Sherehe ya Huruma ya Mungu inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka Dominika ya Pili ya Kipindi cha Pasaka, mwaliko wa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani. Sherehe ya Huruma ya Mungu inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka Dominika ya Pili ya Kipindi cha Pasaka, mwaliko wa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani. 

Sherehe Ya Huruma Ya Mungu: Iweni Mashuhuda Na Vyombo Vya Huruma Ya Mungu

Papa Francisko: Sherehe ya Huruma ya Mungu inaadhimishwa na Mama Kanisa, Dominika ya Pili baada ya Sherehe ya Pasaka. Sherehe ya huruma ya Mungu ni shule ya huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Hapa ni mahali pa kujifunza huruma ya Mungu, ili hatimaye, kuimwilisha katika uhalisia wa maisha ili kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na haki” anasema, huruma ya Mungu inapaswa kuendelezwa katika medani mbali mbali za maisha ya watu kama utimilifu wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Huruma ya Mungu inajionesha katika maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa, lakini kwa namna ya pekee kabisa, Sakrameti ya Ekaristi Takatifu, Upatanisho na Mpako wa Wagonjwa. Huruma ya Mungu inaendelea kujifunua katika historia na maisha ya watu kwa njia ya Neno la Mungu, ikikumbukwa kwamba, Biblia ni muhtasari wa ufunuo wa huruma ya Mungu kwa binadamu!

Mihimili ya Habari Njema ya Wokovu na hasa zaidi Mapadre na Mashemasi wanatakiwa kuhakikisha kwamba, wanaandaa mahubiri yao vyema na kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayojikita katika: ukarimu, ushuhuda wa maisha, msukumo wa kichungaji, uwazi na utayari wa kutoa huduma ya huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Uso wa huruma “Misericordia vultus” na “Misericordia et misera” yaani “Huruma na haki” ni nyaraka zinazoweza kuwasaidia waamini kutambua na kuthamini ukuu wa huruma na upendo wa Mungu changamoto anasema Baba Mtakatifu ni kwa Jumuiya za Kikristo kuhakikisha kwamba, zinaendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, kama kielelezo makini cha imani tendaji. Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole unaooneshwa na Mama Kanisa kwa waamini wake. Hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonyesha huruma na upendo.

Mama Kanisa anataka kutangaza na kushuhudia Huruma ya Mungu
Mama Kanisa anataka kutangaza na kushuhudia Huruma ya Mungu

Kanisa “lina hamu isiyo na kikomo katika kuonesha na kushuhudia huruma ya Mungu". Baba Mtakatifu Francisko anasema, huenda tumejisahau kwa muda mrefu jinsi ya kuonesha na kuiishi huruma ya Mungu. Kishawishi, kwa upande mmoja ni kutaka kulengea tu haki, kimewafanya waamini kusahau kwamba, hii ndiyo hatua ya kwanza tu, muhimu na isiyoweza kukwepeka. Lakini Kanisa linahitaji kupiga hatua kubwa na kuwania lengo la juu na la maana zaidi. Kwa upande mwingine, Papa Francisko anasikitika kusema, watu wa Mungu wanapaswa kukubali kuwa tendo la huruma linafifia zaidi na zaidi katika utamaduni mamboleo. Mara nyingi, neno hili linaonekana kutokomea kimatumizi. Hata hivyo, bila ushuhuda wa huruma, maisha yanakuwa bila matunda na tasa, kana kwamba imetengwa jangwani. Wakati umewadia kwa Mama Kanisa kuitikia kwa mara nyingine tena huu wito wa furaha wa huruma na msamaha. Ni wakati wa kurudi kwenye msingi wa imani na kubeba madhaifu na mahangaiko ya watu wa Mungu. Huruma ni msukumo unaoamsha maisha mapya na kuwatia waamini ujasiri wa kuangalia siku za usoni kwa matumaini makubwa, licha ya wasi wasi na giza nene ambalo linaendelea kutanda kwa sasa kutokana na vita na magonjwa kama vile Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Dominika au Sherehe ya Huruma ya Mungu inaadhimishwa na Mama Kanisa, Dominika ya Pili baada ya Sherehe ya Pasaka. Sherehe ya huruma ya Mungu ni shule ya huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Hapa ni mahali pa kujifunza huruma ya Mungu, ili hatimaye, kuimwilisha katika uhalisia wa maisha ili kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa jirani. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano 20 Aprili 2022 amewashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu nchini Poland kwa kuwa ni mashuhuda na vyonbo vya huruma na upendo wa Mungu kwa wakimbizi wa vita kutoka nchini Ukraine. Wakimbizi hawa wanaonja huruma na upendo wa Mungu unaofunuliwa kwao. Huu ni mwaliko pia wa kuwakumbuka na kuwazamisha: wazee, wagonjwa na wale wote waliovunjika na kupondeka moyo kwenye bahari ya huruma ya Mungu. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, awakirimie na kupyaisha tena imani na matumaini ndani mwao.

