Maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Dunia  kuanzia tarehe 22 Juni hadi 26 Juni 2022 ni fursa ya kutafakari: ukuu, utakatifu; changamoto, matatizo na matumaini ya maisha ya ndoa na familia. Maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Dunia kuanzia tarehe 22 Juni hadi 26 Juni 2022 ni fursa ya kutafakari: ukuu, utakatifu; changamoto, matatizo na matumaini ya maisha ya ndoa na familia. 

Mkutano wa X wa Familia Duniani 2022: Sherehe ya Familia! Yaani!

Maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani kuanzia tarehe 22 hadi 26 Juni, 2022 yananogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” ni wakati muafaka wa kufanya tafakari ya kina kuhusu Wosia wa Kitume wa Papa Francisko: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” yalizinduliwa rasmi tarehe 19 Machi 2021 na yanahitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani mjini Roma, kuanzia tarehe 22 hadi 26 Juni, 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” ni wakati muafaka wa kufanya tafakari ya kina kuhusu Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”. Baba Mtakatifu Francisko anasema, furaha ya upendo inayopatikana katika familia ni furaha ya Kanisa pia. Bado waamini wengi wanataka kufunga ndoa takatifu kwa sababu ni tamko la Kikristo kuhusu familia na Habari Njema kweli! Huu ni wakatiuliokubaliwa wa kutafakari tunu msingi za maisha ya ndoa na familia katika mwanga wa Neno la Mungu, Mapokeo na Mafundisho ya Mama Kanisa.

Uzinduzi wa Sherehe ya Familia kwa mwaka 2022
Uzinduzi wa Sherehe ya Familia kwa mwaka 2022

Ni muda wa kuyaangalia matukio mbalimbali ya maisha, utume na changamoto ambazo familia zinakabiliana nazo katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Waamini na watu wenye mapenzi mema wanahimizwa kumtaza Kristo Yesu, ili kutambua na kuendeleza wito wa ndoa na familia kwa kujikita zaidi katika nyaraka mbalimbali ambazo zimetolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya: Familia, Sakramenti ya Ndoa na Malezi kwa watoto ndani ya familia. Baba Mtakatifu anawaalika wanandoa kukuza na kudumisha upendo unaobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao. Wanandoa wanahimizwa kuendelea kupyaisha upendo huu, ili kuzaa matunda yanayokusudiwa. Arusi ya Kana ya Galilaya ndicho kielelezo kilichochaguliwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha sanjari na Jimbo kuu la Roma, ambalo ni Mwenyeji wa maadhimisho haya! Mtakatifu Paulo Mtume na mwalimu wa Mataifa akitafakari kuhusu upya wa kidugu nyumbani anakaza kusema, “siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari za Kristo na Kanisa”. Ef 5:32. Akiwa kwenye arusi ya Kana, mji wa Galilaya, Kristo Yesu alifanya muujiza wake wa kwanza, kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu amefunga ndoa na watu wake. Hiki ni kiini cha Habari Njema, ingawa wale waliokuwepo arusini, hawakutambua kwamba, kati yao, alikuwepo Mwana wa Mungu, ambaye kimsingi ndiye Bwana arusi.

Muujiza wa Arusi ya Kana ya Galilaya unafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa kwa uwepo wa Kristo Yesu anayejifunua kati ya watu wake kama Bwana arusi, aliyetangazwa na kushuhudiwa na Manabii na kwamba, Yeye ndiye kiini cha Agano Jipya linalojikita katika upendo. Bikira Maria alipogundua kwamba, wanaarusi wanatindikiwa na divai, mara akamwendea Yesu na kumwambia kwamba, “hawana divai” na Yesu akatenda muujiza wake wa kwanza, kwa kugeuza maji kuwa divai. Maandiko Matakatifu yanaonesha kuwa, divai ni sehemu muhimu sana kwenye karamu ya Kimasiha, kwa sababu ni chemchemi ya furaha! Yesu anageuza Sheria ya Musa katika Injili ili kuwakirimia watu furaha ya kweli! Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake ya ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani mjini Roma, Jumatano tarehe 22 Juni 2022, amesikiliza shuhuda, uzoefu na mang’amuzi ya familia zinazoishi katika hali ya wasi wasi; furaha, mateso na matumaini. Ni jambo muhimu kwa wanandoa na familia kuanza hija ya kutembea pamoja kama wanandoa, kama wanafamilia; kutembea pamoja na majirani na Kanisa katika ujumla wake kwa kujikita katika ujirani mwema, huruma, ujirani, ukarimu na mapendo, kwa kuondokana na utamaduni wa kutojali shida na mahangaiko ya wengine.

