Papa Francisko:Ekaristi ni mwaliko wa kupeleka Mungu katika maisha kila siku!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya Katekesi ya Papa Fransisko JUmatano tarehe 15 Juni 2022 akitoa salamu zake kwa mahujaji waliokuwapo katika Uwanja wa Mtakatifu Petro Vatican, amezungumzia siku kuu ya Corpus Domini yaani 'Mwili na Damu ya Yesu Kristo' itakayoadhimishwa Alhamaisi 16 Juni 2022 mjini Vatican. Kardinali Mauro Gambetti, Mkuu wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Vatican ataongoza maadhimisho ya kiliturujia ya Sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, katika Altare ya Kanisa kuu, Saa 4.30 asubuhi.
Kwa maana hiyo Papa Francisko akizungumza kwa wanaozungumza lugha ya kijerumani amewaalika kuwa: “Sherehe ya Corpus Domini inatoa mwaliko wa kutoka nje ili kumpeleka Bwana katika maisha ya kila siku. Hasa kwa kumpeleka mahali ambapo maisha hujifunua pamoja na furaha na mateso yake yote" Papa Francisko vile vile pamoja na mahujaji wanaozungumza Kihispania, ameongeza kutoa mwaliko wa "kumwomba Mungu ili atujalie kuwa watu wa 'Ekaristi', tunashukuru kwa zawadi tuliyopokea na uwezo wa kujitoa kwa wengine kwa kutumikia kwa furaha; hasa wale ambao wanahitaji zaidi”.
Uzoefu wa upendo wa Mungu katika Mwili na Damu ya Kristo
Hata kwa mahujaji wa Poland, Papa Francisko ameeleza kwamba katika Maadhimisho ya Siku Kuu ya Mwili na Damu Takatifu ya Kristo, uwepo halisi wa Mungu katika Ekaristi kwa namna ya mkate na divai unakumbukwa na matumaini hata na tamasha la Uinjilishaji kwa maana matukio yanayofanyika nchini Poland ili yaweze kwa hakika kuamsha imani kwa wote na ili kwa kupokea Mwili na Damu ya Kristo waweze kuonja upendo wake kwa undani zaidi. Hatimaye Papa Francisko amekumbusha kwamba, nchini Italia maadhimisho ya Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Kristo itaadhimishwa Dominika ijayo na kwamba "Ekaristi, fumbo la upendo, liwe kwao wote chemchemi ya neema na mwanga unaoangazia mapito ya maisha, msaada kati ya shida, faraja ya hali ya juu katika mateso ya kila siku".