Huruma ni utambulisho wa Mwenyezi Mungu
Huruma ni utambulisho wa Mwenyezi Mungu

Baba Mtakatifu anasema sababu msingi zilizomfanya kuitisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kuanzia tarehe 8 Desemba 2015 Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili hadi tarehe 20 Novemba 2016 kwanza kabisa ni: sala, tafakari na mafundisho ya viongozi wa Kanisa waliotangulia, kwa kuona kwamba, Kanisa ni sawa na hospitali iliyoko kwenye uwanja wa vita, Kanisa linapaswa kuwa karibu zaidi na waamini wake ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu. Kanisa lilikuwa linahitaji muda wa mageuzi katika maisha na utume wake, kwani watu wengi kwa sasa wamepoteza dhana ya dhambi pamoja na kuhisi kwamba, hakuna uwezekano wa kusamahewa dhambi zao. Uulimwengu mamboleo umejeruhiwa sana kutokana na magonjwa ya kijamii, yaani: ujinga, maradhi, umaskini, mipasuko ya kijamii, utumwa mamboleo pamoja na kutopea kwa imani. Kutokana na sababu zote hizi, binadamu anahitaji huruma ya Mungu na kwamba, huruma ni utambulisho wa Mungu ambaye licha ya magumu yanayomsibu na kumwandama mwanadamu, lakini bado anabaki kuwa mwaminifu katika ahadi zake. Waamini wanapaswa kutambua ubaya wa dhambi kama anavyoelezea Nabii Ezekieli, ili kuambata huruma na msamaha wa Mungu, kwa mwamini kutambua dhambi na mapungufu yake, tayari kutubu na kumwongokea Mungu.

Hapa Baba Mtakatifu anawaalika Mapadre kujisadaka kwa ajili ya kuwaungamisha waamini wao kwa: Ibada, ari na moyo mkuu. Pale ambapo muungamishaji anashindwa kumwondolea mwamini dhambi zake, basi walau ampatie baraka, ili kumwonjesha upendo wa Mungu hata kwa mwamini ambaye kutokana na sababu mbalimbali hawezi kupokea Sakramenti za Kanisa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, waungamishaji wana dhamana na wajibu nyeti sana, kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Mapadre wawe na ujasiri wa kuwasikiliza kwa makini waamini wanaokimbilia huruma ya Mungu katika maisha yao, kwani kuna baadhi yao wanatambua kwamba, hawawezi kupokea Sakramenti za Kanisa kutokana na vikwazo mbali mbali, lakini wanaweza kupata baraka ya kusonga mbele katika maisha yao ya Kikristo. Baba Mtakatifu anazungumzia kuhusu zawadi na umuhimu wa maungamo. Anakiri kwamba, mwamini anaweza kuomba huruma ya Mungu moja kwa moja bila kupitia kwa viongozi wa Kanisa waliopewa dhamana na kuwaondolea watu dhambi zao. Lakini, Mama Kanisa kwa busara yake, anataka watoto wake kuonesha moyo wa toba kwa kumwendea Padre anayemwakilisha Kristo Yesu katika kiti cha maungamo, Mahakama ya Huruma ya Mungu.

Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu, shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu
Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu, shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu

Hii ndiyo njia sahihi ya kuweza kupata: upendo, huruma na msamaha wa Mungu ambao kimsingi una mwelekeo pia wa kijamii, tayari kuponya madonda, mipasuko na kinzani za kijamii. Waamini wanakwenda kwenye kiti cha huruma ya Mungu si kwa kutaka kuhukumiwa, bali kukutana na hatimaye, kuambata upendo na huruma ya Mungu inayoendelea kuusimamisha ulimwengu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linalaani dhambi, lakini linamkumbatia mdhambi anayetambua dhambi zake na udhaifu wake tayari kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Kanisa halina budi kusamehe bila kuchoka kama anavyofundisha Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake. Mwenyezi Mungu yuko radhi kumpokea mwamini anayeonesha moyo wa toba na wongofu wa ndani, tayari kukumbatia na kuambata huruma ya Mungu. Kanisa lipo ili kuwawezesha waamini kukutana na huruma ya Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu anasema, ili Kanisa liweze kutekeleza dhamana na wajibu wake, halina budi kutoka kwa kutambua kwamba, Kanisa ni kama hospitali kwenye uwanja wa vita, ambako linakutana na majeruhi wanaohitaji kusikilizwa, kueleweka, kusamahewa pamoja na kuonjeshwa upendo. Waamini wakaribishwe kwa heshima na taadhima wanapokimbilia huruma ya Mungu, bila kuwanyanyasa wala kuwakejeri. Upendo wa Mungu unaowakumbatia wadhambi wakati mwingine unaonekana kuwa ni kashfa mbele ya macho ya binadamu.