Msamaha wa kweli upate chimbuko lake katika akili na moyo wa mtu, ili kujenga amani
Msamaha wa kweli upate chimbuko lake katika akili na moyo wa mtu, ili kujenga amani

Ni mwaliko wa kuchukua na kuambata Msalaba, ukweli katika upendo; tayari kusamehe na kusahau. Msamaha ni zawadi ya Mungu kwa wanandoa, inayopaswa kuadhimishwa na familia nzima, pale panapotokea “patashika nguo kuchanika”. Familia zijenge utamaduni wa ukarimu na upendo; kwa kuwathamini na kuwajali jirani. Familia zenye ukarimu na mapendo, ni chemchemi ya furaha, amani, upendo na matumaini kwa jamii. Baba Mtakatifu anawachangamotisha wanandoa kujenga utamaduni wa udugu wa kibinadamu. Wanandoa wanapoishi kwa pamoja, wajenge pia utamaduni wa kuthaminiana na kuaminiana; kwani kila mmoja wao ni zawadi kwa mwenza wake wa ndoa. Furaha na upendo ndani ya familia inajengwa kwa kusikilizana, kupendana na kuthaminiana.

Kardinali Kevin Joseph Farrell, Rais wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika hotuba yake ya utanguzi katika maadhimisho ya Sherehe ya Familia, amesema, kwamba, umati mkubwa wa familia hizi ni kielelezo cha ushirika na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Wawakilishi wa wanandoa waliotoa ushuhuda wao ni kutoka Italia, Ukraine na DRC. Hawa ni wanandoa wenye mambo mema yakujifunza lakini pia wanakasoro zao, kwani hakuna familia ya watu wakamilifu. Lengo la shuhuda hizi ni kunogesha mchakato wa utakatifu wa maisha ya ndoa na familia unaokita mizizi yake katika: upendo, huruma, msamaha, uvumilivu, udumifu; ukweli, uwazi na unyenyekevu.

Wanandoa wale mashuhuda wa Injili ya maisha ya ndoa na familia kwa jirani zao
Wanandoa wale mashuhuda wa Injili ya maisha ya ndoa na familia kwa jirani zao

Naye Prof. Gabriella Gambino Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, kuna haja ya kupyaisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa familia, ili kuwasikiliza wanandoa na kuwajenga matumaini ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu licha ya changamoto wanazopitia katika maisha. Ni fursa ya kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinazokita mizizi yake kwa uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika familia. Sera na mikaka ya shughuli za kichungaji kwa familia ziguse maisha yote tangu maandalizi ya ndoa, mtoto anapotungwa mimba, malezi na makuzi hadi kufikia mtu mzima. Huu ni mchakato wa kuwafunda wanandoa, kuwasindikiza; kuwarithisha imani, ili kuendelea kujikita katika utakatifu wa maisha, kila mtu kadiri ya hali na wito wake. Familia ni kitovu cha elimu ya uraia mwema. Maisha ya ndoa na familia ni kielelezo cha: Ukuu, uzuri, utakatifu na ushuhuda wa Injili ya familia unaobubujika kutoka katika sura na mfano wa Mungu. Ndani ya familia kuna matatizo na changamoto zake, lakini waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Sherehe ya familia 2022

 

 

24 June 2022, 15:41