Papa Francisko: Dhamana Na Wajibu Wa Chuo Kikuu Cha Kikatoliki Duniani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kunako mwaka 1919, watu watano mashuhuri akina Padre Agostino Gemelli, Ludovico Necchi, Francesco Olgiati, Armida Barelli pamoja na Ernesto Lombardo walianzisha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” “L'Università Cattolica del Sacro Cuore (UCSC) Jimbo kuu la Milano. Kilianza kufanya kazi rasmi tarehe 7 Desemba 1921 ili kujibu hitaji la mahali pa malezi na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya nchini Italia, changamoto iliyovaliwa njuga na matokeo yake Chuo hiki kimeendelea kukua na kupanuka na hatimaye, kuwa ni jukwaa la malezi na majiundo ya kielimu kitaifa na kimataifa. Ni kati ya vyuo vikuu vya kikatoliki maarufu sana Barani Ulaya. Hiki ni Chuo Kikuu cha Kikatoliki ambacho kimewekeza sana katika tafiti makini, ili kuendelea kusoma alama za nyakati. Haya ni matokeo ya sadaka kubwa ya akili na ukarimu inayotekelezwa na wadau wa Jumuiya ya Chuo kikuu, bila kusahau kwamba, wanafunzi wana imani na wanathamini sana mchango huu. Tarehe 13 Aprili 2021, Askofu mkuu Mario Delpin wa Jimbo kuu la Milano aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya uzinduzi wa Jubilei ya Miaka 100 tangu Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” Jimbo kuu la Milano, kilipoanzishwa.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe kwa maadhimisho haya alikazia kuhusu: “dhana ya moto” wa elimu ambao umewasha, kurithishwa na kushuhudiwa na wadau mbalimbali katika sekta ya elimu. Anasema, Elimu ni njia makini ya kujenga na kudumisha utu, heshima haki msingi za binadamu. Huu ni urithi mkubwa wa kitamaduni na maisha ya kiroho unaotoa utambulisho wa Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore.” Kuelimisha maana yake ni kuwasha moto wa elimu unaoweza kushuhudiwa na mtu binafsi na jumuiya katika ujumla wake. Hii ni historia ya miaka 100 inayong’arishwa na imani, elimu, ujuzi na maarifa, tayari kujielekeza kwa siku za usoni! Baba Mtakatifu aendelea kufafanua kuhusu matumaini, ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, huo ni utamaduni wa kutupa. Chuo kikuu ni mahali pa kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini sanjari na mchakato wa malezi mtambuka unaotekelezwa na wadau mbalimbali ndani ya jamii. Hii ni dhamana ya majalimu wa Chuo kikuu, wanaopaswa kuhakikisha kwamba, moto huu unaendelea kuwaka hadi kieleweke.
Elimu isaidie kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii, ili kujibu maswali msingi yanayotolewa na jamii, bila woga wala makunyanzi. Ukweli, uwazi na ukarimu ni amali za kijamii zinazopaswa kurithishwa kwa vijana wa kizazi kipya. Upyaisho wa mfumo wa elimu katika ulimwengu mamboleo utawasaidia watu wa Mungu kupambana na changamoto zinazojitokeza kwa wakati huu, ili kujenga leo na kesho yenye matumaini. Elimu ni upendo unaowajibisha na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, ili kuondokana na ubinafsi unaopelekea watu kutokuthaminiana. Kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano unaosimikwa katika kipaji cha kusikiliza, kujadiliana na maelewano. Mabadiliko ya mfumo wa elimu duniani yanapaswa kuwahusisha wadau mbalimbali katika sekta ya elimu, ili kuondokana na ukosefu wa haki jamii; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili hatimaye, kuweza kupambana na umaskini pamoja na tabia ya watu kutowajali na kuwathamini wengine.
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya 98 ya Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” amewataka wadau katika sekta ya elimu kuwasha moto wa matumaini kwa vijana wa kizazi kipya, utakaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu. Hii ni fursa ya kufanya kumbukizi la historia iliyopita, ari na mwamko katika huduma, kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Uwepo na ukarimu wa Mungu ni kielelezo cha upendo na faraja ya Mungu kwa watu wanaoteseka. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Dominika, Mei Mosi, 2022 amemtaja Mwenyeheri Armida Barelli, Muasisi na mwamasishaji wa Utume wa Vijana Wakatoliki Italia, aliyewataka kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili huduma kwa Kanisa na jamii katika ujumla. Mwenyeheri Armida Barelli alishirikiana na Padre Gemelli kuanzisha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore.”
Mei Mosi, 2022 Kanisa nchini Italia limeadhimisha Siku ya Kitaifa ya Chuo Kikuu cha “Sacro Cuore” na kwa mwaka huu, maadhimisho haya yamenogeshwa na kauli mbiu “Kwa moyo wa mwanamke katika huduma ya utamaduni na katika jamii.” Mwenyeheri Armida Barelli aliyekuwa Mtunza Hazina wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki, alifanikiwa kila mwaka kuadhimisha Siku ya Chuo Kikuu Kikatoliki Kitaifa kwa kuwaalika watu wa Mungu kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika elimu. Leo hii Kardinali Pietro Parolin anasema, Mwenyeheri Armida Barelli anapaswa kukumbukwa kama shuhuda na chombo cha amani, upatanisho na matumaini kwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huyu ni mwanamke aliyefanikiwa kuunganisha uaminifu kwa Mungu na ufanisi katika Taasisi hii, mchango mkubwa kutoka kwa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa muda wa mika thelathini, aliongoza Utume wa Wasichana Wakatoliki, kwa kukazia majiundo na malezi huru ya vijana yanayosimikwa katika: ufahamu na ujuzi wa kisayansi; tunu msingi za maisha adili na matakatifu; sanjari na uwajibikaji kwa ajili ya ujenzi wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.