Tafuta

Nyumba zilivyoharibiwa huko  Mariupol Nyumba zilivyoharibiwa huko Mariupol 

Utayari wa Papa Francisko kufanya kila iwezekanavyo kusimamisha vita

Katika gazeti la Osservatore Romano limechapisha muhtasari wa mahojiano yaliyotolewa na Papa katika gazeti la Argentina liitwalo"La Nación".Papa amesema"Vita vyote ni vya kivita katika ulimwengu huu na katika ngazi hii ya ustaarabu. Majaribio ya Vatican katika harakati za kuweza kufikia amani hayatakoma kamwe.Papa ameeleza kuahirishwa kwa mkutano na Kirill.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

“Niko tayari kufanya lolote ili kukomesha vita”. Haya ni maneno yaliyosikia katika mahojiano na gazeti la Argentina la: “La Nación” lililochapishwa Alhamisi tarehe 21 Aprili 2022, ambapo Papa Francisko hakutumia maneno ya kuzunguka ili kuthibitisha kipaumbele cha kupatikana kwa amani nchini Ukraine. Kwa mwandishi wa habari Joaquín Morales Solá, Papa Francisko alithibitisha kwamba: "siku zote kuna juhudi za kufikia amani. Vatican haitulii kamwe. Siwezi kukuambia kwa undani kwa sababu hazingekuwa tena juhudi za kidiplomasia. Lakini majaribio hayatakoma.”

Alipoulizwa kuhusu ziara yake, aliyofanya siku ile asubuhi ya Februari 25, kwa Ubalozi wa Shirikisho la Urussi kwa mwakilishi Vatican, kupitia njia ya Conciliazione, Papa amesema: “Nilikwenda peke yangu. Sikutaka mtu yeyote anisindikize. Ilikuwa ni jukumu langu binafsi. Ulikuwa ni uamuzi nilifanya mkesha usiku nikifikiri kuhusu Ukraine. Ni wazi kwa wale wanaotaka kuona mambo nilivyokuwa nikielekeza kwa serikali kwamba wanaweza kumaliza vita mara moja. Kusema kweli, nilitaka kufanya kitu ili kuhakikisha kwamba kusitokee kifo hata kimoja zaidi nchini Ukraine. Na wala hata mmoja zaidi. Na niko tayari kufanya chochote”.

Na juu ya sababu zilizoanzisha vita hivyo, Papa amesema: “Vita vyote ni vya kivita katika ulimwengu huu na katika ngazi hii ya ustaarabu. Kwa maana hiyo nilibusu hadharani bendera ya Ukraine. Hi ilikuwa ni ishara ya mshikamano na waliokufa, familia zao na wale ambao walilazimika kuhama”. Zaidi ya hayo, juu ya uwezekano wa safari yake ya kwenda Kiev, Papa ameeleza: “Siwezi kufanya chochote kinachohatarisha malengo ya yaliyo ya juu, ambayo ni mwisho wa vita, suluhisho, au angalau uwezekano wa mkondo wa kibinadamu. Je inafaa nini kwa Papa kwenda Kiev ikiwa vita vitaendelea siku iliyofuata?

Katika swali kutoka kwa mwandishi wa habari kuhusu “Kwa hamtaji Putin au Urussi?”, Papa Francisko amejibu kwamba: “Papa kamwe hataji mkuu wa nchi, sembuse nchi, ambayo ni bora kuliko mkuu wake wa nchi”. Papa Francisko pia alizungumza juu ya uhusiano mzuri sana na juu ya mkutano unaowezekana na Patriaki wa Moscow, Kirill. “Ninasikitika kwamba Vatican ililazimika kughairi mkutano wa pili na Patriaki Kirill, ambao tulikuwa tumepanga kufanya mwezi Juni huko Yerusalem. Lakini diplomasia yetu ilionelea kuwa mkutano kati yetu kwa wakati huu unaweza kusababisha machafuko mengi. Siku zote nimehamasisha mazungumzo ya kidini. Nilipokuwa askofu mkuu wa Buenos Aires niliunganisha Wakristo, Wayahudi na Waislamu pamoja katika mazungumzo yenye matunda. Ilikuwa ni moja ya mipango ninayojivunia sana. Ni sera ile ile ninayohamasisha Vatican. Kama umenisikia nikisema mara nyingi, kwangu mimi makubaliano ni bora kuliko mzozo.”

22 April 2022, 18:36