inayoharibu sana mazingira nyumba ya wote. Kumbe, ni wajibu na dhamana ya watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kupambana na mifumo hii tenge. Kwa hakika imesababisha anasema Baba Mtakatifu mateso makubwa kwa familia, kwa kujikita katika sera za kibaguzi, maamuzi mbele na nyanyaso katika maeneo ya nyumbani na kwa wanafunzi katika maeneo ya shule. Watu Asilia wa Canada wakadhalilishwa na kutwezwa kiasi cha kupoteza utambulisho wa kitamaduni, madhara ambayo watu hawa wamekumbana nayo katika historia ya maisha. Haya ni mambo ambayo Baba Mtakatifu anasema yanamsikitisha sana kutoka moyoni mwake.

Utu, heshima na haki msingii za binadamu ni muhimu sana
Utu, heshima na haki msingii za binadamu ni muhimu sana

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, yamegusa na kutikisa utu, heshima na utambulisho wao wa kitamaduni na maisha ya kiroho. Haya ni mambo ambayo yanakwenda kinyume kabisa cha tunu msingi za Injili. Baba Mtakatifu anapenda kuungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Canada kuomba msamaha kwa ukatili, nyanyaso na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Kanisa linapenda kujikita katika mchakato wa upendo, ukarimu na huduma bila kuhukumu wala “kuchefuliwa” na maamuzi mbele. Ni mwaliko wa kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wale wote waliosimama kidete katika imani, heshima, utu na ukarimu, wakatangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili kwa ari na moyo mkuu; mambo msingi ambayo yamewawezesha kuimarisha mshikamano kati ya kizazi kimoja hadi kingine. Baba Mtakatifu anawasihi Maaskofu Katoliki nchini Canada kujielekeza zaidi katika mchakato wa kutafuta na kudumisha ukweli na uwazi; kuganga na kuponya madonda, tayari kujikita katika upatanisho wa Kitaifa. Ni wajibu wa Mama Kanisa kuwa ni shuhuda na chombo cha upendo; majadiliano katika ukweli na uwazi, ili hatimaye kujenga jamii inayosimikwa katika furaha na tunu msingi za Kiinjili.

Kwa upande wake, Askofu Raymond Poisson, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Canada “The Canadian Conference of Catholic Bishops (CCCB)” lililoanzishwa kunako mwaka 1943 na kutambuliwa rasmi na Vatican mwaka 1948 amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kutenga muda wa kusikiliza: historia, amana na utajiri wao wa kitamaduni; imani, matumaini na madonda yao ya ndani, bila kusahau kilio chao kutokana na nyanyaso na dhuluma walizokutana nazo katika maisha. Kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Canada, amewatambulisha wajumbe mia mbili waliokuwa wameandama naye. Wote hawa katika umoja na utofauti wao ni sehemu muhimu sana ya watu wa Mungu nchini Canada. Wote hawa wako tayari katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika msingi wa haki, umoja na udugu wa kibinadamu. Kipaumbele cha kwanza kwa sasa nchini Canada ni mchakato wa upatanisho wa Kitaifa, ili kujenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu.

Askofu Raymond Poisson anasema Kanisa nchini Canada linajivunia kuwa na Mtakatifu Kateri Tekakwitha ambaye ataendelea kuwasindikiza katika hija ya haki na upatanisho wa Kitaifa, huku akiwaombea watu wa Mungu nchini Canada waweze kutambua mapenzi ya Mungu na kuyatekeleza katika maisha yao, tayari kujikita katika upatanisho wa Kitaifa. Itakummbukwa kwamba, Mtakatifu Kateri Tekakwitha (kwa lugha yake ya Kimohawk jina linatamkwa ˈgaderi degaˈgwita) aliishi tangu mwaka 1656 hadi 17 Aprili 1680. Mtakatifu Kateri alizaliwa Ossernenon, leo Auriesville, New York, Marekani, akafariki dunia huko Kahnawake, Quebec nchini Canada. Ni mtoto kutoka familia ya Watu Asilia wa Amerika ya Kaskazini. Anajulikana hasa kwa imani na maadili yake ya Kikristo, dini aliyojiunga nayo na kubatizwa mwaka 1676, na kudumu katika imani thabiti licha ya pingamizi na changamoto alizokumbana nazo kutoka ndani ya familia yake. Alitangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni Mwenye heri tarehe 22 Juni 1980, na hatimaye Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 21 Oktoba 2012.

Watu Asilia Canada

 

 

 

02 April 2022, 14:02