Yesu anataka kuwaponya na kuwaokoa wale wanaoteseka kiroho na kimwili; tayari kuwaonjesha upendo na huruma ya Mungu. Waamini wanapaswa kushinda kishawishi cha kujiona kuwa ni watakatifu, wenye haki na wateule, bali watambue kwamba, ni wadhambi na wanahitaji kweli huruma na upendo wa Mungu. Hapa Kanisa linapaswa kuwafungulia watu malango ya huruma ya Mungu katika ukweli na uwazi pasi na unafiki. Kanisa lisiwatwishwe watu mizigo mizito, bali liwaonjeshe waamini huruma ya Mungu pasi na kumezwa na malimwengu, uchu wa fedha pengine hata madaraka. Baba Mtakatifu anasema, Mdhambi anaweza kuvumiliwa lakini fisadi na mla rushwa, hawa ni watu hatari kwani wanatenda dhambi lakini si wepesi kuungama dhambi zao, tayari kujipatanisha na Mungu. Mafisadi na wala rushwa ni watu wanaowatesa na kudhalilisha wananchi wengine; ni wanafiki. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko aliwaalika na kuwaasa mafisadi na wala rushwa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuanza ukurasa mpya wa maisha yao. Wamwombe Mungu neema ya kuona aibu kwa dhambi walizotenda. Huruma ni chachu muhimu sana inayoweza kudumisha umoja na udugu kati ya watu na kwamba, haki peke yake haitoshi, bali inapaswa kukamilishwa na fadhila ya huruma na mapendo, kwani Mungu anavuka haki na kwamba, hakuna haki pasi na msamaha.

Waamini wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa jirani
Waamini wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa jirani

Msamaha ni msingi wa maisha ya jamii inayojikita katika haki na mshikamano na kwamba, huruma inapaswa kumwilishwa katika maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ndiyo maana Kanisa linapinga adhabu ya kifo. Familia ni shule ya kwanza ya huruma ya Mungu na kwamba hapa wanafamilia wanajifunza kupenda na kupendwa, kusamehe na kusamehewa. Si matarajio yake kuona malango ya magereza yanafunguliwa na wafungwa wote kuachiwa huru hata wale waliotenda makosa makubwa ya jinai. Hapa Baba Mtakatifu anakaza kusema, wafungwa wasaidiwe kutubu, kuongoka na kuanza tena kuandika ukurasa mpya wa maisha yao, wakiwa ni watu wema zaidi kuliko walivyoingia magerezani. Kumbe, huduma ya kiroho kwa wafungwa magerezani ni sehemu muhimu sana ya Kanisa kama chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu. Itakumbukwa kwamba, Dominika ya Huruma ya Mungu ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000. Mtakatifu Maria Faustina Kowalska ni kati ya watakatifu waliotangaza, wakashuhudia na hatimaye, kueneza Ibada ya huruma ya Mungu.

Chemchemi ya huruma ya Mungu inafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Ibada ya huruma ya Mungu inakolezwa kwa kwa njia ya Novena ya Huruma ya Mungu inayoanza Ijumaa kuu, Siku ile Kristo Yesu alipoteswa na kufa Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kuhitimishwa katika maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu. Kuna Saa kuu la Huruma ya Mungu, huu ni mwaliko kwa waamini kujizamisha katika huruma ya Mungu, ili kuiabudu, kuitukuza na kusifu uweza mkuu wa Mungu katika kuwahurumia na kuwakomboa wadhambi. Huruma ya Mungu imeshinda haki! Waamini wanahamasishwa kukuza na kudumisha Ibada na uchaji wa Mungu wanapoadhimisha Sakramenti za Huruma ya Mungu yaani: Ekaristi Takatifu na Upatanisho, chemchemi ya utakatifu na mchakato katika uinjilishaji mpya unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Rozari ya Huruma ya Mungu ni chombo cha Ibada kinachowaunganisha waamini wote kuomba huruma ya Mungu kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu mzima. Kristo Yesu ni mwokozi Mwenye Huruma isiyokuwa na kifani. Rozari ya Huruma ya Mungu inawasaidia waamini kutekeleza dhamana na wajibu wao wa Kikuhani, waliojitwalia wakati walipobatizwa. Kwa njia hii, wanapyaishwa na kuwa ni sadaka safi inayounganishwa na Sadaka ya Kristo Yesu, Mfalme wa amani, haki, upendo na huruma!

Papa Huruma ya Mungu 2022

 

21 April 2022, 10:43