Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 1 Aprili 2022 amekutana na kuzungumza na Wanachama wa Mfuko wa Usonzi Italia “Fondazione Italiana Autismo.” Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 1 Aprili 2022 amekutana na kuzungumza na Wanachama wa Mfuko wa Usonzi Italia “Fondazione Italiana Autismo.” 

Siku ya Usonji Duniani 2 Aprili 2022: Mshikamano Wa Upendo

Baba Mtakatifu Francisko amekazia umuhimu wa jamii kujikita katika utamaduni shirikishi dhidi ya utamaduni wa kutupa; Ushiriki mkamilifu ili kubomolea mbali kuta za utengano na nyanyaso na hatimaye, umuhimu wa kujenga mtandao wa mshikamano katika huduma, sala na upendo. Mduko wa Usonzi Italia unajielekeza katika katika tafiti na huduma za maisha ya kiroho na kiutu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Usonji “Autism”, ni ugonjwa ambao kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani, WHO, hukumba mtoto mmoja kati ya kila watoto 160 duniani. Usonji ni tatizo la kibaiolojia analopata mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake na dalili huonekana kuanzia umri wa miaka mitatu na kuendelea. Kabla ya hapo wataalamu wanasema ni aghalabu kuona dalili hizo ambapo zinapojitokeza mtoto hukosa mbinu za mahusiano na mafungamano ya kijami kiasi cha kushindwa kuzungumza na wakati mwingine kurukaruka na hata kujing’ata. Watoto hawa kutokana na tatizo hilo wengine hutekelezwa na jamii na kunyimwa haki zao za msingi ikiwemo kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa. Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Aprili, inaadhimisha Siku ya Usonji Duniani, lengo ni kutoa elimu zaidi, ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii, ili kuwasaidia watoto wanaoteseka kwa ugonjwa huu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 1 Aprili 2022 amekutana na kuzungumza na Wanachama wa Mfuko wa Usonzi Italia “Fondazione Italiana Autismo.”

Maadhimisho ya Siku ya Usonji Duniani
Maadhimisho ya Siku ya Usonji Duniani

Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa jamii kujikita katika utamaduni shirikishi dhidi ya utamaduni wa kutupa; Ushiriki mkamilifu ili kubomolea mbali kuta za utengano na nyanyaso na hatimaye, umuhimu wa kujenga mtandao wa mshikamano katika huduma, sala na upendo. Mfuko wa Usonzi Italia “Fondazione Italiana Autismo” tangu mwaka 2015 umekuwa ukiwahusisha watafiti, madaktari na vyama vya kifamilia ili kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo na mshikamano kwa Watoto walioathirika kwa ugonjwa wa Usonji. Mwelekeo huu umesaidia kuvunjilia mbali utamaduni wa kutupa sanjari na uchumi unaobagua, ili kudumisha usawa. Leo hii kuna ushindani mkubwa, kiasi kwamba, wenye nguvu ndio wanaopewa nafasi ya kuishi na wanyonge hawana nafasi tena katika jamii. Matokeo yake kuna umati mkubwa watu wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali zao. Rej. Evangelii gaudium 53. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni shirikishi dhidi ya utamaduni wa kutupa, kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Ushiriki mkamilifu usaidie kubomoa ubaguzi, maamuzi mbele na utengano.
Ushiriki mkamilifu usaidie kubomoa ubaguzi, maamuzi mbele na utengano.

Mwelekeo huu unapaswa kuchukuliwa kama wito wa maisha unaomsukuma mtu kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kutumia karama na mapaji yake kwa ajili ya jirani zake wenye shida zaidi. Hii ni njia inayowaelekeza watu wa Mungu katika ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika huduma. Pili, Baba Mtakatifu anawataka wanachama hawa kujenga na kudumisha utamaduni wa ushiriki mkamilifu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili. Lengo ni kuwaendeleza Watoto walioathirika na ugonjwa wa Usonji katika medani mbalimbali za maisha, ili hatimaye kuondokana na ubaguzi, maamuzi mbele pamoja na ukosefu wa usawa. Tatu, wajitahidi kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo na mshikamano katika sala, huduma ya upendo na kushirikishana mema ya nchi, daima Watoto wagonjwa wakipewa kipaumbele cha kwanza. Mshikamano wa udugu wa kibinadamu uwe ni kiini cha sera na mikakati ya kiuchumi, ili hatimaye, kujenga na kudumisha uchumi shirikishi.

Usonjo 2022

 

01 April 2022, 14:20